Monday, 15 June 2015

Albino wamtoa chozi Kikwete

> Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete 


Posted  Jumapili,Juni14  2015  saa 8:56 AM
Kwa ufupi
Akizungumza katika maadhimisho ya kimataifa ya siku ya kuongeza uelewa wa albino duniani, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Rais Kikwete alisema mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yanayoendelea nchini yanamsononesha na kulitia doa Taifa.
Dar/Arusha. Rais Jakaya Kikwete ametokwa na machozi wakati akisikiliza wimbo ya masikitiko ya watoto wenye ulemavu wa ngozi (albino), na akaeleza kuwa ni upumbavu kuamini kuwa viungo vyao vinaleta utajiri.
Akizungumza katika maadhimisho ya kimataifa ya siku ya kuongeza uelewa wa albino duniani, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Rais Kikwete alisema mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yanayoendelea nchini yanamsononesha na kulitia doa Taifa.
Rais Kikwete alisema wimbo wa watoto wenye albino kutoka Tanga, ulivyoanza alianza kuhisi angetokwa machozi na baadaye alishindwa kujizuia na kutokwa na machozi.
“Hawa watoto wameimba mambo ambayo yamenigusa sana, na tumepokea kilio chenu kwa umuhimu mkubwa na ninaahidi tutashirikiana kuyashughulikia matatizo yenu,” alisema.
Alisema suala la matibabu ya albino ni jambo ambalo linashughulikiwa, ili kuhakikisha vifaa tiba ambavyo vinahitajika hasa kutibu magonjwa ya ngozi vinapatikana na kuwawezesha kupata matibabu bure.
Akizungumzia hatua za Serikali, Rais Kikwete alimpa nafasi Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe kueleza hatua zilizofikiwa katika kuunda kamati ya kitaifa ya kuishauri Serikali.
Waziri Chikawe alieleza kuwa tayari wizara yake, imekamilisha mchakato wa kuunda kamati hiyo, ambayo itakuwa na wajumbe 15, watano kutoka chama cha wenye albino, watano chama cha waganga wa jadi na watano kutoka serikalini.
Awali Mwakilishi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unicef) nchini, Zulmira Rodrigues aliiomba Serikali kuwaondoa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) waliowekwa katika vituo maalumu, kwa kuwa kitendo hicho kinawanyanyapaa.
Akizungumza katika mkutano uliokuwa wa kuelezea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelimishaji kuhusu albino jijini hapa jana, Rodrigues alisema vituo hivyo vinaweza kutumika kwa ajili ya kuwahifadhi albino kwa muda mfupi na si kuvifanya suluhisho la kudumu litakalowapa ulinzi.
“Kuwatenga albino na kuwaweka katika vituo ambavyo wanaishi pekee yao ni kukiuka haki za binadamu na kuwanyima uhuru wao, badala yake jamii iwatengenezee mazingira mazuri yatakayowafanya waishi kwa usalama kama watu wengine,” alisema Rodrigues.
Imeandikwa na Goodluck Eliona (Dar) na Mussa Juma na Bertha Ismail (Arusha).

Saturday, 13 June 2015

Mkurugenzi wa Wizara ya Afya kortini kwa tuhuma za rushwa

Mkurugenzi wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Elias Chinamo akipelekwa rumande chini ya ulinzi wa polisi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana. Chinamo anatuhumiwa  kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa. Picha na Anthony Siame 
Na Tausi Ally na Samwel Eugen

Posted  Juni13  2015  saa 10:18 AM
Kwa ufupi
Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai alidai wakati akisoma mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Renatus Rutta, kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kati ya Juni 2011 na Februari 2013.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Elias Chinamo amefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu akikabiliwa na mashtaka 14 ya kuomba na kupokea rushwa.
Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai alidai wakati akisoma mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Renatus Rutta, kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kati ya Juni 2011 na Februari 2013.
Swai alidai kuwa katika kipindi hicho mshtakiwa aliomba na kupokea rushwa ya zaidi ya Sh14.44 milioni.
Mwendesha Mashtaka huyo alidai kuwa Chinamo alipokea rushwa ya Sh6.1 milioni kutoka kwa Suzana Nchala, fedha ambazo alidai alizipokea kupitia akaunti yake yenye namba 0152237197600 iliyopo tawi la benki ya CRDB la Holland.
Alidai kuwa alipokea fedha hizo kama faida ya kumpa nafasi ya kuandaa semina mbalimbali na mikutano ya wizara hiyo, kitu ambacho kipo kinyume na matakwa ya mwajiri wake.
Pia mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa Chinamo alipokea Sh2.06 milioni kutoka kwa Fadhili Kilemile, fedha ambazo zilipitishiwa kwenye akaunti hiyo kwa lengo la kumpa nafasi ya kuandaa semina mbalimbali na mikutano ya wizara hiyo kinyume na matakwa ya mwajiri wake.
Katika shtaka jingine, Chinamo anadaiwa kupokea Sh3.28 milioni kutoka kwa Emmanuela Safari, Sh700,000 kutoka kwa Joseph Bilango na Sh2.3 milioni kutoka kwa Anyitike Mwakitalima kupitia akaunti ya CRDB na 019201018063 ya NBC, tawi la Kichwele.
Chinamo aliyakana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wake umekamilika.
Hakimu Rutta alimuachia huru mshtakiwa huyo baada ya kukamilisha masharti ya kusaini dhamana ya Sh10 milioni pamoja na kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya dhamana ya maneno yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha. Kesi imeahirishwa hadi Julai Mosi, 2015 atakaposomewa maelezo ya awali.
              Habari na: http://www.mwananchi.co.tz

DR. SHEIN AWATAKA WAZAZI, SERIKALI NA WATOTO WENYEWE KUSHIRIKIANA KUKOMESHA MIMBA ZA UTOTONI

Baadhi ya watoto walioshiriki mbio za hisani za Nusu marathoni zilizoandaliwa katika shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika zinazotarajiwa kufikia kilele chake tarehe 16/6/2015 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar BaloziSeif Ali Iddi akisalimiana na baadhi ya watoto walioshiriki mbio za hisani za Nusu marathoni zilizoandaliwa katika shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika huko uwanja wa amani mjini Zanzibar.
Watoto wakionyeshana ubabe wakati wa mashindano yao yam bio za Nusu marathoni zilizoandaliwa katika shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika.

Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Zainab Omar Mohammed akijiandaa kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuzungumza katika shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein
Balozi Seif akisalimiana na Mwakilishi wa Baraza la Watoto kutoka Handeni Mkoani Tanga Mohammed Khalid kwenye hafla ya mbio za hisani za Nusu marathoni zilizoandaliwa katika shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika hapo uwanja wa amani.

Balozi Seif kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein akitoa zawadi kwa washiriki wa mbio za hisani za Nusu marathoni zilizoandaliwa katika shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika.

                                                                                            Picha na – OMPR, ZNZ.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alisema kwamba ili kupata mafanikio makubwa katika kukomesha Ndoa na Mimba za Utotoni ushirikiano wa lazima wa kupambana na kadhia hiyo unahitajika kati ya Wazazi,Serikali pamoja na watoto wenyewe.

Alisema elimu ya maadili inapaswa kutiliwa mkazo katika kuwapatia watoto na wzazi kwa lengo la kupiga vita tatizo hilo linaloonekana kuendelea kudhalilisha watoto na akina Mama na hatimae kuviza ustawi wao.

Dr. Shein alitoa kauli hiyo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika zilizoanza kwa Mbio za Hisani za nusu Marathoni.

Mbio hizo zilizochukuwa zaidi ya saa Moja zimeshirkisha Watoto pamoja na Wazazi na kufanyika katika uwanja wa Michezo wa Amani Mjini Zanzibar zikishuhudiwa na wanafunzi na watu mbali mbali.

Alisema Wazazi hawanabudi kuhakikisha kwamba wanazingatia maadili na misingi mizuri ya malezi ya watoto yanayoambatana na mazingira yatayowapa elimu na uelewa wa kutosha juu ya athari za mimba za utotoni.


Dr. Shein alifahamisha kwamba mimba za utotoni na ndoa za umri mdogo ni utamaduni unaoonekana kujengeka kwa baadhi ya Makabila na familia hapa Nchini jambo ambalo wazazi wanapaswa kulisimamia kidete katika kulipinga kwa nguvu zao zote.

Alisema vitendo vya unyanyasaji vinalitia aibu Taifa, ni kinyume na mafundisho ya dini zote zinazofuatwa hapa Nchini ambapi pia ni kinyume na haki za Binaadamu na haki za Kikatiba.

Rais wa Zanzibar alishukuru na kuzipongeza Taasisi na mashirika ya Kimataifa na yale ya Kitaifa yanayoendelea kujitolea kwenyea kuunga mkono juhudi za Serikali zote mbili katika kupinga udhalilishaji wa Watoto hasa lile la kuozeshwa wakiwa na umri mdogo.

Dr. Shein alifahamisha kwamba Serikali kupitia taasisi mbali mbali na vyombo vya sheria inaendelea kuhakikisha kuwa juhudi zinaochukuliwa sasa kuimarisha ustawi wa watoto zinaleta mafanikio.

“ Mafanikio ya pamoja ndio yatakayotuwezesha kutokomeza mimba za utotoni na ndoa za umri mdogo. Kila mmoja aweze kutekeleza wajibu wake na kutoa mashirikiano yanayohitajika katika kukomesha matendo hayo “. Alisema Dr. Shein.

Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania nay a Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa zikipanga na kutekeleza mipango tofauti kwa lengo la kulinda na kuimarisha maslahi na ustawi wa watoto hapa nchini.

Alisema Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa miongoni mwa Mataifa ya mwanzo yaliyoridhia Mkataba wa Haki za Mtoto uliopitishwa katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa Tarehe 20 Novembwa mwaka 1989 na kutia saini mwaka 1990.

Alieleza kwamba katika kuhakikisha watoto wanapata heshima, fursa na haki zao zilizobainishwa ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010- 2015 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianzisha Mahakama ya watoto nchini ili kuongeza kasi ya uendeshaji kesi na ufanisi wa kesi zinazohusiana na masuala ya watoto.

Dr. Shein alisema Mahkama hizo zimejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya watoto ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa watoto ambayo yatawasaidia kuweza kujieleza sambamba na kutoa ushahidi bila ya hofu.

Alisema Mahakama hizo zinaenda sambamba na utolewaji wa mafgunzo kupitia Mabaraza ya Wazazi katika shehia mbali mbali juu ya malezi bora ya watoto na namna ya kuripoti matukio ya udhalilishaji.

“ Nimefurahi kuona kwamba leo tumezindua mtandao wa simu za huduma ya kwanza kwa wahanga wa masuala ya udhalilishaji wa wanawake na watoto { Helpline 116 } ambao naamini wengi wetu tunaiponga matendo machafu tulikuwa tukiusubiri kwa hamu “. Alisema Dr. Shein.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekikti wa Baraza la Mapinduzi aliipongeza Taasisi hiyo isiyo ya kiserikali ya C-Sema yenye makao makuu yake Dar es salaam kwa juhudi zake ilizotoa katika kuunga mkono mapambano dhidi ya udhalilishaji wa watoto na wanawake hapa Nchni.

Balozi wa Shirika la Kimataifa la kutetea haki za Watoto { Save The Children } ambae ni Mwanariadha mashuhuri wa Tanzania aliyewika katika mbio za Kimataifa Suleiman Nyambui alionya kwamba jamii isisubiri kuonywa au kuelekezwa juu ya kupiga vita Ndoa na Mimba za utotoni.

Suleiman Nyambui aliendelea kukemea tabia ya baadhi ya Makabila Nchini wenye kuendeleza mila potovu za kuwakataza watoto na wanawake kutokula baadhi ya vyakula vyenye siha na kujenga afya ni kuwanyima kahi yao ya msingi.

Akitoa salamu za Shirika la Kimataifa la Kutetea haki za Watoto { Save The Children } Mkurugenzi wa Shirika hilo Nchini Tanzania Steve Thorne alisema kwamba juhudi zinapaswa kuchukuliwa na taasisi tofauti kwa kushirikiana na Serikali katika kusaidia kuondosha vifo vya watoto.

Bwana Steve aliipongeza Tanzania kwa hatua yake iliyochukuwa na kufikia hatua ya nne katika mapambano yake dhidi ya vifo vya watoto kwa mujibu wa mpango wa Kimataifa wa Milenia wa kupunguza vifo hasa Barani Afrika.

Akimkaribisha Mgeni rasmi katika shamra shamra hizo Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Zainab Omar Mohammed alisema Mtoto za Kizanzibari lazima akuwe salama na kuepushwa na vikwazo ili apate nafasi ya kulitumikia Taifa lake kwa ufanisini.

Mh. Zainab alisema katika kufanikisha hilo aliwaombna wazazi lazima watenge muda wao kwa kucheza na watoto wao ili kukabiliana na changamoto la mtoto kulelewa na mmzazi mmoja tu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

                              Habari na: http://rweyunga.blogspot.com

Lifti Muhimbili zazua kasheshe

Image result for lifti muhimbili

Na Pamela Chilongola
Kwa ufupi
Wauguzi watumia ngazi kupanda na kushuka na maiti, wagonjwa. Kaimu mkurugenzi akiri lifti kutofanyakazi
Dar es Salaam. Lifti za wodi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zimeharibika na kusababisha wauguzi kulazimika kuwabeba wagonjwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Pia, wauguzi hao wanalazimika kuzibeba maiti kutoka wodini na kuzipeleka kwenye chumba cha kuhifadhi kupitia ngazi za hospitali hiyo kutokana na tatizo hilo la lifti na kuwasababishia adha kubwa.
“Kuharibika kwa lifti hizi kwa zaidi ya mwezi sasa kunasababishia kufanya kazi katika mazingira magumu hasa ya utoaji huduma kwa wagonjwa na ubebaji wa maiti,” alisema jana mmoja wa wauguzi wa wodi ya Kibasila, Afred Ismail.
Alisema mgonjwa mahututi akipelekwa kwenye wodi hiyo anatakiwa kulazwa chumba namba 16 ambacho kipo gorofa ya tatu wanalazimika kumweka chumba cha upasuaji ambacho kipo chini na kusababisha kutotibiwa kwa wakati.
“Wauguzi tuna wakati mgumu wa kazi, utakuta mgonjwa anatakiwa alazwe kwenye chumba namba 16 kutokana na lifti kuwa mbovu, tunashindwa kumpandisha kwenye ngazi hadi hapo tutafute watu zaidi ya saba wa kumbeba ili akapatiwe matibabu,” alisema Ismail.
Muuguzi Edita Amandous alisema wanapata wakati mgumu hasa mgonjwa anapofariki kwani kumtoa ghorofa ya tatu na kumshusha chini ili kumpeleka kwenye chumba cha mahututi wanalazimika kumbeba watu zaidi ya 10 kushuka kwenye ngazi.
Kaimu Mkurugenzi wa MNH, Dk Hussein Kidanto alisema hospitali hiyo ilijengwa miaka mingi iliyopita hivyo wanampango wa kuboresha wodi ya Kibasila, Mwaisela na Sewahaji ila wanasubiria fedha zilizotengwa kwa ajili ya hospitali hiyo.
Dk Kidanto alisema, suala la lifti ni tatizo kubwa hasa kwenye wodi ya Kibasila na Sewahaji hivyo uongozi wa hospitali hiyo wamekuwa wakitengeneza kwa gharama kubwa kutokana na kuwa chakavu kila wakati zimekuwa zikiharibika.
“Hizi lifti kila wakati tunazitengeneza na tunatumia gharama kubwa sana lakini sasa hivi tumejipanga kununua mpya na tunampango wa kujenga wodi ya ghorofa 10 ambayo itaondoa hii changamoto,” alisema Dk Kidanto.
Alisema changamoto zinazojitokeza zinasababishwa na ufinyu wa bajeti, hivyo fedha inayotengewa hospitali hiyo ni ndogo na kusababisha kushindwa kuboresha majengo na kununua vifaa vya hospitali hiyo.
                                                                  Habari kutoka: Gazeti la Mwananchi

Friday, 12 June 2015

WAONE MHE. LOWASSA USO KWA USO NA MHE.SAMWELI SITTA LEO LIVE..HEBU SIKIA KAULI ZAO

Leo tumekutana na ndugu yangu Mheshimiwa Samuel Sitta. Mimi na Sitta tumetoka mbali kikazi na kindugu. Tumefanya kazi pamoja bungeni, ndani ya CCM na serikalini kwa mafanikio makubwa.
Namtakia heri katika harakati zake huku nikiamini kwa dhati kwamba uhusiano wetu ndiyo msingi wa umoja na mshikamano ndani ya CCM na kwa taifa letu kwa siku zijazo.

Habari na masama Blog:

WEKA MAONI YAKO HAPA

Thursday, 11 June 2015

Mimba za utotoni, nani wa kumfunga paka kengele?

