Thursday 23 July 2015

Mauzauza ya BVR yahamia Dar


Fundi wa mashine za Biometric Voters
Fundi wa mashine za Biometric Voters Registration (BVR) zinazotumika kuandikisha wananchi kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, Neema Mbwambo akiirekebisha moja ya mashine hizo katika kituo kilichopo Shule ya Sekondari ya Zawadi, Tabata Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory 
By Waandishi Wetu
Dar es Salaam. Kasoro za uandikishaji wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura zilizokuwa zikitokea katika mikoa mbalimbali nchini, zimejitokeza pia jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku ya kwanza ya kazi hiyo.
Mwananchi ilipita katika maeneo mbalimbali jana na kushuhudia wananchi wengi wakiwa wamekutana na changamoto kadhaa kwenye baadhi ya vituo ikiwamo ya kukosekana mashine za Biometric Voters Registration (BVR).
Wananchi hao walisema licha ya kwamba Dar es Salaam imepewa siku 10 ya uandikishaji, kama changamoto hizo hazitachukuliwa hatua kazi hiyo inaweza isikamilike kwa wakati.
Miongoni mwa changamoto nyingine ni kuharibika kwa mashine zilizopo, ukosefu wa umeme, uchache wa watendaji na kuelemewa na watu, mtandao usio wa uhakika na nani aanze kuandikishwa kati ya wenye mahitaji maalumu na wasionayo.
Katika kituo cha uandikishaji cha Shule ya Msingi Oysterbay ambako kuna vituo vidogo vitano, wakala wa uandikishaji, Margereth Galway alisema mwitikio wa vijana umekuwa mkubwa kiasi kwamba inakuwa shida kuwapa nafasi ya upendeleo wazee, viongozi, walemavu au wajawazito na wanaonyonyesha.
“Eneo hili lina wazee na viongozi wengi wa chama na Serikali. Mwitiko mkubwa wa vijana unatufanya tushindwe kuwasaidia watu hao,” alisema Galway.
Alisema wasimamizi wote wa kituo hicho wamekubaliana kuwa kuanzia leo, wateue mashine moja na itengwe kwa ajili ya wenye mahitaji maalumu ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi wanaokuwa wamesimama kwenye foleni muda mrefu.
“Tayari wameshakuja Warioba (Jaji Joseph), Msekwa (Pius) na Butiku (Joseph) wakiwa na wake zao na kujiandikisha. Pamoja na kufahamika kwao bado vijana hawakuwa radhi kuwapisha wakitaka wajipange jambo ambalo ni gumu kulitekeleza.
“Kama tutafanikiwa kuwashawishi waandikishaji basi foleni za watu wa kawaida zitakuwa nne na moja itaachwa kwa ajili ya wenye mahitaji muhimu,” alisema.
Katika Kituo cha Shule ya Msingi Kawe A, wazee wengi walikutwa wamekaa kwenye madawati, nje ya madarasa wakisubiri kuandikishwa baada ya vijana kutokubali kuwapisha wakidai waandaliwe utaratibu ambao hautoingilia foleni iliyopoo.
Katika Shule ya Msingi Hekima iliyopo wilayani Kinondoni, kulikuwa na malalamiko kama hayo na wananchi wakaiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuweka utaratibu maalumu.
Mmoja wa waliofika kujiandikisha, Mwanaidi Abdallah alisema katika uandikishaji huo wanawake wamekuwa wakipata shida kutokana na utaratibu mbovu.
Alisema inachukua muda mrefu kupata huduma kwa sababu baadhi ya vijana wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kujiandikisha.
Katika kituo cha Mtendaji kilichopo Mtaa wa Mzimuni, Kata ya Kawe, wananchi walikutwa wakiwa nje saa 8:00 mchana wakisubiri mashine ili uandikishaji uanze licha ya kutangaziwa kazi hiyo ingeanza asubuhi.
Kitu pekee kilichokuwa kinaendelea ni wananchi kujiorodhesha kwenye daftari na kupewa namba ya foleni hadi mashine zitakapoletwa.
Mkazi wa Ununio Beach, Joseph Mrisho alisema licha ya wananchi kujitokeza kwa wingi kuna vituo viwili mashine ziligoma kufanya kazi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ununio Beach, Mwijuma Mwinyihija alisema usumbufu waliokumbana nao wananchi umesababisha malalamiko na wengine wamekataa tamaa na kuamua kuondoka kwenda kwenye shughuli zao za kujitafutia kipato.
Katika Kata ya Wazo Mtaa wa Salasala eneo la IPTL, hadi saa 9:00 alasiri wananchi walikuwa hawajaandikishwa kutokana na mashine kugoma.
Mkazi wa eneo hilo, Blandina Hizza alisema alilazimika kurudi nyumbani mara kadhaa akijipa matumaini huenda mashine hiyo itatengemaa ili aandikishwe, lakini hadi muda huo hakufanikiwa.
Frank Etta alisema: “Hatuelewi imekuwaje hadi sasa wahusika hawajaleta mashine.”
Kituo cha Shule ya Msingi Mlimani kilichopo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho kinastahili kuwa na vituo vidogo vitatu, kina mashine moja tu iliyopelekwa.
Mwandikishaji Msaidizi katika kituo hicho, Isabella Mkumbwa alisema mwitikio wa watu ni mkubwa, lakini uandikishaji unakwenda taratibu kwa sababu watu wote wanatakiwa kusubiri mashine moja.
“Baadhi ya watu wameondoka ili wakaendelee na kazi zao. Tunasubiri mashine nyingine mbili ziongezwe wakati tukiendelea kuitumia hii iliyopo,” alisema msimamizi huyo.
Kituo cha Shule ya Sekondari Zawadi kiliyopo Tabata, uandikishaji ulikuwa haujaanza hadi saa 4:00 asubuhi wakati gazeti hili lilipotembelea kituoni hapo na kukuta mashine ikitengenezwa.
“Niliwahi kufika na nikapewa namba 23 ila tumeelezwa kuwa walimu wataanza kuandikisha pindi mashine zitakapotengamaa. Wamesema kuwa zimegoma kutokana na mtikisiko wa kusafirishwa kutoka mikoani,” alisema James Mwandumbya aliyefika kujiandikisha.
Maeneo ya Pugu Kigogo Fresh (Stesheni) waandikishaji walielemewa na wingi wa watu na kulazimika kutoa namba ili wengine waende siku nyingine.
Katika kituo cha Shule ya Msingi Mtambani, Kinondoni, wananchi walilalamika gharama za uendeshaji ambazo wameombwa wachangie ili kufanikisha uandikishaji uendelee kama ulivyopangwa.
Katika Kituo cha Shule ya Msingi Makuburi, Ofisa mwandikishaji, Karim Mweneghoha alisema walikumbwa na changamoto ya umeme iliyochangiwa na kukosekana kwa waya za kuunganisha kutoka kwenye soketi kwenda kwenye mashine.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Julius Mallaba alikiri kupokea taarifa kutoka katika baadhi ya maeneo na kudai kuwa tayari ufumbuzi umepatikana.
“Kuna taarifa nilipokea asubuhi kwamba uandikishaji unaendelea, ngoja niwasiliane na ofisa uandikishaji ili nijue (changamoto) ndipo niweze kuzungumzia vyema jambo hili,” alisema. Awali, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo ndiyo inahusika na shughuli hiyo ilisema mashine zaidi ya 8,000 zitatumika ili kufanikisha shughuli hiyo baada ya kukamilika uandikishaji mikoani.
Imeandikwa na Beatrice Moses, Julius Mathias, Bakari Kiango na Colnely Joseph.
               Habari toka: http://www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment