Dar es Salaam. Kasoro za
uandikishaji wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura zilizokuwa
zikitokea katika mikoa mbalimbali nchini, zimejitokeza pia jijini Dar es
Salaam ikiwa ni siku ya kwanza ya kazi hiyo.
Mwananchi
ilipita katika maeneo mbalimbali jana na kushuhudia wananchi wengi
wakiwa wamekutana na changamoto kadhaa kwenye baadhi ya vituo ikiwamo ya
kukosekana mashine za Biometric Voters Registration (BVR).
Wananchi
hao walisema licha ya kwamba Dar es Salaam imepewa siku 10 ya
uandikishaji, kama changamoto hizo hazitachukuliwa hatua kazi hiyo
inaweza isikamilike kwa wakati.
Miongoni mwa changamoto
nyingine ni kuharibika kwa mashine zilizopo, ukosefu wa umeme, uchache
wa watendaji na kuelemewa na watu, mtandao usio wa uhakika na nani aanze
kuandikishwa kati ya wenye mahitaji maalumu na wasionayo.
Katika
kituo cha uandikishaji cha Shule ya Msingi Oysterbay ambako kuna vituo
vidogo vitano, wakala wa uandikishaji, Margereth Galway alisema mwitikio
wa vijana umekuwa mkubwa kiasi kwamba inakuwa shida kuwapa nafasi ya
upendeleo wazee, viongozi, walemavu au wajawazito na wanaonyonyesha.
“Eneo
hili lina wazee na viongozi wengi wa chama na Serikali. Mwitiko mkubwa
wa vijana unatufanya tushindwe kuwasaidia watu hao,” alisema Galway.
Alisema
wasimamizi wote wa kituo hicho wamekubaliana kuwa kuanzia leo, wateue
mashine moja na itengwe kwa ajili ya wenye mahitaji maalumu ili
kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi wanaokuwa wamesimama kwenye
foleni muda mrefu.
“Tayari wameshakuja Warioba (Jaji
Joseph), Msekwa (Pius) na Butiku (Joseph) wakiwa na wake zao na
kujiandikisha. Pamoja na kufahamika kwao bado vijana hawakuwa radhi
kuwapisha wakitaka wajipange jambo ambalo ni gumu kulitekeleza.
“Kama
tutafanikiwa kuwashawishi waandikishaji basi foleni za watu wa kawaida
zitakuwa nne na moja itaachwa kwa ajili ya wenye mahitaji muhimu,”
alisema.
Katika Kituo cha Shule ya Msingi Kawe A, wazee
wengi walikutwa wamekaa kwenye madawati, nje ya madarasa wakisubiri
kuandikishwa baada ya vijana kutokubali kuwapisha wakidai waandaliwe
utaratibu ambao hautoingilia foleni iliyopoo.
Katika
Shule ya Msingi Hekima iliyopo wilayani Kinondoni, kulikuwa na
malalamiko kama hayo na wananchi wakaiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) kuweka utaratibu maalumu.
Mmoja wa waliofika
kujiandikisha, Mwanaidi Abdallah alisema katika uandikishaji huo
wanawake wamekuwa wakipata shida kutokana na utaratibu mbovu.
Alisema inachukua muda mrefu kupata huduma kwa sababu baadhi ya vijana wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kujiandikisha.
Katika
kituo cha Mtendaji kilichopo Mtaa wa Mzimuni, Kata ya Kawe, wananchi
walikutwa wakiwa nje saa 8:00 mchana wakisubiri mashine ili uandikishaji
uanze licha ya kutangaziwa kazi hiyo ingeanza asubuhi.
Kitu
pekee kilichokuwa kinaendelea ni wananchi kujiorodhesha kwenye daftari
na kupewa namba ya foleni hadi mashine zitakapoletwa.
Mkazi
wa Ununio Beach, Joseph Mrisho alisema licha ya wananchi kujitokeza kwa
wingi kuna vituo viwili mashine ziligoma kufanya kazi.