 
Na Lilian Timbuka
Kwa ufupi
Hiyo ni changamoto inayolikabili taifa, huku baadhi ya watu wakiliona kuwa ni jambo la kawaida na hulipuuza wakati wengine wanalikemea.

Kila kukicha kumekuwa na kesi za migogoro ya ardhi, mirathi na hata kesi za wazazi kuozesha mabinti zao wakiwa na umri mdogo licha ya suala hilo kupigiwa kelele muda mrefu.
Hiyo ni changamoto inayolikabili taifa, huku baadhi ya watu wakiliona kuwa ni jambo la kawaida na hulipuuza wakati wengine wanalikemea.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Haki za Binadamu Duniani(Amnesty) iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Tanzania ni moja ya nchi zinaoongoza kwa matukio ya mimba za utotoni.
Takwimu zinaonyesha kuwa, kwa siku, watoto 16 wanapachikwa mimba za utotoni.
Kwa mujibu wa wataalamu, hali hiyo imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu na kwa asilimia kubwa inazorotesha maendeleo ya mtoto wa kike.
Ili kumwokoa mtoto wa kike kutoka janga hilo, jitihada mbalimbali zimefanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali kuhakikisha inawaokoa hasa wale ambao tayari wameshatumbukia katika dimbwi hilo.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Chama chaWaandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), unaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2012/2013, matukio 228 ya mimba na matukio 42 ya ndoa za utotoni yaliripotiwa.
Hata hivyo, mimba na ndoa za utotoni zimetajwa kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyowapata watoto wa kike wa Tanzania, tatizo ambalo bado ni kubwa katika baadhi ya maeneo ya Tanzania Bara na Visiwani.
Mimba za utotoni na ukatili
Kwa kiasi kikubwa tatizo hilo linakwenda sanjari na ukatili wa kijinsia ambapo kwa Tanzania Visiwani hali hiyo imeonekana zaidi katika Mkoa wa Kusini Pemba na Wilaya ya Kati Unguja, huku upande wa Tanzania Bara maeneo yenye ukatili dhidi ya wanawake pamoja na mimba za utotoni yakitajwa kuwa ni Wilaya za Kahama, Tarime, Sengerema, Newala, Mbulu, Bunda, Nkasi, Babati, Chunya, Dodoma, Bariadi, Busega na Singida vijijini.
Bokhe Odhiambo (31), mkazi wa Tarime mkoani Mara, anasema kuwa vitendo vya ukatilli dhidi ya wanawake ndani ya ndoa na mimba za utotoni kwa watoto wa kike ni mambo ya kawaida na jamii inaonekana kuwa haina muda wa kuyakemea.
“Kupigwa au kufanyiwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ndani ya ndoa, migogoro ya ardhi na mimba za utotoni kwa watoto wa kike ni mambo ya kawaida tu kwenye jamii yetu licha ya wasaidizi wa kisheria kutoa elimu,” anssema Odhiambo.
Kutokana na changamoto hiyo, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) kimejitosa kutoa msaada wa kisheria katika mikoa yenye changamoto lengo likiwa ni kupunguza tatizo hilo.
Mwenyekiti wa Tawla, Aisha Bade anasema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo chama chake kimeamua kusambaza wasaidizi wa kisheria 400 nchi nzima lengo likiwa ni kusaidia kutatua migogoro ya ardhi na mirathi.
Bade anasema Tawla imebaini kuwa mikoa ya Pwani na Morogoro, Mtwara, Lindi, Arusha , Tanga, Shinyanga, Manyara na Mwaza inaongoza kwa kuwa na migogoro ya mirathi, vitendo vya ukatili na kuozesha watoto katika ndoa za utotoni.
Anasema kuwa mbali na mikoa hiyo pia mikoa ya Tanga, Arusha, Dodoma inaongoza kwa kuwa na migogoro ya ardhi pamoja na mirathi na hivyo juhudi mbalimbali zinahitajika kukabiliana na tatizo hilo. “Tumesambaza wasaidizi wa kisheria 400 nchi nzima lengo ni kutatua migogoro iliyopo hasa katika maeneo ya vijijini ambayo tumeona hayana msaada wa kisheria” anasema Bade.
“Mbali na mikoa hiyo pia mikoa ya Tanga, Arusha, Dodoma nayo ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kuwa na changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi na miradhi na kwamba juhudi za pamoja zinahitajika kushirikia katika kutatua changamoto hiyo ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea kutokana na tatizo hilo”anasema Beda.
Tawla imefanya nini?
Anasema kuwa Tawla ilianza mafunzo ya wasaidizi wa sheria mwaka 2006 na kutokana mafunzo hayo zaidi ya wananchi 4,600 wamenufaika kwa kupata msaada wa kisheria vijijini katika kipindi cha mwaka jana pekee.
John Maziku, mkazi wa mkoani Shinyanga, anasema kuwa utoro kwa wanafunzi a shule za sekondari na msingi ni tatizo linaloukabili mkoa huo kwa sasa na sababu kubwa ni wazazi kutokuwa karibu na watoto wao.
“Wazazi wengi wanakwenda migodini wanakaa huko kwa muda mrefu na hwakumbuki kama wana familia, mama anabakia na mzigo mkubwa wa kuitunza.
“Wazazi ndiyo chanzo kikubwa cha utoro katika wilaya ya Bukombe kwa sababu baba anapokwenda kwenye machimbo ya migodi hakumbuki kuwa wanaacha shule na kwenda kutafuta pesa,”anasema.
Mwajuma Mohamed (15), mkazi wa Ushirombo amekatiza masomo yake akiwa darasa la sita baada ya kupewa mimba na dereva wa magari makubwa. Hivi sasa ana mtoto wa miezi saba, lakini baba yake hajawahi kupeleka huduma ya mtoto.
Mchango wa Tamwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Valerie Msoka anasema wamefanya kampeni ya kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondai na msingi juu ya umuhimu wa elimu na madhara ya mimba za utotoni ambayo bado chama hicho kinaendelea nayo, lengo likiwa kuifikia mikoa yote nchini.
Anasema kwamba elimu hiyo imetolewa katika wilaya kumi za mikoa ya kusini ambayo ni Lindi na Mtwara na kwamba mikoa ya Pwani na Dar es Salaam imepata elimu hiyo kupitia mradi wa GEWE, unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Denmark (Danida).
“Elimu inayotolewa kwa wanafunzi inalenga kumwezesha mwanafunzi namna ya kujitambua na kujua malengo ya elimu aipatayo itamsaidiaje katika maisha yake ,” anasema Msoka.
Anasema mafunzo hayo ni kitu cha muhimu na yatachangia maendeleo ya mwanafunzi hapo baadaye.
“Hata kama wazazi wanapomlazimisha kuolewa, binti anatakiwa kukataa ili aweze kumaliza elimu yake vizuri,” anasema Msoka na kuongeza: “Kazi hii ya kupambana na janga hili ni lazima pia lifanywe na wanasiasa hasa katika kipindi hiki tunachoelekea katika Uchaguzi Mkuu.” Anabainisha kuwa miongoni mwa wanasiasa imejengeka tabia ya kutotilia maanani matatizo kama ya unyanyasaji wa kijinsia, hasa kipindi kama hiki wakihofia kukosa kura.
“Ninawasihi wanasiasa, waache tabia ya kufumbia macho matatizo yanayowakabili wapiga kura wao bali wayatafutie ufumbuzi,” anasema Msoka.
Hata hivyo, swali linalobaki ni nani wa kulaumiwa kwa mimba za utotoni; ni nani wa kuwafichua watuhumiwa na kukomesha ouvu huo, nani wa kumfunga paka kengele?
                                                        Habari hii imepatikana katika gazeti la Mwanannchi.

