Thursday, 11 June 2015

WILAYA YA LUDEWA YAANDAA MPANGO WA KUKUZA SEKTA YA ELIMU

                                   Bw.Haji Mnasi ofisa elimu shule za msingi wilaya ya Ludewa

 Bw.Haji Mnasi ofisa elimu shule za msingi wilaya ya Ludewa akiongea na mwandishi wa habari Bw.Bazil Makungu

                                                 hii ni baadhi ya nyumba ya mwalimu 
                              Deo Filikunjombe akiongea na watendaji wa Srikali wilayani Ludewa
Mwalimu Kayombo wa shule ya msingi Masi mavalafu  mwenye shati nyeupe akitoa malalamiko ya makato ya kodi ya nyumba za walimu kwa katibu wa ccm wilaya ya Ludewa Bw.Lusiano Mbosa
 Diwani wa kata ya Ibumi Bw.Haule mwenye suti akimkabidhi zawadi ya mbunga mbunge wa jimbo la  Ludewa Deo Filiknjombe katika kijiji cha Masi mavalafu
 Filikunjombe akiongea na wananchi wa Masi mavalafu kuhusiana na shida wanazozipata walimu na utatuzi wake


Halmashauri ya wilaya ya Ludewa katika mkoa wa Njombe kupitia Idara ya elimu imeandaa mpango mkakati wa kukuza kiwango cha elimu katika ufaulu ili kushindana na wilaya zingine katika mkoa huu kwani wilaya ya Ludewa imekuwa na kiwango cha chini kwa miaka mingi na kusababisha baadhi ya wananchi kuiona idara ya elimu haifanyi kazi kwa kiwango kinachoridhisha.

Akiongea na wanahabari ofisini kwake ofisa elimu shule za msingi wilaya ya Ludewa Bw.Haji Mnasi alisema kuwa wilaya ya Ludewa imekuwa na matokeo mabaya kwa muda wa miaka mingi kutokana na changamoto mbalimbali hivyo ofisi yake kupitia wataalamu wa elimu umeandaliwa mpango mkakati utakao ivusha elimu kutoka kiwango cha hali ya chini na kuongeza ufaulu kama wilaya nyingine mkoa wa Njombe.

Bw.Mnasi alisema kuwa wilaya ya Ludewa ni wilaya kama nyingine nchini hivyo hakuna sababu ya kila mwaka kushika nafasi za mwisho kimkoa na kitaifa katika ufaulu wa wanafunzi kwani idara yake imeshazibaini changamoto zinazosababisha kutokea kwa hali hiyo na tayari suruhisho limepatikana la kukomesha hali hiyo.

Alisema kuwa mpango ulioandaliwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika shule zote kupitia idara ya ukaguzi na kuhakikisha kila shule inakuwa na walimu wakutosha kwani awali kuna baadhi ya shule zilikuwa na walimu wengi na nyingine zilikuwa na hali mbaya zaidi kutokana na kuwa na mwalimu mmoja hivyo zilishindwa kutoa elimu nzuri hali iliyopelekea kutofaulisha wanafunzi.

“Idara ya ukaguzi imekuwa na hali ngumu ya kifedha hivyo ilipelekea kushindwa kufanya kazi yao vizuri lakini hata mimi mwenyewe nitapita vijijini na kuzitembelea shule mara kwa mara  ili kuleta ufanisi wa kielimu licha ya kuwa mazingira ya Ludewa ni magumu kutokana na vijiji kuwa mbalimbali hivyo inatulazimu kutumia gharama nyingi katika ufuatiliaji lakini naamini tutafanikiwa tu”,alisema Bw.Mnasi.

Bw.Mnasi alisema kuwa wilaya ya Ludewa kuna baadhi ya kata hazifikiki kwa kutumia usafiri wa gari hasa kata za mwambao wa ziwa Nyasa hivyo hulazimika kutumia boti ambayo inagharimu fedha nyingi hasa katika ununuzi wa petroli lita 200 kwa safari moja na kutokana na bajeti ya Serikali kuwa ndogo katika ufuatiliaji kwa namana hiyo ukaguzi ulifanyika zaidi kata za jirani kutokana na ufinyu wa bajeti.

Kuhusu baadhi ya walimu wapya kukataa kufanya kazi katika baadhi ya maeneo kutokana na ugumu wa mazingira Bw.Mnasi alisema kuwa halmashauri inaandaa mipango ya kutoa motisha kwa baadhi ya walimu wanaofanya kazi katika mazingira magumu ili kuinusuru elimu wilayani hapa ambapo miaka ya nyuma wilaya ya Ludewa ilisifika kwa kutoa wasomi wazuri ambao walisoma katika mazingira hayo na walimu waliweza kuishi popote bila malalamiko.

Bw.Mnasi alisema kuwa Serikali imeshawaleta walimu wapya 42 katika wilaya ya ludewa na tayari wameshaanza kuripoti wilayani hapa lakini mpango wa idara ya elimu kwa mwaka huu ni kuwasambaza walimu hao katika tarafa ya Masasi na Mwambao ambako ndiko kunauhaba mkubwa wa walimu kwa miaka mingi licha ya kuwa wanafunzi wanaotoka maeneo hayo wamekuwa na uwezo mkubwa kielimu kwa kuwatumia walimu wachache waliokuwa nao.

Wilaya ya Ludewa imekuwa na changamoto kubwa katika idara ya Elimu kutokana na halamshauri ya wilaya hii kupitisha sheria ya kuwakata fedha za malipo ya Nyumba wanazoishi walimu hata kama nyumba hiyo ni mbovu huko vijijini kila mwalimu anakatwa kiasi cha shilingi elfu kumi kwa mwezi hali ambayo imekuwa ni kero kwa walimu hao na kuwafanya kukata tamaa ya utendaji katika maeneo yao ya kazi.

Kutokana na hali hiyo inayowakumba walimu mbunge wa jimbo la Ludewa Mh.Deo Filikunjombe ameitaka Halmashauri kutengua sheria hiyo ili kuwapatia unafuu wa maisha walimu hao kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili kwani halmashauri inaweza kubuni vyanzo vingine vya mapato na si kuwakamua walimu ambao ilipaswa wapate motisha katika kazi yao.

Mh.Filikunjombe aliyasema hayo katika kijiji cha ibumi ambako alikutana na changamoto hiyo kwani baadhi ya walimu walimweleza kuwa Serikali ya halmashauri inawapuuza na kuwanyonya kwa kuwatoza nyumba zisizo na kiwango cha kuishi walimu kwani nyumba nyingi wanazoishi vijijini hazina sakafu wala mifuniko ya madirisha hali ambayo ni hatari kwa walimu.

Mh.Filikunjombe alisema kuwa kimsingi Halmashauri inapaswa kutoa motisha kwa walimu hao kwani wengi wao wanaishi mbali na makao makuu ya wilaya hali ambayo huwalazimu wakati wa mwisho wa mwezi kutumia robo ya mshahara wao katika usafiri wanapofuata mishahara wilayani hali ambayo si kweli.

Mbunge huyo alisema kuwa anaandaa mpango wa kukutana na walimu wote wa wilaya ya Ludewa ili kuweza kuzungumza nao na kumshawishi mkurugenzi wa halmashauri kuwarudishia fedha zao wale waliokatwa kimakosa kwani kunabaadhi ya walimu vijana wanaishi watatu hadi wanne katika nyumba moja lakini kila mmoja anakatwa kiasi cha shilingi elfu kumi kwa mwezi.

Mwisho.

                                              Habari na: Habari Ludewa Blog.

No comments:

Post a Comment