Na John Nditi ,Morogoro
MEYA wa Halmashauri ya Manispaa Morogoro , Amir Nondo (45), dereva na waandishi wa habari wawili wamepata ajali baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongwa na basi la abiria lenye namba za usajili T 831 CEH, aina ya Scania mali ya kampuni ya Happy Africa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao na kulazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Tukio hilo lilitokea Januari 30, mwaka huu majira ya saa 9: 30 alasiri , eneo la Msamvu Mzambarauni darajani katika barabara kuu ya Morogoro- Dar es Salaam, ambapo basi hilo lilikuwa likotokea mkoani Njombe.
Majina ya watu hao wengine waliojeruhiwa na kulaza katika wodi za daraja la kwanza katika hospitali ya rufaa ya mkoa , ni dereva wa gari la Meya, Mwambala Ally (55) , na waandishi wa habari ambao ni wapigapicha vituo vya televisheni , Anitha Chali (30) pamoja na Hussein Nuha (28).
Mstahiki meya huyo aliyekuwa kwenye gari ya Halmashauri ya Manispaa hiyo yenye namba za usajili SM 4151, ikiendeshwa na Mwambala ambamo pia walikuwemo waandishi wa habari hayo na alikuwa katika msafara wa ziara ya kikazi ya mkuu wa mkoa huo,Dk Rajab Rutengwe.
Meya Nondo akizungumzia ajali hiyo, akiwa wodini akipatiwa matibabu ,sambamba na majeruhi wengine alisema baada ya kufika eneo la Mizambarauni, Darajani, lilichomoka pembeni basi la abiria ililokuwa likitokea Njombe kuelekea Dar es salaam, na kuligonga kwa mbele gari alilokuwemo.
Mashuhuda wa ajali hiyo waliwaambia waandishi wa habari wakiwa eneo la tukio, kuwa chanzo cha ajali hiyo ni basi la abiria mali ya kampuni ya Happy Africa, kuingilia msafara huo wa mkuu wa mkoa uliokuwa ukielea mjini baada ya kukagua shughuli za ujenzi wa vyumba vya maabara na kuzungumza na wananchi wa Kata ya Bigwa katika Shule ya Sekondari Sumaye.
Mkuu wa mkoa kwa takribani wiki mbili amekuwa katika ziara katik halmashauri saba za mkoa huo kwa ajili ya kukagua shughuli za ujenzi na umaliziaji wa maabara tatu kwa kila shule ya skondari ya Kata na pia kutumia fursa hiyo kujitambulisha , kusikiliza kero na kuzipatia majawabu ya msingi.
Januari 29 na 30 mwaka huu ilikuwa ni zamu ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Shule ya sekondari Sumaye kilikuwa ni kituo chake cha mwisho katika ziara hiyo na baadaye kufanyika kwa majumuisho ya ziara hiyo Januari 31, mwaka huu mjini Morogoro.
Hata hivyo baada ya kufikishwa hospitali ya rufaa ya mkoa , viongozi mbalimbali walifika kuwajulia hali wakati wakiendelea kupatia matubabu na madaktari mbingwa wa hospitali hiyo, akiwemo Mganga mkuu wa mkoa , Godfrey Mtei.
Mstahiki Meya Nondo ameumia sehemu ya kichani na mkononi , wakati na mpiga picha Anita Chali, ameumia kichwani, huku dereva pamoja na Hussein wakiumia zaidi kwenye paji la uso na kichwani huku Hussein akisaidiwa na mashine ya kupumulia (oxygen).
Kufuatia tukio hilo Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa mkoa imesema itatoa taarifa ya ajali hiyo jumamosi ya Januari 31, mwaka huu.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Rajab Rutengwe ( wa kwanza kushoto) akiwa na Mkuu wa wilaya ya Morogoro , Said Amanzi , wakipita eneo ambalo gari la namba SM 4151 Nissan iliyokuwa ikitumiwa na Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amir Nondo , ilipogongwa Januari 30, mwaka huu saa 9: 30 alasiri eneo la Mzambarauni Darajani -Msamvu barabara kuu ya Moro- Dar na Basi la Abiria aina ya Scania yenye namba za usajili T 831 CEH (Happy Africa ),iliyokuwa ikitokea mkoani Njombe kwenda Dar es Salaam .Meya huyo na watu wengine watatu walijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na kulazwa wakindelea kupatiwa matibabu.
Wasamalia wakimuwahisha Hospital,Mmoja wa majeruhi mara baada ya kupata ajali eneo la Mzambarauni Darajani -Msamvu barabara kuu ya Moro- Dar na Basi la Abiria aina ya Scania yenye namba za usajili T 831 CEH (Happy Africa ),iliyokuwa ikitokea mkoani Njombe kwenda Dar es Salaam .
Hili ndilo basi lililogongana na Gari ya Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amir Nondo.
Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amir Nondo ,(45) akiwa amelazwa wodi namba tano ya daraja la kwanza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro baada ya kujeruhiwa kufuatia gari yake SM 4151 ilipogongwa Januari 30, mwaka huu saa 9: 30 alasiri eneo la Mzambarauni Darajani , Msamvu Barabara kuu ya Moro- Dar na Basi la Abiria aina ya Scania yenye namba za usajili T 831 CEH (Happy Africa ),iliyokuwa ikitokea mkoani Njombe kwenda Dar es Salaam ,mbali na Meya huyo na watu wengine watatu ,Dereva Mwambala Ally (55), na waandishi wa habari , Anita Chali (30) pamoja na HUSSEIN Nuha (28) pia walijeruhiwa na kulazwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu. ( Picha na John Nditi).
Mwandishi wa habari,Anita Chali akiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro baada ya kujeruhiwa kufuatia gari waliyoipata,walipokuwa kwenye kazi na Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amir Nondo.
Habari na Masamablog