Thursday 2 July 2015

WAKULIMA KIJIJI CHA AMANI WILAYANI LUDEWA WAFUNDWA ILI KUENDELEA KUZALISHA MAHINDI KWA WINGI.

                                            Siku ya wakulima wa Amani ndivyo ilivyokuwa 
Mgeni rasmi wa hafla hiyo ambaye ni ofisa kilimo wa wilaya ya Ludewa  Bw.Naftari Mundo akiongea na wakulima wa kata ya Mundindi katika kijiji cha Amani

Mkulima wa kijiji cha Amani wilayani Ludewa akitoa maelekezo namna ya elimu aliyoipata na na alivyoweza kuitumia katika uzalishaji wa zao la mahindi


                                        Afisa miradi wa shirika la ACTN Bw.Deogratias Ngotio
                                                                 wakulima wakipata somo

                                   mtaalamu wa mbegu za mahindi Bw.Mbele akiongea na wakulima
                             Mtaalamu wa mbolea toka YARA Bw.Shine akitoa elimu kwa wakulima








Wakulima wa kijiji cha amani wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe wamepata elimu ya kilimo bora cha mazao ya mahindi,maharage na soya kupitia mashamba darasa ili kuweza kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao hayo kutokana na kijiji hicho kuwa kinara wa uzalishaji wa mazao ya aina hiyo wilayani hapa na mkoa wa Njombe kwa ujumla.

Elimu hiyo imetolewa hivi karibuni na wafadhiri ambao ni African conservation tillage network(ACTN BRITEN,RUDI na CRDB BANK wakiwa na kauli mbiu isemayo “kilimo hifadhi kwa mazao bora mavuno zaidi gharama nafuu na ardhi yenye rutuba”ikiwa na lengo kuu la kukuza uchumi kwa wakulima ambao wataanza kufanya kazi za kilimo kwa kisasa zaidi.

Akiongea katika hafla ya kufunga mafunzo hayo na wakulima wa kata ya Mundindi katika kijiji cha Amani wilayani Ludewa afisa miradi wa ACTN Bw.Deogratias Ngotio alisema kuwa  muungano wao ni kutoa mafunzo ya miradi shirikishi ya kuongeza tija ya uzalishaji katika nyanda za juu kusini mwa Tanzania kwa mazao ya mahindi,mpunga,maharage na soya kupitia elimu hiyo wakulima wataweza kunafaika na kilimo.

Bw.Ngotio alisema kuwa kilimo kimekuwa ni mzigo kwa wakulima kutokana na wakulima kutokuwa na elimu ya kutosha ya kilimo hivyo wadau wa kilimo nchini wameona ni bora kutoa elimu ya kilimo bora na kuhifadhi ardhi yenye rutuba ili kilimo kiweze kuwa ni ukombozi kwa wakulima na sio mzigo wa wakulima kama inavyoonesha katika meneo mengi.
 

Alisema kuwa wakulima walio wengi wamekuwa wakilima maeneo makubwa na kupata mavuno kidogo hali inayowakatisha tama wakulima na wengine huachana na kilimo kwa kuona hakina faida ikiwa haya yate husababishwa na elimu duni waliyonayo wakulima wa Nyanda za juu kusini lakini kwa kupitia wadau mbalimbali wa kilimo wanaoweza kutoa elimu baadhi ya wakulima wameshaanda kutambua umuhimu wa kilimo katika uchumi wa taifa na maisha yao kwa ujumla.

“tumegundua kuwa baadhi ya wakulima wanakatishwa tama ya kuendelea na kilimo kutokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusiana na kilimo bora lakini kutokana na muungano wetu kwa pamoja tumeweza kutoa elimu ya shamba darasa ambapo baadhi ya wakulima wameanza kupata mafanikio kupitia mafunzo yetu hali ambayo inatupatia moyo wa kuendelea na mafunzo haya maeneo mbalimbali ili kuweza kuwainua wakulima katika mavuno zaidi”,alisema Bw.Ngotio.

Mmoja wa wakulima  wa Kijiji cha Amani Bw.Fransis Mlelwa alisema kuwa  kijiji hicho kinachoongoza wilayani Ludewa na mkoa wa Njombe kwa uzalishaji wa mazao ya mahindi na maharage ambapo mkulima wa hali ya chini anauwezo wa kuvuna magunia 1500 katika msimu mmoja wa kilimo kwa hali hiyo mashirika mbalimbali yameweza kuungana kuanza kutoa elimu ya kilimo bora.

Bw.Mlelwa alisema kuwa licha ya kupata mafunzo hayo ambayo ni msaada mkubwa kwao katika uzalishaji pia changamoto kubwa inayowakabili wakulima wa kijiji hicho ni upatikanaji wa masoko ya mahindi wakati wa mavuno kwani kumekuwana na shida kubwa kutokana na uzalishaji mkubwa wa mahindi walio nao.

Alisema licha ya kuwa Serikali imekuwa ikiyanunua mahindi kupitia wakala wa hifadhi ya chakula ya Taifa lakini bado wakulima wamekuwa wakibaki na kiasi kikubwa cha mahindi na kushindwa kupata masoko hivyo aliiomba Serikali kuiangalia upya wilaya ya Ludewa kutokana na uzalishaji mkubwa wa zao la mahindi unaofanyika.

Mgeni rasmi wa hafla hiyo ya mafunzo ya shamba darasa ambaye ni ofisa kilimo wa wilaya ya Ludewa Bw.Naftari Mundo akitoa hotuba yake kwa wakulima hao alisema kuwa anatoa pongezi kwa shirika la ACTN kwa kubuni mafunzo hayo ambayo yatainua uchumi wa wakulima na Taifa kwa ujumla katika mpango mzima wa uboreshaji wa kilimo nchini.

Bw.Mundo alisema kuwa Serikali bado inaangalia uwezekano wa kutafuta mashirika mbalimbali ya nje ya nchi ili yaweze kuyanunua mazao ya wakulima kwa bei nzuri hivyo wakulima hawapaswi kukata tama ya kuendelea na kilimo kutokana na kukosa masoko kwani tayari juhudi za ununuzi wa mazao yao zimeshafanyika.

Aidha aliwataka wadau mbalimbali wa kilimo kuiga mfano wa ACTN na washirika wake katika kuendeleza kilimo nchini ili kuweza kuinua pato la taifa na kutengeneza maisha bora ya wakulima kwani kilimo nio msingi wa maisha ya mtanzania bila kilimo hakuna chakula.

mwisho.
                                              Habari na: http://habariludewa.blogspot.com

No comments:

Post a Comment