Saturday 20 June 2015

ALIYETEKA ALBINO TABORA AFUNGWA JELA MIAKA 10

ALIYETEKA ALBINO TABORA AFUNGWA JELA MIAKA 10

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Juma Bwire akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo Juni 16, 2015.
Masanja Mwinamila (44) mara baada ya kufikishwa katika kituo cha Polisi Wilaya ya Nzega Juni 15, 2015.
Na Daniel Mbega, Nzega

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Nzega leo hii imemhukumu Masanja Mwinamila (44), mkazi wa Kitongoji cha Kona Nne, Kijiji cha Ugembe II, Kata ya Mwakashanhala, Tarafa ya Puge wilayani Nzega katika Mkoa wa Tabora kwenda jela miaka 10 kwa kosa la kuteka mtoto mwenye albinism, Margreth Hamisi (6).

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Saraphine Nsana, alitoa hukumu hiyo baada ya mshtakiwa kusomewa shtaka na kukiri kutenda kosa hilo.

Ilielezwa mahakamani hapo kwamba, mnamo Juni 15, 2015 majira ya saa 3:00 usiku katika Kijiji cha Ugembe II, Kata ya Mwakashanhala wilayani Nzega, mtuhumiwa alimteka binti huyo kwa lengo la kwenda ‘kumuuza’ ili ajipatie fedha (kiasi kimehifadhiwa).

Hii ni mara ya kwanza kwa kesi inayohusisha utekaji nyara, kujeruhi na mauaji dhidi ya watu wenye albinism kuchukua muda mfupi zaidi, kwani ndiyo kwanza kesi hiyo ya Jinai Namba 116/2015 imefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kutolewa hukumu.

Jitihada za Polisi

Mafanikio ya kukamatwa kwa Masanja Mwinamila akiwa katika harakati za kutaka kumuuza mtoto Margreth Hamisi, ambaye ni mpwa wake, yametokana na umakini wa Jeshi la Polisi nchini ambapo maofisa wake wa Kikosi Kazi cha Taifa waliweka mtego na kufanikiwa kumnasa mtuhumiwa kabla hajamdhuru mateka wake.

Tukio hilo limefanikisha kuubomoa mtandao hatari wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwani ni takriban wiki tatu tu tangu maofisa usalama walipofanikiwa kuwanasa watu wengine sita wakiwa katika harakati za kuuza mifupa inayodhaniwa kuwa ya binadamu (albino) mjini Kahama Mei 22, 2015 ambapo tayari wamekwishafikishwa mahakamani pamoja na wengine watatu waliokamatwa baadaye.

Matukio hayo mawili makubwa yaliyotokea katika kipindi hicho yamedhihirisha namna serikali kupitia jeshi hilo na vyombo vingine vya usalama inavyoshughulikia mitandao hiyo hatari usiku na mchana ili kuhakikisha Watanzania wote wanaishi kwa amani na usalama.


Kukamatwa na hatimaye kuhukimiwa kwa Masanja Mwinamila kumedhihirisha kwamba matukio mengi ya kuuawa au kujeruhiwa kwa watu wenye albinism yanapangwa na kufanikishwa na wanandugu wenyewe kwa sababu ya mawazo potofu ya kutafuta utajiri kwa njia za mkato.

Kama alivyoeleza Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP. Juma Bwire, Juni 16, 2015, Masanja alithubutu kwenda kumnyakua mtoto huyo Margret Hamisi (6) majira ya saa 3 usiku na kukimbia naye gizani akiwa na lengo la kumuuza ajipatie utajiri.

Lakini habari kutoka eneo la tukio zinaeleza kwamba, haikuwa kazi rahisi kwa wanausalama kumwokoa binti huyo akiwa hai na kumtia mbaroni mtuhumiwa, kwani walilazimika kujifanya ‘wanunuzi’ ili kuweka mtego wa kumkamata mtuhumiwa na kumwokoa mateka.

Taarifa za uchunguzi zinaeleza kwamba, mtuhumiwa huyo alianza mchakato wa kutafuta ‘soko’ la kumuuza mtoto wa dada yake mapema mwezi Juni 2015, lakini wasamaria wema wakawaarifu wanausalama kuhusu kinachotaka kutokea katika eneo hilo.

Ilibidi maofisa wawili wa usalama wapangiwe kazi ambapo mmoja alijifanya mnunuzi na mwingine mganga wa jadi anayeambatana na ‘tajiri’ huyo feki ambao walikutanishwa na mtuhumiwa huyo aliyewaeleza kwamba ‘dili la albino lipo’.

“Alisema kuna dada yake mwenye albinism ambaye ana watoto wawili – wa kiume na wa kike – ambaonao wana albinism, huyo dada ni mtoto wa baba yake mdogo ambaye alifariki mwaka jana (2014), hivyo nyumbani hakuna mtu wa kiume wa kuleta upinzani.

“Akasema kwamba biashara hiyo ingefanyika sana, kwani alipanga kuanza kumuuza mtoto wa kike, halafu angemuuza yule wa kiume na hatimaye kummalizia dada yake!” kilisema chanzo cha ndani kutoka eneo la tukio.

