Thursday 11 June 2015

Mimba za utotoni, nani wa kumfunga paka kengele?

 
Na Lilian Timbuka
Kwa ufupi
Hiyo ni changamoto inayolikabili taifa, huku baadhi ya watu wakiliona kuwa ni jambo la kawaida na hulipuuza wakati wengine wanalikemea.

Kila kukicha kumekuwa na kesi za migogoro ya ardhi, mirathi na hata kesi za wazazi kuozesha mabinti zao wakiwa na umri mdogo licha ya suala hilo kupigiwa kelele muda mrefu.
Hiyo ni changamoto inayolikabili taifa, huku baadhi ya watu wakiliona kuwa ni jambo la kawaida na hulipuuza wakati wengine wanalikemea.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Haki za Binadamu Duniani(Amnesty) iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Tanzania ni moja ya nchi zinaoongoza kwa matukio ya mimba za utotoni.
Takwimu zinaonyesha kuwa, kwa siku, watoto 16 wanapachikwa mimba za utotoni.
Kwa mujibu wa wataalamu, hali hiyo imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu na kwa asilimia kubwa inazorotesha maendeleo ya mtoto wa kike.
Ili kumwokoa mtoto wa kike kutoka janga hilo, jitihada mbalimbali zimefanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali kuhakikisha inawaokoa hasa wale ambao tayari wameshatumbukia katika dimbwi hilo.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Chama chaWaandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), unaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2012/2013, matukio 228 ya mimba na matukio 42 ya ndoa za utotoni yaliripotiwa.
Hata hivyo, mimba na ndoa za utotoni zimetajwa kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyowapata watoto wa kike wa Tanzania, tatizo ambalo bado ni kubwa katika baadhi ya maeneo ya Tanzania Bara na Visiwani.
Mimba za utotoni na ukatili
Kwa kiasi kikubwa tatizo hilo linakwenda sanjari na ukatili wa kijinsia ambapo kwa Tanzania Visiwani hali hiyo imeonekana zaidi katika Mkoa wa Kusini Pemba na Wilaya ya Kati Unguja, huku upande wa Tanzania Bara maeneo yenye ukatili dhidi ya wanawake pamoja na mimba za utotoni yakitajwa kuwa ni Wilaya za Kahama, Tarime, Sengerema, Newala, Mbulu, Bunda, Nkasi, Babati, Chunya, Dodoma, Bariadi, Busega na Singida vijijini.
Bokhe Odhiambo (31), mkazi wa Tarime mkoani Mara, anasema kuwa vitendo vya ukatilli dhidi ya wanawake ndani ya ndoa na mimba za utotoni kwa watoto wa kike ni mambo ya kawaida na jamii inaonekana kuwa haina muda wa kuyakemea.
“Kupigwa au kufanyiwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ndani ya ndoa, migogoro ya ardhi na mimba za utotoni kwa watoto wa kike ni mambo ya kawaida tu kwenye jamii yetu licha ya wasaidizi wa kisheria kutoa elimu,” anssema Odhiambo.
Kutokana na changamoto hiyo, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) kimejitosa kutoa msaada wa kisheria katika mikoa yenye changamoto lengo likiwa ni kupunguza tatizo hilo.
Mwenyekiti wa Tawla, Aisha Bade anasema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo chama chake kimeamua kusambaza wasaidizi wa kisheria 400 nchi nzima lengo likiwa ni kusaidia kutatua migogoro ya ardhi na mirathi.
Bade anasema Tawla imebaini kuwa mikoa ya Pwani na Morogoro, Mtwara, Lindi, Arusha , Tanga, Shinyanga, Manyara na Mwaza inaongoza kwa kuwa na migogoro ya mirathi, vitendo vya ukatili na kuozesha watoto katika ndoa za utotoni.
