Tuesday, 21 July 2015

Wabunge wa Chadema wamkaribisha Lowassa

Wafuasi wa Chadema wakiwa katika moja ya
Wafuasi wa Chadema wakiwa katika moja ya mikutano ya hadhara ya chama hicho. Picha na Maktaba 
By Florence Majani, Mwananchi
Dar es Salaam. Baadhi ya wabunge wa Chadema wamezungumzia taarifa zinazosambaa zikieleza kuwapo mkakati wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhamia katika chama hicho, wengi wao wakimkaribisha.
Wakati wabunge hao wakikubali kumpokea, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa amesema wananchi wasubiri mambo yatakapokuwa tayari badala ya kutegemea mitandao ya kijamii.
“Nitazungumza pale mambo yatakapokuwa sawa, siwezi kuzungumza sasa, subirini… sasa hivi mambo mengi yanazungumzwa kwenye mitandao,” alisema Dk Slaa ambaye pia anatajwa kuwa mgombea wa chama hicho ndani ya Ukawa.
Msemaji wa Lowassa, Aboubakary Liongo alipoulizwa kuhusu kuwapo kwa mpango huo alisema hawezi kulizungumzia hilo kwa kuwa ni suala la mtu binafsi. Hata hivyo, jitihada za kumpata Lowassa jana hazikufanikiwa kwani simu yake iliita pasi na kupokewa.
Hivi karibuni, idadi kubwa ya madiwani wa CCM walirudisha kadi zao na kujiunga na Chadema wakisema sababu ni kutoridhishwa na kukatwa kwa jina Lowassa kati ya wagombea urais wa CCM.
Kadhalika, mtandao wa kijamii uliokuwa ukimuunga mkono mbunge huyo wa Monduli unajulikana kwa jina la 4U Movement ulitangaza kuhamia Chadema hali inayoashiria kuwa kuna dalili ya Lowassa pia kujiunga nao.
Wakiandika katika akaunti ya Twitter ya 4U Movement, wafuasi hao walisema: “Ukimya ni hekima na ukimya ni busara. Ukimya wa Edward Lowassa ni kutafakari Safari ya Matumaini... Tuungane kuyapata mabadiliko nje CCM.”
Chadema ni kanisa la wokovu
Akizungumzia taarifa hizo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alikifananisha chama hicho na kanisa ambalo kwa kawaida halikatai mtu, bali linawapokea wenye dhambi na kuwaongoza kufanya toba.
“Chadema ni kama kanisa, hakataliwi mtu, tunahubiri habari njema ya wokovu, ukija hapa unatubu unaendelea kufanya kazi,” alisema.
Kuhusu viongozi wa CCM kuhamia Chadema, Msigwa alisema inawezekana kasi hiyo inachagizwa na Lowassa kukosa nafasi aliyoitaka ndani ya chama hicho.
“Unapokuwa mwanasiasa unakuwa na wafuasi, inawezekana wengine wanaohamia Chadema ni watu wake ambao wameona mtu wao amekosa nafasi aliyoitaka ndiyo maana wanakihama chama,” alisema.
Msigwa alisema Chadema ilikuwa inakusanya wanachama wapya kwa muda mrefu hata kabla ya vuguvugu la Lowassa na chama chake kuibuka na ushindi na wanaohamia wanafanya hivyo kwa sababu wanakipenda chama na wameichoka CCM.
Huenda akatimiza safari ya matumaini
Akizungumzia ujio wa Lowassa kwenye chama hicho, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema iwapo Lowassa atahamia Chadema anakaribishwa na huenda akaitimiza safari yake ya matumaini.
“Namkaribisha Lowassa Chadema, huenda safari yake ya matumaini ikaishia huku, akawa mwanachama au hata kiongozi,” alisema.
Alisema hakuna shaka kuwa mbunge huyo wa Monduli ana nguvu ndani ya CCM ndiyo maana viongozi wengi wa chama hicho wanakihama wakati huu.
“Hiyo ilijionyesha kuanzia kwenye Kamati Kuu ya CCM, Halmashauri Kuu, Lowasa amekamata wajumbe kwa asilimia 80 na hiyo ni ishara kuwa ameishika CCM,” alisema.
Lema aliongeza kuwa wanaoihama CCM hawaihami kwa bahati mbaya, bali wameona mtu wao waliyemtarajia ameondoka.
“Ni wengi wanaohamia Chadema, kwa sasa kadi zimetuishia na hiyo ni ishara kuwa CCM inakufa, ripoti za mikoa yote tunazo,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya alisema  wanaoihama CCM kwa sasa wamegundua kuwa chama pekee kinachoweza kutetea wananchi ni Chadema.
“Sisi tunawakaribisha kwa mikono miwili, waje tuchape kazi, ilimradi wanafuata kanuni na taratibu za chama, basi.  Wamejionea wenyewe kuwa CCM hakuna chochote,” alisema.
 Alisema CCM waliamua kupitisha katiba bila kuwapo kwa Ukawa, lakini sasa wameona kuwa walichokifanya ni makosa na wameanza kurudi Chadema ambako wanaamini kuna demokrasia ya kweli.
Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Paresso alisema: “Tunamkaribisha kwa mikono miwili. Tumekinyooshea CCM vidole kwa muda mrefu kuwa kuna rushwa na makundi na hilo linajidhihirisha sasa. Lakini wale wote wanaokuja Chadema, tunawakaribisha ili mradi wafuate kanuni na taratibu zetu.”
Paresso alisema hana tathmini ya kina kuhusu wafuasi wa Lowassa wanaoihama CCM, bali wanaokihama chama hicho wameona kina matatizo.
Atakiwa akidhi vigezo na masharti
Licha ya kuonyesha kumkaribisha, katika chama hicho, baadhi ya wabunge walimtaka Lowassa afuate kanuni ili awe mwanachama mwenye sifa.
Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde alisema anakaribishwa lakini hana budi kufuata sheria na kanuni za chama... “Anatakiwa afuate taratibu za chama, milango ipo huru, lakini afuate kanuni… asije akafikiri ataleta taratibu zake hapa, sitakubali.”
Silinde alisema wanaohamia Chadema hawajapendezwa na mwenendo mzima wa uteuzi wa mgombea wa urais na hivyo wameifuata demokrasia ya kweli ndani ya chama hicho.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo lakini alisema endapo atajiunga, chama hicho kitampokea kulingana na vigezo na taratibu.
“Akihamia Chadema nitatoa maoni yangu lakini ninachoweza kusema ni kuwa kila mtu ana haki ya kwenda chama chochote ili mradi ana tija,” alisema.
Mdee alisema wanaCCM wanaohamia Chadema wamesoma alama za nyakati na kuona kuwa CCM haiendani na ahadi zake.
Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo alisema, Lowassa ni binadamu wa kawaida kwa hiyo kuhamia kwake Chadema si kitu cha ajabu ilimradi afuate kanuni... “Cha muhimu afuate masharti ya chama, kanuni na  taratibu, kama watu wanahama vyama vingine yeye ni nani asihame CCM?”
Lyimo alisema wanaCCM wengine wanakaribishwa kujiunga kwa sababu kwenye siasa hakuna rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu.
Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul, aliwataka wana CCM na Lowasa kuhamia zaidi  Chadema ili kuunganisha nguvu na kuichukua nchi.
 “Mfikishie salamu Lowassa mwambie karibu kwenye jeshi la ukombozi,” alisema.
Katibu wa CCM amuonya
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Ofisi za CCM Mkoa wa Dodoma, Katibu wa CCM mkoa huo, Albert Mgumba alisema ingawa kuhama chama ni hiari ya mtu, Lowassa hapaswi kuchukua uamuzi wa hasira kiasi hicho badala yake awe mstari wa mbele kuhamasisha umoja ndani ya chama.
Alimtaka kutothubutu kuihama CCM na endapo afanya uamuzi huo atambue kuwa hawezi kukisababishia pengo lolote zaidi ya kujipunguzia hadhi yake ya kisiasa.
“Mgombea tuliyempata sasa ni makini kuliko, anapendwa, utendaji wake unajulikana kila mahali,” alisema Mgumba.
Mgumba alisisitiza kuwa badala ya Lowassa kuwa na mawazo ya kuihama CCM, anapaswa kutuliza fikra na kuonyesha ukomavu wake kisiasa kwa kuwa mstari wa mbele kuwaonya na kuwatuliza wote waliokuwa wakimuunga mkono ili wabaki kwa utulivu ndani ya chama na si vinginevyo.
“CCM siyo Mgumba, ni taasisi iliyosimama. Lowassa anapaswa kutambua hilo, atulie na awe mstari wa kwanza kuwaonya wanachama wachanga kisiasa, wasiokuwa na uzalendo ndani ya chama kwa kumfikiria mtu badala ya chama na masilahi ya Taifa” alisema Mgumba.
Habari na: http://www.mwananchi.co.tz