Monday 22 June 2015

Mwanamke Mtanzania adakwa na kilo 74 za unga

Mwanamke Mtanzania adakwa na kilo 74 za unga

 
Na Pamela Chilongola
Kwa ufupi
Mwanamke huyo, Chambo Fatuma Basil alikamatwa na Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha India kilichopata taarifa za kuwapo kwa mtu huyo ambaye alikutwa na hati ya kusafiria ya Tanzania.

Dar es Salaam. Matukio ya Watanzania kukamatwa nje ya nchi wakiwa na dawa za kulevya zilizopigwa marufuku yanazidi kukithiri baada ya mwanamke mmoja kukamatwa na kilo 74 za dawa aina ya ephedrine kwenye Uwanja wa Ndege wa Mumbai, India.
Mwanamke huyo, Chambo Fatuma Basil alikamatwa na Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha India kilichopata taarifa za kuwapo kwa mtu huyo ambaye alikutwa na hati ya kusafiria ya Tanzania.
Kwa mujibu wa tovuti ya hindustantimes.com limewanukuu maofisa wa Idara ya Uhamiaji wa India, Kitengo cha Intelijensia cha Uwanja wa Ndege (AIU) wakisema Chambo alithibitishwa Mtanzania baada ya kufanyia ukaguzi na kukibainisha kuwa kiwango alichokutwa nacho ni kikubwa kulivyo mzigo wowote wa dawa za kulevya uliowahi kukamatwa kwenye uwanja huo wa ndege.
Maofisa hao walisema walimnasa mwanamke huyo baada ya kudokezwa na kufuatilia taarifa ya abiri huyo aliyekuwa akielekea Dar es Salaam kupitia Doha, Qatar.
“Mtuhumiwa alikamatwa saa 7:00 mchana. Mbwa maalum alielekezwa kukagua mizigo yake iliyokuwa inaingizwa chini ya ndege na akatoa ishara chanya,” alisema Milind Lanjewar, kamishna wa ziada wa ushuru wa Uwanja wa Ndege.
Mizigo yake mitatu ilikuwa imewekwa pakiti za unga mweupe unaosadikiwa kuwa wa methaqualone au mandrax, dawa ambayo hutumiwa kama mbadala wa cocaine, imeandika tovuti hiyo.
Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema kwa kuwa mwanamke huyo amekamatwa nchini India, Tanzania haiwezi kuingilia kwa undani ingawa wanasubiri iwapo India watawapigia simu.
“Kila nchi ina sheria yake na ina uwezo wa kumchukulia hatua Fatuma kwa kuwa yupo ndani ya nchi hiyo,”alisema.
Nzowa alisema nchi nyingi duniani zipo kwenye vita dhidi ya dawa za kulevya hivyo hashangai kwa Mtanzania huyo kukamatwa nchini India.
Nzowa alisema dawa hizo ni kemikali au vibashirifu vinavyotumika kutengeneza dawa za kulevya na huzalishwa zaidi India.
Alisema ephedrine zinatumika kutengenezea dawa za kikohozi lakini kinachojitokeza watu wanabadilisha matumizi yake na kutengeneza dawa za kulevya.
Nzowa alisema aina hiyo ya vibashirifu inalimwa kihalali nchini India kwa vibali maalumu kwa ajili ya kutengenezea dawa ya kikohozi .