Mwanamke Mtanzania adakwa na kilo 74 za unga
Na Pamela Chilongola
Kwa ufupi
Mwanamke huyo, Chambo Fatuma Basil alikamatwa na
Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha India kilichopata taarifa za
kuwapo kwa mtu huyo ambaye alikutwa na hati ya kusafiria ya Tanzania.
Mwanamke huyo, Chambo Fatuma Basil alikamatwa na
Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha India kilichopata taarifa za
kuwapo kwa mtu huyo ambaye alikutwa na hati ya kusafiria ya Tanzania.
Kwa mujibu wa tovuti ya hindustantimes.com
limewanukuu maofisa wa Idara ya Uhamiaji wa India, Kitengo cha
Intelijensia cha Uwanja wa Ndege (AIU) wakisema Chambo alithibitishwa
Mtanzania baada ya kufanyia ukaguzi na kukibainisha kuwa kiwango
alichokutwa nacho ni kikubwa kulivyo mzigo wowote wa dawa za kulevya
uliowahi kukamatwa kwenye uwanja huo wa ndege.
Maofisa hao walisema walimnasa mwanamke huyo baada
ya kudokezwa na kufuatilia taarifa ya abiri huyo aliyekuwa akielekea
Dar es Salaam kupitia Doha, Qatar.
“Mtuhumiwa alikamatwa saa 7:00 mchana. Mbwa maalum
alielekezwa kukagua mizigo yake iliyokuwa inaingizwa chini ya ndege na
akatoa ishara chanya,” alisema Milind Lanjewar, kamishna wa ziada wa
ushuru wa Uwanja wa Ndege.
Mizigo yake mitatu ilikuwa imewekwa pakiti za unga
mweupe unaosadikiwa kuwa wa methaqualone au mandrax, dawa ambayo
hutumiwa kama mbadala wa cocaine, imeandika tovuti hiyo.
Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Madawa ya
Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema kwa kuwa mwanamke huyo amekamatwa
nchini India, Tanzania haiwezi kuingilia kwa undani ingawa wanasubiri
iwapo India watawapigia simu.
“Kila nchi ina sheria yake na ina uwezo wa kumchukulia hatua Fatuma kwa kuwa yupo ndani ya nchi hiyo,”alisema.
Nzowa alisema nchi nyingi duniani zipo kwenye vita
dhidi ya dawa za kulevya hivyo hashangai kwa Mtanzania huyo kukamatwa
nchini India.
Nzowa alisema dawa hizo ni kemikali au vibashirifu vinavyotumika kutengeneza dawa za kulevya na huzalishwa zaidi India.
Alisema ephedrine zinatumika kutengenezea dawa za
kikohozi lakini kinachojitokeza watu wanabadilisha matumizi yake na
kutengeneza dawa za kulevya.
Nzowa alisema aina hiyo ya vibashirifu inalimwa
kihalali nchini India kwa vibali maalumu kwa ajili ya kutengenezea dawa
ya kikohozi .