Kwa kawaida asilimia kubwa ya wakazi wa Kanda ya Ziwa ni wapagani na wanawaamini waganga wa jadi kuliko mtu yeyote, hiyo alipokutanishwa na watu hao wawili, mtuhumiwa Masanja Mwinamila aliamini kila alichoambiwa na ‘mganga’.

Mganga huyo feki, mbali ya kumpigia ramli na kumwogesha dawa kwenye njiapanda, alimtaka mtuhumiwa kuleta mtoto huyo akiwa hai kwa maelezo kwamba inabidi ‘afanye tambiko ili dawa zifanye kazi’, lakini lengo likiwa kumzuia mtuhumiwa asimdhuru mtoto na hivyo kupata nafasi ya kumwokoa.

Akiwa na shauku kubwa ya kupata mamilioni ya fedha, baada ya kukubali masharti ya mganga, Masanja alimuomba ‘tajiri’ atafute bunduki ili wakati yeye atakapomnyakua mtoto, wafyatue risasi hewani kuwatisha watu watakaokimbilia eneo la tukio mara yowe litakapopigwa.

Taarifa zinasema, wanausalama waliposikia kauli hiyo wakahisi mtuhumiwa angeweza kwenda hata na panga na kuwajeruhi watu atakaowakuta eneo la tukio ili amchukue mtoto, hivyo mganga huyo akatoa masharti kwamba hata kama bunduki itapatikana, lakini asingependa kuona damu inamwagika kwa yeyote huku akimwaminisha kwamba dawa atakazoogeshwa zitamfanya awe ‘kiza’ asionekane na mtu yeyote.

Takriban mara tatu zoezi hilo liliahirishwa kwa kuangalia mazingira ya kiusalama, lakini baada ya wanausalama kujipanga vyema, ndipo Juni 15, 2015 wakafanikisha mtego huo na kumkamata mtuhumiwa akiwa amembeba mtoto ambaye alinyakuliwa akiwa usingizini.

“Ilikuwa ni kazi ngumu, lakini kama siyo imani kwa mganga, ingekuwa hatari sana hata kwa wanausalama wenyewe. Jamaa alipewa masharti kwamba, mtoto huyo anayeuzwa anatakiwa afikishwe kwa mganga akiwa hai bila kujeruhiwa mahali popote; Familia itakayovamiwa pia isimwage damu; Fedha za manunuzi kabla ya kukabidhiwa mlengwa lazima zifanyiwe tambiko na masharti ya matumizi; hakutakiwa kufanya zianaa siku nne kabla ya tukio; na lazima kuogeshwa dawa wale wote watakaokwenda kwenye tukio,” kilifafanua chanzo kingine.

Bi. Joyce Mwandu Nkimbui (33), ambaye ni mama wa Margret, anasema siku tatu mfululizo kabla ya tukio, mtuhumiwa huyo ambaye ni kaka yake anayeishi jirani na hapo alikuwa akija asubuhi na jioni akijifanya kuja kusalimia na wakati mwingine hata kupikiwa chakula.

Hata hivyo, alishangaa kukuta kwamba ndiye aliyevamia nyumbani kwao usiku wa Juni 15, 2015 na kumwamuru asikimbie kabla yeye hajaingia ndani na kumkwapua mtoto.

“Walikuja usiku, sijui walikuwa wangapi, lakini wakanilazimisha ‘wewe mama tulia’, nikaogopa na kukimbilia kwenye majani, nikaanguka kwa sababu sioni vizuri usiku, nikakutana na mwenyekiti wa kitongoji, ambaye tulikwenda naye nyumbani na kukuta tayari mtoto hayupo,” Joyce alisema kwa masikitiko.

Matukio mbalimbali

Tangu mwaka 2006 serikali imekuwa ikipambana na matukio ya kuuawa na kujeruhiwa kwa watu wenye albinism nchini, ambapo tayari watu zaidi ya 10 wamehukumiwa kunyongwa, wengine kesi zao ziko mahakamani na watuhumiwa wengine wanaendelea kusakwa kwa kuhusika na matukio hayo ya kutisha.

Wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya wenye albinism duniani jijini Arusha Juni 13, 2015, Rais Jakaya Kikwete alisisitiza kuwa kati ya watu 13 waliohukumiwa kunyongwa wawili kesi zao zipo katika hatua ya mwisho kufikishwa kwake na kuahidi zitakapofika mezani kwake atazitendea haki stahiki.

"Lakini mwaka 2014 hadi 2015 serikali tumepambana na watu wakatili dhidi ya walemavu kwa kuwakamata watu 25 kati yao sita kesi zao zipo mahakamani, huku watano upelelezi unaendelea na 11 wameachiwa huru kwa kutopatikana na hatia," alisema.

Rais Kikwete pia aliwahakikishia wenye albinism kupatiwa vifaa vya kupambana na kansa ya ngozi bure kwenye hospitali za serikali.

Mwaka 2009, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliangua kilio bungeni kuonyesha uchungu alionao dhidi ya vitendo vya mauaji ya kikatili ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), na machozi yake yakayeyusha hoja ya wabunge wa upinzani waliokuwa wamepania kumbana, ili ajiuzulu kwa madai kwamba, alitoa amri ya kuua wauaji ambayo ni kinyume na katiba ya nchi.

Habari na  http://rweyunga.blogspot.com