Saturday, 13 June 2015

Mkurugenzi wa Wizara ya Afya kortini kwa tuhuma za rushwa

Mkurugenzi wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Elias Chinamo akipelekwa rumande chini ya ulinzi wa polisi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana. Chinamo anatuhumiwa  kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa. Picha na Anthony Siame 
Na Tausi Ally na Samwel Eugen

Posted  Juni13  2015  saa 10:18 AM
Kwa ufupi
Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai alidai wakati akisoma mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Renatus Rutta, kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kati ya Juni 2011 na Februari 2013.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Elias Chinamo amefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu akikabiliwa na mashtaka 14 ya kuomba na kupokea rushwa.
Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai alidai wakati akisoma mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Renatus Rutta, kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kati ya Juni 2011 na Februari 2013.
Swai alidai kuwa katika kipindi hicho mshtakiwa aliomba na kupokea rushwa ya zaidi ya Sh14.44 milioni.
Mwendesha Mashtaka huyo alidai kuwa Chinamo alipokea rushwa ya Sh6.1 milioni kutoka kwa Suzana Nchala, fedha ambazo alidai alizipokea kupitia akaunti yake yenye namba 0152237197600 iliyopo tawi la benki ya CRDB la Holland.
Alidai kuwa alipokea fedha hizo kama faida ya kumpa nafasi ya kuandaa semina mbalimbali na mikutano ya wizara hiyo, kitu ambacho kipo kinyume na matakwa ya mwajiri wake.
Pia mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa Chinamo alipokea Sh2.06 milioni kutoka kwa Fadhili Kilemile, fedha ambazo zilipitishiwa kwenye akaunti hiyo kwa lengo la kumpa nafasi ya kuandaa semina mbalimbali na mikutano ya wizara hiyo kinyume na matakwa ya mwajiri wake.
Katika shtaka jingine, Chinamo anadaiwa kupokea Sh3.28 milioni kutoka kwa Emmanuela Safari, Sh700,000 kutoka kwa Joseph Bilango na Sh2.3 milioni kutoka kwa Anyitike Mwakitalima kupitia akaunti ya CRDB na 019201018063 ya NBC, tawi la Kichwele.
Chinamo aliyakana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wake umekamilika.
Hakimu Rutta alimuachia huru mshtakiwa huyo baada ya kukamilisha masharti ya kusaini dhamana ya Sh10 milioni pamoja na kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya dhamana ya maneno yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha. Kesi imeahirishwa hadi Julai Mosi, 2015 atakaposomewa maelezo ya awali.
              Habari na: http://www.mwananchi.co.tz

DR. SHEIN AWATAKA WAZAZI, SERIKALI NA WATOTO WENYEWE KUSHIRIKIANA KUKOMESHA MIMBA ZA UTOTONI

Baadhi ya watoto walioshiriki mbio za hisani za Nusu marathoni zilizoandaliwa katika shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika zinazotarajiwa kufikia kilele chake tarehe 16/6/2015 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar BaloziSeif Ali Iddi akisalimiana na baadhi ya watoto walioshiriki mbio za hisani za Nusu marathoni zilizoandaliwa katika shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika huko uwanja wa amani mjini Zanzibar.
Watoto wakionyeshana ubabe wakati wa mashindano yao yam bio za Nusu marathoni zilizoandaliwa katika shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika.

Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Zainab Omar Mohammed akijiandaa kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuzungumza katika shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein
Balozi Seif akisalimiana na Mwakilishi wa Baraza la Watoto kutoka Handeni Mkoani Tanga Mohammed Khalid kwenye hafla ya mbio za hisani za Nusu marathoni zilizoandaliwa katika shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika hapo uwanja wa amani.

Balozi Seif kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein akitoa zawadi kwa washiriki wa mbio za hisani za Nusu marathoni zilizoandaliwa katika shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika.

                                                                                            Picha na – OMPR, ZNZ.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alisema kwamba ili kupata mafanikio makubwa katika kukomesha Ndoa na Mimba za Utotoni ushirikiano wa lazima wa kupambana na kadhia hiyo unahitajika kati ya Wazazi,Serikali pamoja na watoto wenyewe.

Alisema elimu ya maadili inapaswa kutiliwa mkazo katika kuwapatia watoto na wzazi kwa lengo la kupiga vita tatizo hilo linaloonekana kuendelea kudhalilisha watoto na akina Mama na hatimae kuviza ustawi wao.