WILAYA YA LUDEWA YAANDAA MPANGO WA KUKUZA SEKTA YA ELIMU

                                   Bw.Haji Mnasi ofisa elimu shule za msingi wilaya ya Ludewa

 Bw.Haji Mnasi ofisa elimu shule za msingi wilaya ya Ludewa akiongea na mwandishi wa habari Bw.Bazil Makungu

                                                 hii ni baadhi ya nyumba ya mwalimu 
                              Deo Filikunjombe akiongea na watendaji wa Srikali wilayani Ludewa
Mwalimu Kayombo wa shule ya msingi Masi mavalafu  mwenye shati nyeupe akitoa malalamiko ya makato ya kodi ya nyumba za walimu kwa katibu wa ccm wilaya ya Ludewa Bw.Lusiano Mbosa
 Diwani wa kata ya Ibumi Bw.Haule mwenye suti akimkabidhi zawadi ya mbunga mbunge wa jimbo la  Ludewa Deo Filiknjombe katika kijiji cha Masi mavalafu
 Filikunjombe akiongea na wananchi wa Masi mavalafu kuhusiana na shida wanazozipata walimu na utatuzi wake


Halmashauri ya wilaya ya Ludewa katika mkoa wa Njombe kupitia Idara ya elimu imeandaa mpango mkakati wa kukuza kiwango cha elimu katika ufaulu ili kushindana na wilaya zingine katika mkoa huu kwani wilaya ya Ludewa imekuwa na kiwango cha chini kwa miaka mingi na kusababisha baadhi ya wananchi kuiona idara ya elimu haifanyi kazi kwa kiwango kinachoridhisha.

Akiongea na wanahabari ofisini kwake ofisa elimu shule za msingi wilaya ya Ludewa Bw.Haji Mnasi alisema kuwa wilaya ya Ludewa imekuwa na matokeo mabaya kwa muda wa miaka mingi kutokana na changamoto mbalimbali hivyo ofisi yake kupitia wataalamu wa elimu umeandaliwa mpango mkakati utakao ivusha elimu kutoka kiwango cha hali ya chini na kuongeza ufaulu kama wilaya nyingine mkoa wa Njombe.

Bw.Mnasi alisema kuwa wilaya ya Ludewa ni wilaya kama nyingine nchini hivyo hakuna sababu ya kila mwaka kushika nafasi za mwisho kimkoa na kitaifa katika ufaulu wa wanafunzi kwani idara yake imeshazibaini changamoto zinazosababisha kutokea kwa hali hiyo na tayari suruhisho limepatikana la kukomesha hali hiyo.

Alisema kuwa mpango ulioandaliwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika shule zote kupitia idara ya ukaguzi na kuhakikisha kila shule inakuwa na walimu wakutosha kwani awali kuna baadhi ya shule zilikuwa na walimu wengi na nyingine zilikuwa na hali mbaya zaidi kutokana na kuwa na mwalimu mmoja hivyo zilishindwa kutoa elimu nzuri hali iliyopelekea kutofaulisha wanafunzi.

“Idara ya ukaguzi imekuwa na hali ngumu ya kifedha hivyo ilipelekea kushindwa kufanya kazi yao vizuri lakini hata mimi mwenyewe nitapita vijijini na kuzitembelea shule mara kwa mara  ili kuleta ufanisi wa kielimu licha ya kuwa mazingira ya Ludewa ni magumu kutokana na vijiji kuwa mbalimbali hivyo inatulazimu kutumia gharama nyingi katika ufuatiliaji lakini naamini tutafanikiwa tu”,alisema Bw.Mnasi.

