Sunday, 1 February 2015

MADAKTARI NA WAUGUZI WAUZA VIUNGO VYA MIILI YA WATOTO WALIOKUFA HOSPITALI KWA WAGANGA WA JADI!! A+A- PrintEmail

Wakati serikali ikihaha kutafuta muarobaini wa mauaji ya watu wenye ulemavu Ngozo (Albino),katika mikoa ya kanda ya ziwa,huku ikidiriki kutangaza vita dhidi ya wapiga ramli wote, katika hali isiyokuwa ya kawaida imebainika kuwa watoto ambao huzaliwa wakiwa hawajafikisha umri na kufa au kupoteza maisha wakati wa kuzaliwa viungo vyao huuzwa kwa waganga wa kienyeji katika hospitali ya wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu.

Inaelezwa kuwa akina mama wanaojifungua watoto hao na kwa bahati mbaya kupoteza maisha, viungo vya watoto hao huwa havipelekwi kuzikwa kama ilivyo kawaida na taratibu za hospitali, badala yake wauguzi na wafanyakazi wengine huchukua viungo hivyo na kupeleka kwa waganga wa jadi.

Tuhuma hizo zilitolewa juzi mbele ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Mwamvua Jilumbi katika kikao cha pamoja na wadau wa afya mkoa  kilichofanyika katika ukumbi wa kanisa la KKKT mjini Bariadi wakati wa uzinduzi wa mpango mkakati wa kukomesha vifo vya wajawazito
na watoto mkoani Simiyu ulioko chini ya AMREF Tanzania.

Wadau hao walibainisha kuwa hali hiyo imekuwa ikijitokeza kila mara katika hospitali ya Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, ambapo walieleza kuwa mtandao mzima wa kuuzwa kwa viungo hivyo ufanyika kati ya wauguzi pamoja na madaktari ambao ndiyo wahusika wakuu kuzalisha akina mama wajawazito.

Mbele ya Katibu huyo tawala wa Mkoa wadau hao waliendelea kueleza kuwa viungo hivyo vimekuwa vikiuzwa kuanzia shilingi 400,000 hadi 500,000 kiasi ambacho walieleza hutolewa na waganga wa hao wa jadi.

“..katika hospitali yetu ya Bariadi kuna jambo ambalo siyo zuri na jema leo ngoja tulitoboe mbele ya kikao hiki na tena mbele za waandishi wa habari na wewe Katibu tawala wa Mkoa..akina mama wanaojifungua watoto wao kwa bahati mbaya akafariki viungo vya watoto hao huuzwa kwa waganga wa jadi” Alisema Gasper Mathew na kuongeza kuwa..

“ viungo hivyo vinauzwa shilingi 400,000 hadi 500,000 huu ni ushirikina wa hali ya juu na ni hatari..wauguzi pamoja na madaktari ndiyo wanahusika sana..wamekuwa wakipewa kiasi hicho..kila mara wanafaya hivyo lakini tumekuwa kimya” Alisema

Walisema kuwa akinamama  wengi hufika hospitalini hapo kwa lengo la kujifungua na mara wanapojifungua na kwa bahati mbaya mtoto au watoto kufariki  kutokana na matatizo ya afya ya uzazi baadhi huamua kuwahifadhi katika chumba cha maiti lakini wengi hujikuta wakirejea nyumbani mikono mitupu baada ya miili ya watoto wao kuuzwa kwa waganga wa kienyeji.

Akizungumzia tuhuma hizo Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu,Mwamvua
Jilumbi katika kikao hicho alimtaka Mkurugenzi wa Halmshauri ya Mji wa Bariadi Erica Mssika kutoa maelezo juu ya tuhuma hizo.

Akitoa maelezo ya tuhuma hiyo Mkurugenzi huyo alisema kuwa hana taarifa yoyote juu ya kuwepo kwa vitendo hivyo katika hospitali yake, huku akieleza kuwa watafanya uchunguzi mara moja na watakao bainika kufanya hivyo watachukuliwa sheria mara moja.

“..hii ni hatari mimi hili nimelipata hapa na nimelisikia leo sina taarifa yeyote.. ila nawaomba wadau waliotoa tuhuma hizi tushirikiane tufanye uchunguzi haraka ili tuwabaini na watakaobainika tutawachulia sheria za kinidhamu” Alisema Mssika.

Katika kikao hicho Meneja Mradi wa Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masula ya afya AMREF Health Africa tawi la Tanzania,katika mkoa wa Simiyu, Godfrey Matumu, aliitaka  jamii ya mkoa wa Simiyu kushiriki kikamilifu katika kuthibiti vifo vya akinamama wajawazito na watoto wachanga wenye umri chini ya miaka mitano.

Alisema vifo hivyo  vimekuwa vikisababishwa na kuchelewa kupata huduma katika vituo vya afya kwa wakati.wakati wa kuzindua Mpango Mkakati wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto katika mkoa wa Simiyu utakaotekelezwa kwa muda wa miaka 4 (2014-18),chini ya msaada wa watu wa Canada.
Chanzo-http://simiyunews.blogspot.com

TOA MAONI YAKO HAPA

No comments:

Post a Comment