Wednesday 17 June 2015

Akamatwa akitafuta mteja wa mtoto albino

Akamatwa akitafuta mteja wa mtoto albino

Na Robert Kakwesi
Kwa ufupi
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Juma Bwire alimtaja mtuhumiwa huyo aliyekamatwa juzi kuwa ni Masanja Mwinamila (44), mkazi wa Ugembe wilayani Nzega.

Tabora. Mtu mmoja amekamatwa na polisi akiwa katika harakati za kutafuta soko la kuuza mtoto mdogo wa dada yake ambaye ana ulemavu wa ngozi mwenye umri wa miaka sita.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Juma Bwire alimtaja mtuhumiwa huyo aliyekamatwa juzi kuwa ni Masanja Mwinamila (44), mkazi wa Ugembe wilayani Nzega.
Kamanda Bwire alisema polisi walipata taarifa za mtuhumiwa huyo kutafuta wateja ndipo askari walipoweka mtego kwa kujifanya wanunuzi na kukubaliana naye kufanya biashara kwa kiwango cha fedha alichohitaji na kudai kwamba mtuhumiwa alitekeleza makubaliano hayo na kwenda kumchukua mtoto huyo akiwa na mama yake na ndipo askari walipomtia mbaroni. Kamanda Bwire alieleza kuwa mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Kamanda Bwire alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ni mkakati maalumu unaoendelea kufanywa na polisi kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Joyce Mwandu alieleza kuwa kaka yake alifika nyumbani kwake na kudai kuwa amekwenda kumtembelea na baada ya muda alitokomea na mtoto hadi alipopata taarifa za kukamatwa kwake.

No comments:

Post a Comment