Wednesday 24 June 2015

Zigo la JK Kigoma kwa rais ajaye

           Zigo la JK Kigoma kwa rais ajaye


Mji wa Kigoma unavyoonekana ,miongoni mwa ahadi zilizotolewa na JK 2010 ni kuigeuza Kigoma kuwa sasa Dubai .Picha ya Maktaba. 
Na Anthony Kayanda
Kwa ufupi
Kutokana na changamoto hizo, Rais Jakaya Kikwete alipokuwa anaomba kura ili achaguliwe tena mwaka 2010 aliahidi kutekeleza baadhi ya mambo na hilo lilichangia kumpa kura zaidi ya 10,000 kutoka Mkoa wa Kigoma na kumfanya aongoze kwa kuwazidi wagombea wengine, hasa mpinzani wake mkuu Dk Willibrod Slaa wa Chadema.



Kigoma. Mkoa wa Kigoma upo Magharibi ya Tanzania ikiwa ni mojawapo ya mikoa iliyobatizwa jina la ‘pembezoni’ kutokana na umaskini unaowakabili wakazi wake walio wengi, lakini pia kwa miaka mingi umekuwa na changamoto ya miundombinu mibovu ya barabara, usalama wa raia kutokana na ujambazi.
Kutokana na changamoto hizo, Rais Jakaya Kikwete alipokuwa anaomba kura ili achaguliwe tena mwaka 2010 aliahidi kutekeleza baadhi ya mambo na hilo lilichangia kumpa kura zaidi ya 10,000 kutoka Mkoa wa Kigoma na kumfanya aongoze kwa kuwazidi wagombea wengine, hasa mpinzani wake mkuu Dk Willibrod Slaa wa Chadema.
Alitoa ahadi nyingi tu kama vile ujenzi wa barabara, ujenzi wa kiwanja cha ndege, ujenzi wa daraja la mto Malagarasi, ujenzi wa reli mpya ya kati, kuimarisha ulinzi na usalama Ziwa Tanganyika, kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Maziwa Makuu na kuhakikisha kuwa Kigoma inaunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa.
Barabara
CCM iliahidi kujenga barabara ya Kigoma hadi Nyakanazi yenye urefu wa kilomita 330 kwa kiwango cha lami. Barabara hiyo imekuwa haitengenezwi kwa madai ya ukosefu wa fedha, jambo ambalo limesababisha adha kubwa kwa wasafiri hususani kipindi cha mvua nyingi ambapo magari makubwa hukwama na kuziiba.
Hata hivyo, ujenzi wa barabara hiyo umeanza na kwa upande wa Kigoma kuna mkandarasi kutoka China anayejulikana kwa jina la CR 15 Group chini ya Mkandarasi Mshauri, DOCH Limited ya Dar es Salaam ambapo inadaiwa amepewa kipande cha kilomita 50 ajenge kwa kiwango cha lami.
Wameanza kuchimba barabara kuanzia kijiji cha Kasangezi hadi Muzye, umbali wa kama kilomita tano hivi ikiashiria kwamba ndiyo ujenzi unaanza rasmi, lakini kasi ndogo ya ujenzi inatia shaka kama kweli serikali ina nia ya dhati kukamilisha ujenzi huo au inatumika kama kampeni ili kupata kura kwa mgombea atakayepitishwa na CCM.
Kwa upande wa Barabara ya Kigoma hadi Manyoni mkoani Singida yenye urefu wa zaidi ya kilomita 600 imeanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Utekelezaji wake umekamilika kwa zaidi ya asilimia 50.
Licha ya kwamba ujenzi wake haujakamilika kwa maana ya kwamba unaweza kutokaa Kigoma hadi Manyoni kwa lami, lakini maeneo makubwa yamewekwa tabaka la lami, jambo lililofanya baadhi ya mabasi yaanze kutumia barabara hiyo kuanzia Kigoma kwenda Dar es Salaam na kabla ya hapo walikuwa wanatumia barabara ya Kigoma kupitia Nyakanazi, Kahama, Singida na hatimaye kutokea Manyoni.
Kiwanja cha ndege Kigoma
Rais aliahidi kujenga kiwanja kitakachowezesha ndege aina ya Boeing kutua Kigoma ili kurahisisha usafiri kati ya nchi za Burundi, Kongo DRC na Rwanda.
Ilitarajiwa kiwanja hicho kiwe na njia ya kurukia ndege yenye urefu wa mita 3,000 (sawa na kilomita 3) lakini ujenzi wake umekamilika kwa kujengwa mita 1720 kwa kiwango cha lami, urefu ambao hauwezi kutumiwa na ndege aina ya Boeing zilizolengwa kutua hapo kwa ajili ya kubeba bidhaa kupeleka Ulaya na pia kutoa Ulaya kuzileta hapa ikiwa ni pamoja na zile zinazopaswa kwenda Mashariki ya Kongo ambao zaidi wanategemea bidhaa kutoka Kigoma.
Kiwanja hicho kimeingia kwenye mgogoro na baadhi ya wakazi wa kata za Majengo na Machinjioni waliotakiwa kuhama ili kupisha ujenzi huo, lakini wakakataa kuhama wakidai kuwa fidia waliyolipwa ni ndogo ikilinganishwa na gharama halisi za maisha ya sasa.
Uthamini wa mali zao ulifanywa mwaka 2006 lakini wamekuja kulipwa fedha mwaka 2013, miaka saba baadaye tena kwa thamani ya mwaka huo wa 2006, wakati utaratibu upo wazi kwamba ikipita miezi sita kabla mtu hajalipwa fedha baada ya kufanyiwa uthamini wa mali, inatakiwa zoezi la uthamini lirudiwe upya ili mtu alipwe fedha kulingana na wakati uliopo, lakini hilo halikufanyika.
Hiyo imekuwa changamoto kubwa na ahadi ya Rais Kikwete inaonekana kukwama na hakuna dalili za wazi kuonyesha kwamba mradi huo utatekelezwa kabla ya Novemba, 2015 atakapokabidhi madaraka kwa rais ajaye.
Umeme wa Gridi ya Taifa
Mkoa wa Kigoma haujafanikiwa kuunganishwa kupata umeme wa gridi ya Taifa na badala yake wakazi wake wanatumia umeme unaozalishwa kwenye jenereta za kufua umeme na serikali ilikwama kutekeleza ahadi yake ya kuiunganisha Kigoma na umeme ulioishia Kaliua mkoani Tabora au Kahama mkoani Shinyanga.
Kitovu cha biashara
Rais Kikwete aliahidi kwamba atahakikisha mji wa Kigoma unakuwa kama Dubai kwa maana kwamba unageuzwa kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wote huu wa nchi za Maziwa Makuu ambazo badala ya kwenda kufuata bidhaa Dubai na China, wangelazimika kuja Kigoma kununua bidhaa hizo.
Hadi sasa hakuna jitihada zozote za makusudi zinazoonekana kutekeleza ahadi hiyo na badala yake mji unazidi kuchoka na maisha ya wakazi wengi wa Kigoma yanazidi kuwa magumu.
                                                             habari kutoka gazeti la mwananchi:

No comments:

Post a Comment