Kuna kila dalili kwamba mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa Zanzibar yamevurugika baada ya wahusika wakuu wa pande mbili, kuzungumza hadharani na kutoa misimamo tofauti.
Wakati Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF akiitisha mkutano wa waandishi wa habari Dar es Salaam jana na kusema chama chake hakipo tayari kuona uchaguzi unarudiwa, Dk Ali Mohamed Shein wa CCM amewataka wafuasi wa chama hicho kujiandaa kwa uchaguzi wa marudio.
Akihutubia mkutano maalumu wa CCM wa maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, uliofanyika Viwanja vya Maisara Suleiman, mjini hapa, Dk Shein amewataka wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio pindi Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) itakapotangaza tarehe.
Rais huyo wa Zanzibar alisema jana kwamba huo ndiyo msimamo wa chama chake na hakijatafuna maneno tangu ZEC ilipotangaza uamuzi wa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015