Bw.Mnasi alisema kuwa wilaya ya Ludewa kuna baadhi ya kata hazifikiki kwa kutumia usafiri wa gari hasa kata za mwambao wa ziwa Nyasa hivyo hulazimika kutumia boti ambayo inagharimu fedha nyingi hasa katika ununuzi wa petroli lita 200 kwa safari moja na kutokana na bajeti ya Serikali kuwa ndogo katika ufuatiliaji kwa namana hiyo ukaguzi ulifanyika zaidi kata za jirani kutokana na ufinyu wa bajeti.

Kuhusu baadhi ya walimu wapya kukataa kufanya kazi katika baadhi ya maeneo kutokana na ugumu wa mazingira Bw.Mnasi alisema kuwa halmashauri inaandaa mipango ya kutoa motisha kwa baadhi ya walimu wanaofanya kazi katika mazingira magumu ili kuinusuru elimu wilayani hapa ambapo miaka ya nyuma wilaya ya Ludewa ilisifika kwa kutoa wasomi wazuri ambao walisoma katika mazingira hayo na walimu waliweza kuishi popote bila malalamiko.

Bw.Mnasi alisema kuwa Serikali imeshawaleta walimu wapya 42 katika wilaya ya ludewa na tayari wameshaanza kuripoti wilayani hapa lakini mpango wa idara ya elimu kwa mwaka huu ni kuwasambaza walimu hao katika tarafa ya Masasi na Mwambao ambako ndiko kunauhaba mkubwa wa walimu kwa miaka mingi licha ya kuwa wanafunzi wanaotoka maeneo hayo wamekuwa na uwezo mkubwa kielimu kwa kuwatumia walimu wachache waliokuwa nao.

Wilaya ya Ludewa imekuwa na changamoto kubwa katika idara ya Elimu kutokana na halamshauri ya wilaya hii kupitisha sheria ya kuwakata fedha za malipo ya Nyumba wanazoishi walimu hata kama nyumba hiyo ni mbovu huko vijijini kila mwalimu anakatwa kiasi cha shilingi elfu kumi kwa mwezi hali ambayo imekuwa ni kero kwa walimu hao na kuwafanya kukata tamaa ya utendaji katika maeneo yao ya kazi.

Kutokana na hali hiyo inayowakumba walimu mbunge wa jimbo la Ludewa Mh.Deo Filikunjombe ameitaka Halmashauri kutengua sheria hiyo ili kuwapatia unafuu wa maisha walimu hao kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili kwani halmashauri inaweza kubuni vyanzo vingine vya mapato na si kuwakamua walimu ambao ilipaswa wapate motisha katika kazi yao.

Mh.Filikunjombe aliyasema hayo katika kijiji cha ibumi ambako alikutana na changamoto hiyo kwani baadhi ya walimu walimweleza kuwa Serikali ya halmashauri inawapuuza na kuwanyonya kwa kuwatoza nyumba zisizo na kiwango cha kuishi walimu kwani nyumba nyingi wanazoishi vijijini hazina sakafu wala mifuniko ya madirisha hali ambayo ni hatari kwa walimu.

Mh.Filikunjombe alisema kuwa kimsingi Halmashauri inapaswa kutoa motisha kwa walimu hao kwani wengi wao wanaishi mbali na makao makuu ya wilaya hali ambayo huwalazimu wakati wa mwisho wa mwezi kutumia robo ya mshahara wao katika usafiri wanapofuata mishahara wilayani hali ambayo si kweli.

Mbunge huyo alisema kuwa anaandaa mpango wa kukutana na walimu wote wa wilaya ya Ludewa ili kuweza kuzungumza nao na kumshawishi mkurugenzi wa halmashauri kuwarudishia fedha zao wale waliokatwa kimakosa kwani kunabaadhi ya walimu vijana wanaishi watatu hadi wanne katika nyumba moja lakini kila mmoja anakatwa kiasi cha shilingi elfu kumi kwa mwezi.

Mwisho.

                                              Habari na: Habari Ludewa Blog.

  MANGULA ATAJA VIGEZO 13 VYA MGOMBEA URAIS WA CCM..NI HIVI HAPA

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula amesema vigezo 13, vitatumika kuwachuja wanachama wa chama hicho ambao wameomba kugombea urais CCM.

Alisema hayo jana mjini hapa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya CCM mjini Dodoma.

Aliwakumbusha watangaza nia kuwa hawaruhusiwi kutoa rushwa, kushawishi au kushawishika kuwapa rushwa wale wanaowadhamini.

Vigezo vyenyewe
Alitaja vigezo 13 vitakavyotumika kuwachuja wagombea kuwa ni uwezo mkubwa na uzoefu katika uongozi, uadilifu, unyenyekevu na busara.

Pia, kuwa na elimu ya chuo kikuu au inayolingana na hiyo, mtu mwenye upeo mkubwa wa kuimarisha na kuendeleza Muungano, umoja na amani.

“Anatakiwa kuwa na upeo mkubwa usiotiliwa mashaka kuhusu masuala ya kimataifa, asiye na hulka ya kidikteta au mfashisti, awe tayari kulinda kanuni, sheria na utawala bora,” alisema Mangula.

Alitaja vigezo vingine ni kuwa mtetezi wa wanyonge na haki za binadamu na asiwe na tamaa ya kujipatia umaarufu, kuzifahamu, kuzitetea, kutekeleza sera na Ilani ya CCM, mpenda haki na ajue kupambana na dhuluma, asiwe mtu anayetumia nafasi ya uongozi kujilimbikizia mali.

“Awe ni mtu makini anayezingatia masuala ya uongozi,” alisema.

Alisema katika kipindi hiki cha mchakato wa uteuzi, kanuni zitakazotumika ni zile Kanuni za Uteuzi wa Wagombea katika Vyombo vya Dola, zilizotolewa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ya mwaka 2010.