Dr. Shein alitoa kauli hiyo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye shamra shamra za maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika zilizoanza kwa Mbio za Hisani za nusu Marathoni.

Mbio hizo zilizochukuwa zaidi ya saa Moja zimeshirkisha Watoto pamoja na Wazazi na kufanyika katika uwanja wa Michezo wa Amani Mjini Zanzibar zikishuhudiwa na wanafunzi na watu mbali mbali.

Alisema Wazazi hawanabudi kuhakikisha kwamba wanazingatia maadili na misingi mizuri ya malezi ya watoto yanayoambatana na mazingira yatayowapa elimu na uelewa wa kutosha juu ya athari za mimba za utotoni.


Dr. Shein alifahamisha kwamba mimba za utotoni na ndoa za umri mdogo ni utamaduni unaoonekana kujengeka kwa baadhi ya Makabila na familia hapa Nchini jambo ambalo wazazi wanapaswa kulisimamia kidete katika kulipinga kwa nguvu zao zote.

Alisema vitendo vya unyanyasaji vinalitia aibu Taifa, ni kinyume na mafundisho ya dini zote zinazofuatwa hapa Nchini ambapi pia ni kinyume na haki za Binaadamu na haki za Kikatiba.

Rais wa Zanzibar alishukuru na kuzipongeza Taasisi na mashirika ya Kimataifa na yale ya Kitaifa yanayoendelea kujitolea kwenyea kuunga mkono juhudi za Serikali zote mbili katika kupinga udhalilishaji wa Watoto hasa lile la kuozeshwa wakiwa na umri mdogo.

Dr. Shein alifahamisha kwamba Serikali kupitia taasisi mbali mbali na vyombo vya sheria inaendelea kuhakikisha kuwa juhudi zinaochukuliwa sasa kuimarisha ustawi wa watoto zinaleta mafanikio.

“ Mafanikio ya pamoja ndio yatakayotuwezesha kutokomeza mimba za utotoni na ndoa za umri mdogo. Kila mmoja aweze kutekeleza wajibu wake na kutoa mashirikiano yanayohitajika katika kukomesha matendo hayo “. Alisema Dr. Shein.

Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania nay a Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa zikipanga na kutekeleza mipango tofauti kwa lengo la kulinda na kuimarisha maslahi na ustawi wa watoto hapa nchini.

Alisema Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa miongoni mwa Mataifa ya mwanzo yaliyoridhia Mkataba wa Haki za Mtoto uliopitishwa katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa Tarehe 20 Novembwa mwaka 1989 na kutia saini mwaka 1990.

Alieleza kwamba katika kuhakikisha watoto wanapata heshima, fursa na haki zao zilizobainishwa ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010- 2015 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianzisha Mahakama ya watoto nchini ili kuongeza kasi ya uendeshaji kesi na ufanisi wa kesi zinazohusiana na masuala ya watoto.

Dr. Shein alisema Mahkama hizo zimejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya watoto ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa watoto ambayo yatawasaidia kuweza kujieleza sambamba na kutoa ushahidi bila ya hofu.

Alisema Mahakama hizo zinaenda sambamba na utolewaji wa mafgunzo kupitia Mabaraza ya Wazazi katika shehia mbali mbali juu ya malezi bora ya watoto na namna ya kuripoti matukio ya udhalilishaji.

“ Nimefurahi kuona kwamba leo tumezindua mtandao wa simu za huduma ya kwanza kwa wahanga wa masuala ya udhalilishaji wa wanawake na watoto { Helpline 116 } ambao naamini wengi wetu tunaiponga matendo machafu tulikuwa tukiusubiri kwa hamu “. Alisema Dr. Shein.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekikti wa Baraza la Mapinduzi aliipongeza Taasisi hiyo isiyo ya kiserikali ya C-Sema yenye makao makuu yake Dar es salaam kwa juhudi zake ilizotoa katika kuunga mkono mapambano dhidi ya udhalilishaji wa watoto na wanawake hapa Nchni.

Balozi wa Shirika la Kimataifa la kutetea haki za Watoto { Save The Children } ambae ni Mwanariadha mashuhuri wa Tanzania aliyewika katika mbio za Kimataifa Suleiman Nyambui alionya kwamba jamii isisubiri kuonywa au kuelekezwa juu ya kupiga vita Ndoa na Mimba za utotoni.

Suleiman Nyambui aliendelea kukemea tabia ya baadhi ya Makabila Nchini wenye kuendeleza mila potovu za kuwakataza watoto na wanawake kutokula baadhi ya vyakula vyenye siha na kujenga afya ni kuwanyima kahi yao ya msingi.