Anasema kuwa mbali na mikoa hiyo pia mikoa ya Tanga, Arusha, Dodoma inaongoza kwa kuwa na migogoro ya ardhi pamoja na mirathi na hivyo juhudi mbalimbali zinahitajika kukabiliana na tatizo hilo. “Tumesambaza wasaidizi wa kisheria 400 nchi nzima lengo ni kutatua migogoro iliyopo hasa katika maeneo ya vijijini ambayo tumeona hayana msaada wa kisheria” anasema Bade.
“Mbali na mikoa hiyo pia mikoa ya Tanga, Arusha, Dodoma nayo ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kuwa na changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi na miradhi na kwamba juhudi za pamoja zinahitajika kushirikia katika kutatua changamoto hiyo ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea kutokana na tatizo hilo”anasema Beda.
Tawla imefanya nini?
Anasema kuwa Tawla ilianza mafunzo ya wasaidizi wa sheria mwaka 2006 na kutokana mafunzo hayo zaidi ya wananchi 4,600 wamenufaika kwa kupata msaada wa kisheria vijijini katika kipindi cha mwaka jana pekee.
John Maziku, mkazi wa mkoani Shinyanga, anasema kuwa utoro kwa wanafunzi a shule za sekondari na msingi ni tatizo linaloukabili mkoa huo kwa sasa na sababu kubwa ni wazazi kutokuwa karibu na watoto wao.
“Wazazi wengi wanakwenda migodini wanakaa huko kwa muda mrefu na hwakumbuki kama wana familia, mama anabakia na mzigo mkubwa wa kuitunza.
“Wazazi ndiyo chanzo kikubwa cha utoro katika wilaya ya Bukombe kwa sababu baba anapokwenda kwenye machimbo ya migodi hakumbuki kuwa wanaacha shule na kwenda kutafuta pesa,”anasema.
Mwajuma Mohamed (15), mkazi wa Ushirombo amekatiza masomo yake akiwa darasa la sita baada ya kupewa mimba na dereva wa magari makubwa. Hivi sasa ana mtoto wa miezi saba, lakini baba yake hajawahi kupeleka huduma ya mtoto.
Mchango wa Tamwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Valerie Msoka anasema wamefanya kampeni ya kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondai na msingi juu ya umuhimu wa elimu na madhara ya mimba za utotoni ambayo bado chama hicho kinaendelea nayo, lengo likiwa kuifikia mikoa yote nchini.
Anasema kwamba elimu hiyo imetolewa katika wilaya kumi za mikoa ya kusini ambayo ni Lindi na Mtwara na kwamba mikoa ya Pwani na Dar es Salaam imepata elimu hiyo kupitia mradi wa GEWE, unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Denmark (Danida).
“Elimu inayotolewa kwa wanafunzi inalenga kumwezesha mwanafunzi namna ya kujitambua na kujua malengo ya elimu aipatayo itamsaidiaje katika maisha yake ,” anasema Msoka.
Anasema mafunzo hayo ni kitu cha muhimu na yatachangia maendeleo ya mwanafunzi hapo baadaye.
“Hata kama wazazi wanapomlazimisha kuolewa, binti anatakiwa kukataa ili aweze kumaliza elimu yake vizuri,” anasema Msoka na kuongeza: “Kazi hii ya kupambana na janga hili ni lazima pia lifanywe na wanasiasa hasa katika kipindi hiki tunachoelekea katika Uchaguzi Mkuu.” Anabainisha kuwa miongoni mwa wanasiasa imejengeka tabia ya kutotilia maanani matatizo kama ya unyanyasaji wa kijinsia, hasa kipindi kama hiki wakihofia kukosa kura.
“Ninawasihi wanasiasa, waache tabia ya kufumbia macho matatizo yanayowakabili wapiga kura wao bali wayatafutie ufumbuzi,” anasema Msoka.
Hata hivyo, swali linalobaki ni nani wa kulaumiwa kwa mimba za utotoni; ni nani wa kuwafichua watuhumiwa na kukomesha ouvu huo, nani wa kumfunga paka kengele?
                                                        Habari hii imepatikana katika gazeti la Mwanannchi.

No comments:

Post a Comment