Mwenyekiti
wa Serikali ya Mtaa wa Ununio Beach, Mwijuma Mwinyihija alisema
usumbufu waliokumbana nao wananchi umesababisha malalamiko na wengine
wamekataa tamaa na kuamua kuondoka kwenda kwenye shughuli zao za
kujitafutia kipato.
Katika Kata ya Wazo Mtaa wa
Salasala eneo la IPTL, hadi saa 9:00 alasiri wananchi walikuwa
hawajaandikishwa kutokana na mashine kugoma.
Mkazi wa
eneo hilo, Blandina Hizza alisema alilazimika kurudi nyumbani mara
kadhaa akijipa matumaini huenda mashine hiyo itatengemaa ili
aandikishwe, lakini hadi muda huo hakufanikiwa.
Frank Etta alisema: “Hatuelewi imekuwaje hadi sasa wahusika hawajaleta mashine.”
Kituo
cha Shule ya Msingi Mlimani kilichopo katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam ambacho kinastahili kuwa na vituo vidogo vitatu, kina mashine
moja tu iliyopelekwa.
Mwandikishaji Msaidizi katika
kituo hicho, Isabella Mkumbwa alisema mwitikio wa watu ni mkubwa, lakini
uandikishaji unakwenda taratibu kwa sababu watu wote wanatakiwa
kusubiri mashine moja.
“Baadhi ya watu wameondoka ili
wakaendelee na kazi zao. Tunasubiri mashine nyingine mbili ziongezwe
wakati tukiendelea kuitumia hii iliyopo,” alisema msimamizi huyo.
Kituo
cha Shule ya Sekondari Zawadi kiliyopo Tabata, uandikishaji ulikuwa
haujaanza hadi saa 4:00 asubuhi wakati gazeti hili lilipotembelea
kituoni hapo na kukuta mashine ikitengenezwa.
“Niliwahi
kufika na nikapewa namba 23 ila tumeelezwa kuwa walimu wataanza
kuandikisha pindi mashine zitakapotengamaa. Wamesema kuwa zimegoma
kutokana na mtikisiko wa kusafirishwa kutoka mikoani,” alisema James
Mwandumbya aliyefika kujiandikisha.
Maeneo ya Pugu
Kigogo Fresh (Stesheni) waandikishaji walielemewa na wingi wa watu na
kulazimika kutoa namba ili wengine waende siku nyingine.
Katika
kituo cha Shule ya Msingi Mtambani, Kinondoni, wananchi walilalamika
gharama za uendeshaji ambazo wameombwa wachangie ili kufanikisha
uandikishaji uendelee kama ulivyopangwa.
Katika Kituo
cha Shule ya Msingi Makuburi, Ofisa mwandikishaji, Karim Mweneghoha
alisema walikumbwa na changamoto ya umeme iliyochangiwa na kukosekana
kwa waya za kuunganisha kutoka kwenye soketi kwenda kwenye mashine.
Mkurugenzi
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Julius Mallaba alikiri kupokea taarifa
kutoka katika baadhi ya maeneo na kudai kuwa tayari ufumbuzi
umepatikana.
“Kuna taarifa nilipokea asubuhi kwamba
uandikishaji unaendelea, ngoja niwasiliane na ofisa uandikishaji ili
nijue (changamoto) ndipo niweze kuzungumzia vyema jambo hili,” alisema.
Awali, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo ndiyo inahusika na
shughuli hiyo ilisema mashine zaidi ya 8,000 zitatumika ili kufanikisha
shughuli hiyo baada ya kukamilika uandikishaji mikoani.
Imeandikwa na Beatrice Moses, Julius Mathias, Bakari Kiango na Colnely Joseph.
Habari toka: http://www.mwananchi.co.tz
Habari toka: http://www.mwananchi.co.tz