Saturday 13 June 2015

Lifti Muhimbili zazua kasheshe

Image result for lifti muhimbili

Na Pamela Chilongola
Kwa ufupi
Wauguzi watumia ngazi kupanda na kushuka na maiti, wagonjwa. Kaimu mkurugenzi akiri lifti kutofanyakazi
Dar es Salaam. Lifti za wodi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zimeharibika na kusababisha wauguzi kulazimika kuwabeba wagonjwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Pia, wauguzi hao wanalazimika kuzibeba maiti kutoka wodini na kuzipeleka kwenye chumba cha kuhifadhi kupitia ngazi za hospitali hiyo kutokana na tatizo hilo la lifti na kuwasababishia adha kubwa.
“Kuharibika kwa lifti hizi kwa zaidi ya mwezi sasa kunasababishia kufanya kazi katika mazingira magumu hasa ya utoaji huduma kwa wagonjwa na ubebaji wa maiti,” alisema jana mmoja wa wauguzi wa wodi ya Kibasila, Afred Ismail.
Alisema mgonjwa mahututi akipelekwa kwenye wodi hiyo anatakiwa kulazwa chumba namba 16 ambacho kipo gorofa ya tatu wanalazimika kumweka chumba cha upasuaji ambacho kipo chini na kusababisha kutotibiwa kwa wakati.
“Wauguzi tuna wakati mgumu wa kazi, utakuta mgonjwa anatakiwa alazwe kwenye chumba namba 16 kutokana na lifti kuwa mbovu, tunashindwa kumpandisha kwenye ngazi hadi hapo tutafute watu zaidi ya saba wa kumbeba ili akapatiwe matibabu,” alisema Ismail.
Muuguzi Edita Amandous alisema wanapata wakati mgumu hasa mgonjwa anapofariki kwani kumtoa ghorofa ya tatu na kumshusha chini ili kumpeleka kwenye chumba cha mahututi wanalazimika kumbeba watu zaidi ya 10 kushuka kwenye ngazi.
Kaimu Mkurugenzi wa MNH, Dk Hussein Kidanto alisema hospitali hiyo ilijengwa miaka mingi iliyopita hivyo wanampango wa kuboresha wodi ya Kibasila, Mwaisela na Sewahaji ila wanasubiria fedha zilizotengwa kwa ajili ya hospitali hiyo.
Dk Kidanto alisema, suala la lifti ni tatizo kubwa hasa kwenye wodi ya Kibasila na Sewahaji hivyo uongozi wa hospitali hiyo wamekuwa wakitengeneza kwa gharama kubwa kutokana na kuwa chakavu kila wakati zimekuwa zikiharibika.
“Hizi lifti kila wakati tunazitengeneza na tunatumia gharama kubwa sana lakini sasa hivi tumejipanga kununua mpya na tunampango wa kujenga wodi ya ghorofa 10 ambayo itaondoa hii changamoto,” alisema Dk Kidanto.
Alisema changamoto zinazojitokeza zinasababishwa na ufinyu wa bajeti, hivyo fedha inayotengewa hospitali hiyo ni ndogo na kusababisha kushindwa kuboresha majengo na kununua vifaa vya hospitali hiyo.
                                                                  Habari kutoka: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment