Saturday 30 November 2013

SAMATTA AFUNGA, LAKINI SFAXIEN YAIUA MAZEMBE DAKIKA YA 88 LUBUMBASHI, WAMKOSA MWALI WA CAF HIVI HIVI!

MSHAMBULIAJI Mbwana Ally Samatta na Thomas Emanuel Ulimwengu leo wameshindwa kutimiza ndoto zao za kuwa Watanzania wa kwanza kuvaa Medali za Dhahabu za michuano ya Afrika baada ya klabu yao, Tout Puissant Mazembe kushinda 2-1 dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia, katika fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, hivyo kuangushwa kwa matokeo ya jumla ya 3-2, baada ya awali kufungwa 2-0 Uwanja Olympique de Rades mjini Tunis katika Fainali ya kwanza.
 




Mazembe ilitakiwa kushinda mabao 3-0 leo nyumbani ili kutwaa taji hilo, na ilionekana kama ingeweza kufanya hivyo baada ya kuongoza kwa mabao 2-0 hadi dakika ya 88, yaliyofungwa na nyota wa Mali, Traore Cheibane dakika ya 10 na Samatta dakika ya 24. Lakini wakati Mazembe wakiwa bize na mashambulizi ya kusaka bao la tatu dakika za lala salama, Ben Youssef akaifungia bao muhimu Sfaxien dakika ya 88 na kuzima ndoto za akina Samatta kuvaa Medali za Dhahabu za Kombe la Shirikisho. Katika mchezo wa kwanza, mabao yaliyoizamisha Mazembe yalifungwa na washambuliaji wa kimataifa wa Gabon, Ibrahim Didier Ndong aliyefunga bao la kwanza dakika ya 16 na mshambuliaji Taha Yassine Khenissi aliyefunga la pili dakika ya 90 na ushei wakimtungua kipa mahiri, Robert Muteba Kidiaba. Washambuliaji wote wa Tanzania, Samatta na Ulimwengu walianza katika kikosi cha Mazembe pamoja na Tressor Mputu Mabi, lakini hawakuweza kuwanusuru mabingwa mara nne Afrika na kipigo hicho. Sfaxien, timu pekee iliyoshinda Kombe la Shirikisho mara mbili tangu kutambulishwa kwa mfumo mpya mwaka 2004, yenye maskani yake katika mji uliozungukwa na bahari ya Mediterranean, Sfax kwa ushindi huo itazawadiwa kitita cha dola za Kimarekani, 625 000, wakati Mazembe watapata dola 432 000.  Sfaxien pia watamenyana na mabingwa wa Ligi ya Mabingwa, Al Ahly ya Misri kuwania taji la Super Cup mechi itakayopigwa nchini Misri Februari 2014.  
 
Wachezaji waliokuwa wakiunda kikosi cha Simba SC mwaka 1993 walivalishwa Medali za Fedha pia na Rais mstafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi baada ya kufungwa mabao 2-0 na Stellah Abidjan ya Ivory Coast mwaka 1993 katika fainali ya pili ya Kombe la CAF Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Awali, Simba ilitoa sare ugenini na kuwapa matumaini Watanzania kwamba taji la kwanza kubwa Afrika lingetua nchini mwaka 1993.  Baada ya mchezo huo, Samatta na Ulimwengu watapanda ndege kesho kuelekea Nairobi, Kenya kuungana na kikosi cha Bara, Kilimanjaro Stars kinachoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge.