Saturday, 4 July 2015

Majambazi yachakaza gari la polisi kwa risasi

 
Kwa ufupi
Majambazi hayo pamoja na askari polisi waligeuza mtaa huo kuwa eneo la mapambano baada ya kutupiana risasi kwa zaidi ya dakika 15, huku jambazi moja likiuawa kwa kupigwa risasi na askari waliokuwa kwenye mpambano huo.
SHARE THIS STORY
0
Share


Mwanza. Ilikuwa kama sinema, lakini ndivyo ilivyokuwa, majambazi yamelichakaza gari la polisi kwa risasi wakati wakijiandaa kufanya uhalifu eneo la Nyegezi mkoani Mwanza.
Tukio hilo ambalo lilikuwa la aina yake lilitokea kwenye Kata ya Nyegezi, Mtaa wa Igubinya Wilaya ya Nyamagana mkoani hapa.
Majambazi hayo pamoja na askari polisi waligeuza mtaa huo kuwa eneo la mapambano baada ya kutupiana risasi kwa zaidi ya dakika 15, huku jambazi moja likiuawa kwa kupigwa risasi na askari waliokuwa kwenye mpambano huo.
Tukio hilo lilitokea jana saa sita mchana karibu na Kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), iliyopo Nyegezi Kona.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema majambazi hao walianza kuonekana saa 3:00 asubuhi, wakipita kwenye eneo hilo kila wakati na kuanza kuwatilia shaka.
Tukio hilo lilizua taharuki baada ya milio ya risasi kuanza kusikika, hali iliyosababisha wapita njia na wafanyabishara kuhaha na kukimbia huku na kule bila kujua kitu gani kimetokea.
Kati ya majambazi hayo alikuwemo mwanamke, ambaye naye alionekana akitupiana risasi na polisi kabla ya kukimbia kwa kutumia usafiri wa pikipiki, baada ya kuzidiwa nguvu na askari hao.
Wanajeshi pia walionekana kufurika kwenye eneo hilo, ambao nao walikuwa wanashuhudia kinachoendelea. Baada ya kuzidiwa nguvu majambazi mawili yalikimbia pembezoni mwa eneo la kambi ya jeshi, jambo lililoelezwa kuwa walikuwa wageni.
Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo, Emmanuel John alisema; “Watu hawa walianza kuonekana tangu asubuhi, tuliwatilia shaka, hatukujua wanataka kuiba wapi, lakini baada ya kujua tumewagundua na kwakuwa polisi walikuwa karibu, walikuja ghafla tukaanza kusikia milio ya risasi hewani.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa watu hao ambao walikuwa watatu walifanikiwa kukimbia baada ya kutupiana risasi na polisi, huku mmoja wao akiuawa baada ya kupigwa risasi ya paja.
Alisema polisi waliliua jambazi moja ambalo walilikuta na silaha aina ya SMG ikiwa risasi 19 ambazo hazijatumika pamoja na maganda ya rasasi 23 zilizotumika katika mapambano hayo.
“Nikweli kumetokea tukio la majambazi ambayo yalikuwa yanazunguka zunguka eneo la Nyegezi kona Mtaa wa Igubinya, walitiliwa shaka na watu wa kawaida baada ya kuwahoji,” alisema Mkumbo na kuongeza:
“Kwa bahati nzuri polisi tayari walikuwa wameweka mtego na walikuwa wamefika kwenye eneo hilo na kuyafuatilia. Majambazi hayo yalianza kupiga risasi, jambo ambalo polisi walikabiliana nalo na kuweza kuwadhibiti.”
Alisema jambazi mmoja aliuawa baada ya kupigwa risasi na wengine watatu wakakimbia, polisi inaendele kuwatafuta ili kuhakikisha wanakamatwa.
Mkumbo alisema gari lao aina Land Rover Defender liliharibiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi, lakini hakuna askari aliyejeruhiwa kutokana na tukio hilo.
Eneo la Nyegezi limekuwa na matukio kadhaa ya uharifu ,ambapo mwaka jana matukio mawili yalitokea katika eneo hilo.
                                     Habari na: http://www.mwananchi.co.tz