Akitoa salamu za Shirika la Kimataifa la Kutetea haki za Watoto { Save The Children } Mkurugenzi wa Shirika hilo Nchini Tanzania Steve Thorne alisema kwamba juhudi zinapaswa kuchukuliwa na taasisi tofauti kwa kushirikiana na Serikali katika kusaidia kuondosha vifo vya watoto.

Bwana Steve aliipongeza Tanzania kwa hatua yake iliyochukuwa na kufikia hatua ya nne katika mapambano yake dhidi ya vifo vya watoto kwa mujibu wa mpango wa Kimataifa wa Milenia wa kupunguza vifo hasa Barani Afrika.

Akimkaribisha Mgeni rasmi katika shamra shamra hizo Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Zainab Omar Mohammed alisema Mtoto za Kizanzibari lazima akuwe salama na kuepushwa na vikwazo ili apate nafasi ya kulitumikia Taifa lake kwa ufanisini.

Mh. Zainab alisema katika kufanikisha hilo aliwaombna wazazi lazima watenge muda wao kwa kucheza na watoto wao ili kukabiliana na changamoto la mtoto kulelewa na mmzazi mmoja tu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

                              Habari na: http://rweyunga.blogspot.com

Lifti Muhimbili zazua kasheshe

Image result for lifti muhimbili

Na Pamela Chilongola
Kwa ufupi
Wauguzi watumia ngazi kupanda na kushuka na maiti, wagonjwa. Kaimu mkurugenzi akiri lifti kutofanyakazi
Dar es Salaam. Lifti za wodi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zimeharibika na kusababisha wauguzi kulazimika kuwabeba wagonjwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Pia, wauguzi hao wanalazimika kuzibeba maiti kutoka wodini na kuzipeleka kwenye chumba cha kuhifadhi kupitia ngazi za hospitali hiyo kutokana na tatizo hilo la lifti na kuwasababishia adha kubwa.
“Kuharibika kwa lifti hizi kwa zaidi ya mwezi sasa kunasababishia kufanya kazi katika mazingira magumu hasa ya utoaji huduma kwa wagonjwa na ubebaji wa maiti,” alisema jana mmoja wa wauguzi wa wodi ya Kibasila, Afred Ismail.
Alisema mgonjwa mahututi akipelekwa kwenye wodi hiyo anatakiwa kulazwa chumba namba 16 ambacho kipo gorofa ya tatu wanalazimika kumweka chumba cha upasuaji ambacho kipo chini na kusababisha kutotibiwa kwa wakati.
“Wauguzi tuna wakati mgumu wa kazi, utakuta mgonjwa anatakiwa alazwe kwenye chumba namba 16 kutokana na lifti kuwa mbovu, tunashindwa kumpandisha kwenye ngazi hadi hapo tutafute watu zaidi ya saba wa kumbeba ili akapatiwe matibabu,” alisema Ismail.
Muuguzi Edita Amandous alisema wanapata wakati mgumu hasa mgonjwa anapofariki kwani kumtoa ghorofa ya tatu na kumshusha chini ili kumpeleka kwenye chumba cha mahututi wanalazimika kumbeba watu zaidi ya 10 kushuka kwenye ngazi.
Kaimu Mkurugenzi wa MNH, Dk Hussein Kidanto alisema hospitali hiyo ilijengwa miaka mingi iliyopita hivyo wanampango wa kuboresha wodi ya Kibasila, Mwaisela na Sewahaji ila wanasubiria fedha zilizotengwa kwa ajili ya hospitali hiyo.
Dk Kidanto alisema, suala la lifti ni tatizo kubwa hasa kwenye wodi ya Kibasila na Sewahaji hivyo uongozi wa hospitali hiyo wamekuwa wakitengeneza kwa gharama kubwa kutokana na kuwa chakavu kila wakati zimekuwa zikiharibika.
“Hizi lifti kila wakati tunazitengeneza na tunatumia gharama kubwa sana lakini sasa hivi tumejipanga kununua mpya na tunampango wa kujenga wodi ya ghorofa 10 ambayo itaondoa hii changamoto,” alisema Dk Kidanto.
Alisema changamoto zinazojitokeza zinasababishwa na ufinyu wa bajeti, hivyo fedha inayotengewa hospitali hiyo ni ndogo na kusababisha kushindwa kuboresha majengo na kununua vifaa vya hospitali hiyo.
                                                                  Habari kutoka: Gazeti la Mwananchi