Albino wamtoa chozi Kikwete
Posted Jumapili,Juni14 2015 saa 8:56 AM
Kwa ufupi
Akizungumza katika maadhimisho ya kimataifa ya siku
ya kuongeza uelewa wa albino duniani, katika Uwanja wa Sheikh Amri
Abeid, Rais Kikwete alisema mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi
yanayoendelea nchini yanamsononesha na kulitia doa Taifa.
Akizungumza katika maadhimisho ya kimataifa ya
siku ya kuongeza uelewa wa albino duniani, katika Uwanja wa Sheikh Amri
Abeid, Rais Kikwete alisema mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi
yanayoendelea nchini yanamsononesha na kulitia doa Taifa.
Rais Kikwete alisema wimbo wa watoto wenye albino
kutoka Tanga, ulivyoanza alianza kuhisi angetokwa machozi na baadaye
alishindwa kujizuia na kutokwa na machozi.
“Hawa watoto wameimba mambo ambayo yamenigusa
sana, na tumepokea kilio chenu kwa umuhimu mkubwa na ninaahidi
tutashirikiana kuyashughulikia matatizo yenu,” alisema.
Alisema suala la matibabu ya albino ni jambo
ambalo linashughulikiwa, ili kuhakikisha vifaa tiba ambavyo vinahitajika
hasa kutibu magonjwa ya ngozi vinapatikana na kuwawezesha kupata
matibabu bure.
Akizungumzia hatua za Serikali, Rais Kikwete
alimpa nafasi Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe kueleza hatua
zilizofikiwa katika kuunda kamati ya kitaifa ya kuishauri Serikali.
Waziri Chikawe alieleza kuwa tayari wizara yake,
imekamilisha mchakato wa kuunda kamati hiyo, ambayo itakuwa na wajumbe
15, watano kutoka chama cha wenye albino, watano chama cha waganga wa
jadi na watano kutoka serikalini.
Awali Mwakilishi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la
Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unicef) nchini, Zulmira Rodrigues aliiomba
Serikali kuwaondoa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) waliowekwa
katika vituo maalumu, kwa kuwa kitendo hicho kinawanyanyapaa.
Akizungumza katika mkutano uliokuwa wa kuelezea
maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelimishaji kuhusu albino jijini
hapa jana, Rodrigues alisema vituo hivyo vinaweza kutumika kwa ajili ya
kuwahifadhi albino kwa muda mfupi na si kuvifanya suluhisho la kudumu
litakalowapa ulinzi.
“Kuwatenga albino na kuwaweka katika vituo ambavyo
wanaishi pekee yao ni kukiuka haki za binadamu na kuwanyima uhuru wao,
badala yake jamii iwatengenezee mazingira mazuri yatakayowafanya waishi
kwa usalama kama watu wengine,” alisema Rodrigues.
Imeandikwa na Goodluck Eliona (Dar) na Mussa Juma na Bertha Ismail (Arusha).