Saturday 13 June 2015

Mkurugenzi wa Wizara ya Afya kortini kwa tuhuma za rushwa

Mkurugenzi wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Elias Chinamo akipelekwa rumande chini ya ulinzi wa polisi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana. Chinamo anatuhumiwa  kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa. Picha na Anthony Siame 
Na Tausi Ally na Samwel Eugen

Posted  Juni13  2015  saa 10:18 AM
Kwa ufupi
Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai alidai wakati akisoma mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Renatus Rutta, kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kati ya Juni 2011 na Februari 2013.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Elias Chinamo amefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu akikabiliwa na mashtaka 14 ya kuomba na kupokea rushwa.
Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai alidai wakati akisoma mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Renatus Rutta, kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kati ya Juni 2011 na Februari 2013.
Swai alidai kuwa katika kipindi hicho mshtakiwa aliomba na kupokea rushwa ya zaidi ya Sh14.44 milioni.
Mwendesha Mashtaka huyo alidai kuwa Chinamo alipokea rushwa ya Sh6.1 milioni kutoka kwa Suzana Nchala, fedha ambazo alidai alizipokea kupitia akaunti yake yenye namba 0152237197600 iliyopo tawi la benki ya CRDB la Holland.
Alidai kuwa alipokea fedha hizo kama faida ya kumpa nafasi ya kuandaa semina mbalimbali na mikutano ya wizara hiyo, kitu ambacho kipo kinyume na matakwa ya mwajiri wake.
Pia mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa Chinamo alipokea Sh2.06 milioni kutoka kwa Fadhili Kilemile, fedha ambazo zilipitishiwa kwenye akaunti hiyo kwa lengo la kumpa nafasi ya kuandaa semina mbalimbali na mikutano ya wizara hiyo kinyume na matakwa ya mwajiri wake.
Katika shtaka jingine, Chinamo anadaiwa kupokea Sh3.28 milioni kutoka kwa Emmanuela Safari, Sh700,000 kutoka kwa Joseph Bilango na Sh2.3 milioni kutoka kwa Anyitike Mwakitalima kupitia akaunti ya CRDB na 019201018063 ya NBC, tawi la Kichwele.
Chinamo aliyakana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wake umekamilika.
Hakimu Rutta alimuachia huru mshtakiwa huyo baada ya kukamilisha masharti ya kusaini dhamana ya Sh10 milioni pamoja na kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya dhamana ya maneno yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha. Kesi imeahirishwa hadi Julai Mosi, 2015 atakaposomewa maelezo ya awali.
              Habari na: http://www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment