Tuesday, 23 June 2015

Fanya haya upate mafanikio maishani

Fanya haya upate mafanikio maishani


 
Na Emanuel Gingi
Kwa ufupi
Hata hivyo, unajua siri ya kufanikiwa maishani? Makala haya yanajaribu kutaja baadhi ya njia za unazoweza kupita ili ufike katika safari yako.

Wengi tunapenda mafanikio maishani. Ukiwa mfanyabiashara, mwajiriwa, kiongozi, mama wa nyumbani au mwanafunzi, lazima uwe na ndoto ya kufanikiwa kama sehemu ya kutimiza ndoto yako.
Hata hivyo, unajua siri ya kufanikiwa maishani? Makala haya yanajaribu kutaja baadhi ya njia za unazoweza kupita ili ufike katika safari yako.
Kuwa na mawazo chanya: Akili yako ni kifaa cha ajabu, chaweza kuamua kufanikiwa au kutofanikiwa. Fanya unachoamua kufanya usifanye unachoambiwa ufanye pasipo kukipenda. Inategemea na mawazo uliyoyajaza ndani ya akili yako, kwa hiyo kwa nini usijaze mawazo yako au akili yako na hisia chanya za kufanikiwa?
Zungumza kuhusu mafanikio: Wachunguzi wanasema takribani asilimia 75 ya mawazo ya ndani ya mtu ni hasi, yatupasa kuyabadili mawazo au maneno na kuwa chanya muda wote. Kwa mfano, badala ya kusema tatizo sema fursa, badala ya kusema hakuna kitu ninachoweza kufanya, sema naangalia hatua nyingine.
Jipe mazoezi ya kufanikiwa: Inakupasa kujipa mazoezi ya kujihamasisha hata kama muda mwingine huwezi kujisikia vyema; lazima utoke na kujihamasisha katika hatua chanya.
Jitose: Lazima uishi maisha ya utulivu au kuridhika, jiepushe na mawazo ya kufeli.
Wasome waliofanikiwa: Ukitaka kufanikiwa lazima utafute maisha au uige maisha ya watu waliofanikiwa. Kati ya vitabu au nyaraka nzuri za kukujenga ni pamoja na kutafuta machapisho yanayozungumzia watu kama kina Mwalimu Julius Nyerere, Benjamin Franklin, Abraham Lincoln, Mahatma Ghandhi na wengineo.
Hivi ni vitabu vitakavyokuongezea mbinu au ujuzi wa kushinda changamoto na kuongeza thamani ya kubadilisha maisha yako yakawa mazuri.
Panda mbegu ya mafanikio: Inakupasa wewe mwenyewe kupanda mawazo ya mafanikio kwa kufanya yafuatayo: Nenda sehemu yeyote tulivu labda nyumbani au sehemu yeyote na uzime radio na televisheni. Tafuta kiti kikufaacho na utulize mawazo, anza kufikiria lengo moja ulikamilishe.
Chukua maono ya kukuwezesha au kukamilisha maono yako yafanikiwe. Ukianza kuwa na maono utaanza kujihisi vizuri, utasema vizuri, utaona vizuri. Ni wewe mwenyewe tu. Angalizo ni kuwa kama hujaweka muda maalumu, ni vigumu kukamilisha jambo litokee
Fikiria mafanikio: Lazima uone picha kubwa kwa kila kitu unachokifanya usipoteze muda kwa vitu ambavyo si muhimu katika maisha. Vaa utofauti chanya kwenye familia, jumuiya, kampuni au taasisi. Fikiria makubwa leo kesho utapata mazuri, ukweli ni kwamba ukifikiria makubwa lazima upate makubwa, ukifikiria madogo utapata madogo.
Jiwekee malengo: Vitu ambavyo vinaangusha watu katika maisha ni kukosa malengo madhubuti. Weka malengo katika uchumi, familia, afya, roho na pia taaluma .
Hatua za kuchukua ni hizi: hakikisha lengo au malengo yamepangika, yanafikiwa, yanaeleweka, na yana muda maalumu wa kuyafikia.
Jali mwonekano wako: Watu wenye kupenda mafanikio kwanza wako makini kimwonekano. Ukweli ni kwamba ukiwa upo vizuri kimwonekano utajisikia vizuri. Vaa mavazi na sura ya mafanikio. Kuwa na akili ya mafanikio, wenye hamasa ndiyo wanaokwenda mbele kwa kujiamini.
Wasaidie wengine: Endeleza nia yako kwa kuwasaidia wengine, shirikisha kipawa chako na wengine bila kutarajiwa kulipwa. Faida kubwa ambayo utaipata ni kujenga ujasiri mkubwa pia uzoefu ambao utakufanya uwe tofauti. Daima watu wenye mafanikio, wanapenda hamasa chanya na zenye maana huku wakiwasaidia wengine.
                                         Habari kutoka Gazeti la Mwananchi.

No comments:

Post a Comment