Pia, katika kipindi hiki cha mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola, ni sehemu ya kazi za chama ndani ya chama. Alisema vikao vya uchujaji, vitazingatia pia Kanuni za Uongozi na Maadili Toleo la mwaka 2012.

Alisema kipindi ambacho CCM hudhihirisha dhana ya kazi ya msingi na muhimu katika kujenga uongozi mmoja katika chama, kazi ya kutekeleza kwa dhati kanuni na demokrasia na nidhamu ndani ya chama.

Alisema kanuni hiyo, ndiyo inakiwezesha chama hicho kuwa cha demokrasia na papo hapo kuwa chombo cha kuongoza mapinduzi kutokana na nidhamu yake inayokipa uongozi moja katika vitendo.

Alisema miiko ya shughuli za uchujaji na uteuzi wa wagombea, itazingatiwa. maadili na nidhamu ya chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola, lazima vizingate na wale wote wanaohusika.

“Ni mwiko kwa kiongozi yeyote kwa maneno au vitendo kumpendelea au kumsaidia kupata kura nyingi mwombaji mmoja dhidi ya mwingine.”

Alisema Chama kinakataza mgombea kutumia au kuhusisha ukabila, dini, rushwa, rangi, hila na eneo analotoka katika shughuli yoyote ya uchaguzi.

Alisema ni mwiko kwa mgombea kufanya kampeni ya kupakana matope na ya aina nyingine yoyote ile dhidi ya mgombea mwingine.

Aidha, alisema ni mwiko kwa kiongozi yeyote au mwombaji yeyote wa nafasi ya uongozi, aliyekabidhiwa dhamana ya usimamizi, uangalizi, uchujaji na uteuzi, kufanya vitendo vya ukiukaji wa kanuni ambazo ni Katiba ya CCM, sheria, ratiba na taratibu za uteuzi.

Mangula alisema kwa mujibu wa kanuni za uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola, kutangaza nia kunaruhusiwa kwa masharti, ikiwemo bila kuathiri haki ya mwanachama ya kutangaza nia wakati wowote nia yake ya kutaka kugombea nafasi fulani ya uongozi katika vyombo vya dola, lakini kwa kuwa nafasi hizo zimewekwa muda maalumu wa miaka mitano.

Alisema wakati wa kutafuta wadhamini 450, kila anachokifanya mwana CCM anayetafuta wadhamini, kitaingia katika kumbukumbu za tathmini ya mgombea mtarajiwa.

Pia, alisema kamati za maadili za wilaya, zikutane mara baada ya wagombea watarajiwa kujaza majina ya wadhamini wilayani. Alisema mpaka sasa wagombea urais waliojiandikisha wamefikia 22 na wengine bado wanakwenda.
HABARI NA MASAMA BLOG

WEKA MAONI YAKO HAPA

Wednesday, 10 June 2015

ANGALIA HAPA KUONA NAFASI ZA AJIRA KUTOKA JESHI LA POLISI 2015

ANGALIA HAPA KUONA NAFASI ZA AJIRA KUTOKA JESHI LA POLISI 2015


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
TANGAZO LA AJIRA
Jeshi la Polisi Tanzania linatangaza nafasi za ajira kwa mwaka wa fedha 2015/2016 kwa vijana wenye elimu ya vyuo vya elimu ya juu, waliosomea ujuzi/fani mbalimbali toka vyuo vinavyotambuliwa na Serikali na wahitimu wa kidato cha sita wa mwaka 2014 waliopitia Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria. Wahusika watajaza fomu baada ya kujazwa kikamilifu wataambatanisha vivuli vya vyeti na kutuma Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa njia ya Posta kabla ya tarehe 31/06/2015. Kwa anuani ifuatayo:
Inspekta Jenerali wa Polisi,
Makao Makuu ya Polisi,
S.L.P. 9141,
DAR ES SALAAM.
SHAHADA
Maendeleo ya Jamii(Community development),Ushauri Nasihi [Counselling Psychologist](2) Uchumi(Economy)(10)Ualimu(Education)(2)Menejimenti ya Rasilimali watu(HRM), Utawala katika Utumishi wa Umma(Public Administration)(3) Usimamizi na Utekelezaji wa Sheria[BaLE](12) Sheria (LLB)(2) Uandishi wa Habari(2) Uhandisi Mitambo[Mechanical Engineer](5) TV & Redio Production(5)Ugavi[BA In Procurement & Supplies](2) Mazingira[BA in Environmental Disaster Mgt](5) Uchoraji[BA in Fine Arts](5) Mkemia, Bailojia[Molecular Biology] (10)Kada za Afya(10)Uhandisi Madini[Mining Engineer](5) Land Surveyor(2) Madaktari wa Wanyama(5) Wataalamu wa Ujenzi Mafundi AC(2) Architecture(2) Quantity Surveyor(2) Civil Engineer(2)
STASHAHADA
Utunzaji Kumbukumbu(30) Katibu Muhtasi[Personal Secretary](30) Matengenezo ya kompyuta, Photocopy machines na Fax(10) Mafundi Mitambo wa meli(2) Kada za Afya(5) Wataalamu Magari na Pikipiki Mafundi Umeme wa Magari(5) Mafundi Magari(5) Manahodha(5) Ugavi(2) Mawasiliano[Diploma in RadioCommunication](20) Madaktari wa wanyama(2) Land Surveyor Cathographer (2) Mafundi AC(2) Wataalam ujenzi Hydro Geology Drilling Well(2) Architecture Draftman(2) Civil Engineer(2)ASTASHAHADA(NTA level 3 or 4
Wataalamu Magari na pikipiki Mafundi Pikipiki(4) Mafundi Umeme wa Magari(4) Mafundi Magari(4) Mafundi Rangi za Magari (Spray Painting)(4) Madereva wa magari(50) Mafundi Unyooshaji wa Body (Panel Beating)(5) Mafundi A/C(3) Mafundi Ushonaji (10)Wataalamu wa GIS Cathographer(2) Land Surveyor(2) Madaktari wa Wanyama (3) Refridgeration & Air Condition(2) Motor Rewinding(2) Wataalamu wa Ujenzi Welding & Fabrication(2) Generator Maintenance(2) Electrical(3) Masonry (2) Painting(3) Aluminium & Glass Work(2) Plumbing(2) Wataalamu wa muziki Brass bandi (5) wood wind (5) String jazz (3) Percussive (2)
MASHARTI KWA MWOMBAJI
1. Mwombaji atajaza fomu ya maombi kikamilifu na atabandika
picha yake “Ppt Size” kwenye fomu.
2. Mwombaji aambatanishe katika fomu vivuli vya vyeti vyote
yaani cheti cha kuzaliwa, kuhitimu elimu ya sekondari[Leaving
& Academic], cheti/vyeti vya taaluma[Academic Transcript] na cheti cha
kumaliza Jeshi la kujenga taifa kwa wahitimu wa kidato cha sita.
3. Hati ya kiapo cha kuzaliwa haitakubalika.
SIFA ZA MWOMBAJI
1. Awe Mtanzania kwa kuzaliwa.
2. Awe na umri usiopungua miaka 18 na usiozidi miaka 25 kwa wahitimu wa
astashahada, stashahada na kidato cha sita.
3. Kwa wahitimu wa shahada awe na umri usiopungua miaka 18 na usiozidi
miaka 28.
4. Awe amehitimu chuo mwaka wa masomo 2014 tu.
5. Kwa wahitimu wa kidato cha sita awe amehitimu mwaka 2014 na kupitia
Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria
6. Awe na tabia njema.
7. Asiwe na kumbukumbu za kutenda uhalifu.
8. Awe na afya njema[kimwili na kiakili]
9. Awe hajaoa/hajaolewa au kuwa na mtoto.
10. Asiwe na alama za kuchora mwilini[tatuu].
11. Awe na urefu usiopungua sentimita 155 futi tano nchi mbili
12. Asiwe mtumiaji wa madawa ya kulevya.
13. Awe hajaajiriwa na idara nyingine Serikalini.
14. Awe tayari kuhudhuria mafunzo ya awali ya Polisi.
15. Awe tayari kufanya kazi popote ndani na nje ya Tanzania.
Imetolewa na
Makao Makuu ya Polisi(T)
DAR- ES- SALAAM.

WEKA MAONI YAKO HAPA 

Habari na Masama Blog

Monday, 8 June 2015

MASKINI:MUONE HUYU PADRE NA WANAFUNZI SITA WALIVYOTETEKETEA KWA MOTO

MASKINI:MUONE HUYU PADRE NA WANAFUNZI SITA WALIVYOTETEKETEA KWA MOTO

WANAFUNZI sita wa Sekondari ya CTC Kigonsera inayomilikiwa na Misheni ya Mbinga mkoani Ruvuma na Mkuu wa Shule hiyo, Padre Yazint Kawonga, wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutumbukia bondeni kisha kuwaka moto na kuiteketeza miili yao.


Akizungumza na Mpekuzi juzi shuhuda wa ajali hiyo, Makarius Nchimbi, alisema ilitokea juzi saa tisa alasiri katika mlima uliopo karibu na shule hiyo huku likiwa limewabeba wanafunzi waliokuwa wakitokea shambani kuvuna mahindi ya shule hiyo.


Nchimbi ambaye ni mfanyakazi wa kitengo cha udereva katika misheni hiyo alidai yeye ndiye aliyekuwa dereva wa gari hilo kabla ya kupokelewa na Padre Kawonga aliyemtaka amsaidie kuliendesha kwa kuwarudisha shuleni wanafunzi waliokuwa shamba lililopo Kijiji cha Mkulumus kilichopo Kigonsera.


Alisema gari hilo aina ya Land Rover 110 Station Wagon lenye namba T 306 AYM  lilipofika katika mlima huo lilimshinda Padre Kawonga wakati akitumia gia namba mbili na kuanza kurudi nyuma huku wanafunzi wengine waliokaa juu walifanikiwa kuruka kabla halijatumbukia na baadhi yao 24 waliumia.


Alisema baada ya gari hilo kutumbukia bondeni wao walijitahidi kuingia kwenda kuvunja milango ili waweze kuwaokoa baadhi yao lakini ilishindikana kutokana na nyaya za umeme wa gari kulipuka na kuliunguza huku miili yao ikiwemo ndani  na kusababisha ishindwe kutambulika.


Alisema kutokana na moto kuwaka iliwalazimu watafute mbinu za kuuzima na walitumia maji lakini haikuwezekana na walifanya jitihada ya kuipata winchi iliyoweza kwenda kuliinua gari hilo likiwa limeteketea.


Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Kigonsera, Dk. Patrik Mhagama, alisema kituo hicho kilipokea maiti saba na majeruhi wakiwa 24 na kati ya hao wawili wamepekwa Hospitali ya Mbinga kutokana na hali zao kuwa mbaya huku 17 walitibiwa na kuruhusiwa na watano bado wapo kituoni hapo.


Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikihela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na alisema taratibu za kuyapata majina halisi ya marehemu bado zinaendelea na zikikamilika zitatolewa taarifa.


Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Japheth Komba (16), Regobert Mahai (16), Edgar Maseko (16), Luiza Mbunda, Afa Kifaru (15), Nelalfred Nchimbi (16), Teodora Wolfa (16).
Habari na Masama blog