Monday 15 June 2015

Albino wamtoa chozi Kikwete

> Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete 


Posted  Jumapili,Juni14  2015  saa 8:56 AM
Kwa ufupi
Akizungumza katika maadhimisho ya kimataifa ya siku ya kuongeza uelewa wa albino duniani, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Rais Kikwete alisema mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yanayoendelea nchini yanamsononesha na kulitia doa Taifa.
Dar/Arusha. Rais Jakaya Kikwete ametokwa na machozi wakati akisikiliza wimbo ya masikitiko ya watoto wenye ulemavu wa ngozi (albino), na akaeleza kuwa ni upumbavu kuamini kuwa viungo vyao vinaleta utajiri.
Akizungumza katika maadhimisho ya kimataifa ya siku ya kuongeza uelewa wa albino duniani, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Rais Kikwete alisema mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yanayoendelea nchini yanamsononesha na kulitia doa Taifa.
Rais Kikwete alisema wimbo wa watoto wenye albino kutoka Tanga, ulivyoanza alianza kuhisi angetokwa machozi na baadaye alishindwa kujizuia na kutokwa na machozi.
“Hawa watoto wameimba mambo ambayo yamenigusa sana, na tumepokea kilio chenu kwa umuhimu mkubwa na ninaahidi tutashirikiana kuyashughulikia matatizo yenu,” alisema.
Alisema suala la matibabu ya albino ni jambo ambalo linashughulikiwa, ili kuhakikisha vifaa tiba ambavyo vinahitajika hasa kutibu magonjwa ya ngozi vinapatikana na kuwawezesha kupata matibabu bure.
Akizungumzia hatua za Serikali, Rais Kikwete alimpa nafasi Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe kueleza hatua zilizofikiwa katika kuunda kamati ya kitaifa ya kuishauri Serikali.
Waziri Chikawe alieleza kuwa tayari wizara yake, imekamilisha mchakato wa kuunda kamati hiyo, ambayo itakuwa na wajumbe 15, watano kutoka chama cha wenye albino, watano chama cha waganga wa jadi na watano kutoka serikalini.
Awali Mwakilishi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unicef) nchini, Zulmira Rodrigues aliiomba Serikali kuwaondoa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) waliowekwa katika vituo maalumu, kwa kuwa kitendo hicho kinawanyanyapaa.
Akizungumza katika mkutano uliokuwa wa kuelezea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelimishaji kuhusu albino jijini hapa jana, Rodrigues alisema vituo hivyo vinaweza kutumika kwa ajili ya kuwahifadhi albino kwa muda mfupi na si kuvifanya suluhisho la kudumu litakalowapa ulinzi.
“Kuwatenga albino na kuwaweka katika vituo ambavyo wanaishi pekee yao ni kukiuka haki za binadamu na kuwanyima uhuru wao, badala yake jamii iwatengenezee mazingira mazuri yatakayowafanya waishi kwa usalama kama watu wengine,” alisema Rodrigues.
Imeandikwa na Goodluck Eliona (Dar) na Mussa Juma na Bertha Ismail (Arusha).

No comments:

Post a Comment