Thursday 13 August 2015

Wizara yakanusha kuwepo ebola nchini

Thursday, August 13, 2015
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dr. Seif
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dr. Seif Rashid. 
By Elizabeth Edward
Dar es Salaam.Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imefafanua kuwa hakuna uthibitisho kwamba mkimbizi aliyekufa kwenye kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma, alikuwa akiumwa ugonjwa wa ebola.
Serikali ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana baada ya kuzuka hali ya sintofahamu kufuatia kifo cha mkimbizi huyo kuhusishwa na ugonjwa wa ebola ulioua maelfu wa watu katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi.
Agosti 9 mwaka huu, Buchumi Joel (39) akitokea katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu alipokelewa katika hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni akiwa na dalili za kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili, hasusan kwenye fizi, macho na masikio.
Licha ya kupatiwa matibabu ya hali ya juu kunusuru maisha yake, Buchumi aliaga dunia siku iliyofuata na kuzikwa chini ya uangalizi wa ofisi ya afya ya mkoa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo mpaka sasa hakuna uthibitisho kwamba mgonjwa huyo amekufa kutokana na ebola, licha ya kuwa na viashiria vya ugonjwa huo.
“Ili kupata uhakika wa hilo tayari sampuli ya mgonjwa huyu imechukuliwa na kupelekwa kwenye maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii kwa uchunguzi zaidi, kujua chanzo cha ugonjwa huu,” ilisema taarifa hiyo.
Wizara hiyo imeeleza kuwa imejiandaa vyema kudhibiti ugonjwa huo iwapo utaingia nchini ikiwa ni pamoja na kutengeneza mpango kazi wa miaka mitatu kuanzia 2015 hadi 2017.
Katika hatua nyingine, wananchi wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo uliotikisa dunia katika miaka ya hivi karibuni.
Miongoni mwa tahadhari hizo ni kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, haja ndogo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye dalili za ebola kupitia sehemu zenye michubuko au vidonda.
Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya anapohisiwa kuwepo mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Mpaka sasa zaidi ya watu 11,269 wamepoteza maisha katika nchi za Guinea, Liberia na Siera Leone tangu kuibuka kwa mlipuko wa ugonjwa huo.
Jinsi ya kujikinga na ebola
-Kunawa mikono kabla na baada ya kula.
-Kusafisha mikono muda wote ili kuepuka kusambaza ugonjwa ikiwa mtu atakuwa amemshika mgonjwa au mazingira yenye maambukizi.
-Kuwahi katika vituo vya huduma za afya mtu anapohisiwa kuwa na dalili za ebola. huu.
Kuepukana na mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa ebola.
Kutumia kemikali za kuua vijidudu kutakasa mikono.
Kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za ugonjwa wa ebola, badala taarifa za kifo hicho zipelekwe kwa uongozi wa kituo cha kutoa huduma za afya kwa ushauri.
                                     Habari kutoka:http://www.mwananchi.co.tz

Wananchi wacharukia ushindi wa Nape Mtama

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Nape  Nnauye. 
By Haika Kimaro
Lindi. Hali katika Jimbo la Mtama si shwari baada ya kundi la wananchi kufanya maandamano ya kukataa matokeo ya kura za maoni yaliyompa ushindi Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye huku wakimtaka mpinzani wake achukue uamuzi mgumu.
Katika kura za maoni, Nape alipata kura 9,344 wakati Suleiman Mathew alipata kura 4,766.
Wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa ujumbe wa aina mbalimbali kumpinga Nape na kuonyesha kumkubali Seleman Mathew, ambaye wanaamini ndiye aliyeshinda, wananchi hao walimtaka mgombea huyo atangaze kujiengua CCM, kama makada wengine waliochomoka chama hicho kupinga matokeo ya kura za maoni.
“Karibu Mathew, sisi hatuchaguliwi kiongozi, tuna imani na Messi wetu,” liliandikwa bango moja la karatasi la boksi baada ya wananchi hao kumpokea Mathew na baadaye kumsindikiza kutoka Mnazi Mmoja hadi kijiji cha Mtama, Kata ya Majengo ambako kulikuwa na watu wamekusanyika kwenye uwanja ulio karibu na ofisi za mbunge.
Akizungumza katika eneo la Mnazi Mmoja ambako alipokelewa na wananchi hao waliomtaka ahamie chama chochote cha upinzani, Mathew, ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa Yanga na timu ya Taifa, alisema kuwa amesikia wito wa wazee wa jimbo hilo pamoja na wananchi wengine waliomuita kutoka Dar es Salaam na kumshawishi ahame chama.
Mathew alidai kuwa kulikuwa na mchezo mchafu katika kura za maoni na kwamba uongozi wa CCM wa wilaya hiyo ulishiriki kumuhujumu, akisema katibu wa wilaya hakutangaza matokeo halisi, jambo ambalo alisema linawakosesha amani wananchi wa Mtama.
Wakati Mathew akidai kuibiwa kura, katibu wa Wilaya ya Lindi Vijijini, Christina Bukwi alisema uchaguzi ulifanyika na kumalizika salama kisha kutangaza matokeo mbele ya mkutano wa waandishi wa habari na wanachama wote.
Alisema wagombea wengine walioshindwa kwenye uchaguzi huo walikubali na kusaini fomu, isipokuwa Mathew aliyeamua kukataa.
“Kama alikuwa na malalamiko angekuja ofisini, lakini mpaka sasa sijapokea taarifa zake ofisini na kila mgombea alikuwa na wakala wake kwa ajili ya kulinda kura za wagombea wao, kwa hivyo mimi sitambui hayo malalamiko yake,” alisema Christina.
Lakini Mathew alisema ameshauriwa kutochukua hatua yoyote hadi vikao vya juu vya chama vitakapomaliza uchambuzi wa mwisho wa wagombea ubunge na udiwani, huku akieleza kuwa ana ushahidi kuwa ameporwa haki yake.
Kuhusu taarifa kwamba alifuatwa kushawishiwa awe na subira, Mathew alidai kuwa alifuatwa na viongozi wa Serikali, akiwamo mkuu wa mkoa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyemtaka kuwa mvumilivu mpaka Kamati Kuu itakapotoa matokeo.
“Ni kweli waliniita nikazungumza nao kwa sababu hawa ni viongozi wetu na walitambua Mtama kuna tatizo. Nilipoitwa kuonana na Waziri Mkuu, kubwa nililoambiwa ni kuwa mstahimilivu hadi Kamati Kuu itakapotangaza matokeo ndiyo maana nimekuja hapa kwa sababu lengo letu ni moja tusubiri hiyo tarahe,” alisema Mathew.
Akizungumzia sakata hilo, Nape alisema: “Mimi sizungumzii mambo ya mtu anayepiga kelele barabarani. Halafu ninyi Mwananchi mbona mnapenda kukuza mambo. Ni kwa nini niliposhinda kwa kishindo hamkuandika leo mnataka mambo hayo?”
                                                    Habari kutoka: http://www.mwananchi.co.tz