LILE sakata la mtoto wa miezi 6 (pichani) kufia
mahabusu ya Kituo cha Polisi cha Kova, Mbezi Kwamsuguri, Dar
linaendelea! Safari hii, mama wa mtoto huyo, Meradi Meshack ameibua
mazito akiwataja polisi jamii kuwa ndiyo chanzo cha kifo cha mwanaye.Ψ
Awali ilibainika kuwa, mtoto huyo aliyefariki dunia Novemba 18, mwaka
huu wakati mama yake akiwa amewekwa kituoni hapo kama mhalifu, polisi
wa kituo hicho walitajwa kuhusika.
Akizungumza na waandishi wetu, mama huyo alisema yeye na mtuhumiwa wake aliyemtaja kwa jina la mama Na walikuwa wakidaiana fedha za upatu ambazo alikuwa akimdanganya kuwa wanachama wenzake bado hawajatoa.
Akizungumza na waandishi wetu, mama huyo alisema yeye na mtuhumiwa wake aliyemtaja kwa jina la mama Na walikuwa wakidaiana fedha za upatu ambazo alikuwa akimdanganya kuwa wanachama wenzake bado hawajatoa.
Baada ya usumbufu wa muda mrefu ndipo wakapishana maneno, mwanamke
huyo akampeleka polisi akidai alitaka kumpiga. “Nilifuatwa na polisi
jamii wawili na si polisi wenyewe. Mimi nilikuwa na mume wangu,
niliwaambia mwanangu anaumwa nitakwenda kesho lakini hawakukubali,
wakanitukana na kunichukua kwa mabavu huku mwanangu akiwa na hali mbaya
na walimuona..
“Shangazi yangu na mume wangu walinifuata wakitaka kuniwekea dhamana,
wale polisi jamii wakakataa, wakanitupa mahabusu. Mwanangu akazidi kuwa
na hali mbaya zaidi maana hali ya hewa mle mahabusu ilikuwa ni nzito
sana.
“Usiku nilipitiwa na usingizi, niliposhituka usiku wa manane
nikamuona akikohoa na kupumua kwa shida, baadaye akalegea na kuwa kama
amelala, nikawaita wale polisi jamii lakini hawakuja. “Ndipo alfajiri,
mmoja wao akaja, akanitazama kisha akaondoka zake. Akaja mwingine,
akamshika mwanangu akawa kama ameshtuka, akaniambia niondoke haraka
nimpeleke hospitali
“Kumbe wakati anasema hivyo alishajua mwanangu amefariki dunia,
inauma sana kwa kweli! Nilitoka na kilio kwani nilishampoteza mtoto
wangu na wao sikuwaona tena! Walikimbia! Huu ni ukatili wa hali ya juu,”
alisema mwanamke huyo.
Naye mjumbe wa eneo hilo, Rashid Sultan alisema taarifa za kifo cha
mtoto huyo alizipata na kuwatupia lawama polisi jamii waliojichukulia
uamuzi wa kumweka mahabusu mwanamke huyo tena akiwa na mtoto mchanga
wakati kituo hicho ni kidogo na hakilazi wahalifu nyakati za usiku na
hutakiwa kufungwa saa 12 jioni.
Inadaiwa kuwa, chanzo cha mtoto huyo kufariki dunia ni kukosa hewa
huku akiwa anasumbuliwa na kifua. Hadi Uwazi linakwenda mitamboni,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura hakuwa akipatikana
kwenye simu yake ya mkononi ili kuelekeza anachokijua.