MANGULA ATAJA VIGEZO 13 VYA MGOMBEA URAIS WA CCM..NI HIVI HAPA
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Philip Mangula amesema vigezo 13, vitatumika kuwachuja
wanachama wa chama hicho ambao wameomba kugombea urais CCM.
Alisema hayo jana mjini hapa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya CCM mjini Dodoma.
Aliwakumbusha watangaza nia kuwa hawaruhusiwi kutoa rushwa, kushawishi au kushawishika kuwapa rushwa wale wanaowadhamini.
Vigezo vyenyewe
Alitaja vigezo 13 vitakavyotumika
kuwachuja wagombea kuwa ni uwezo mkubwa na uzoefu katika uongozi,
uadilifu, unyenyekevu na busara.
Pia, kuwa na elimu ya chuo kikuu au
inayolingana na hiyo, mtu mwenye upeo mkubwa wa kuimarisha na
kuendeleza Muungano, umoja na amani.
“Anatakiwa kuwa na upeo mkubwa
usiotiliwa mashaka kuhusu masuala ya kimataifa, asiye na hulka ya
kidikteta au mfashisti, awe tayari kulinda kanuni, sheria na utawala
bora,” alisema Mangula.
Alitaja vigezo vingine ni kuwa
mtetezi wa wanyonge na haki za binadamu na asiwe na tamaa ya kujipatia
umaarufu, kuzifahamu, kuzitetea, kutekeleza sera na Ilani ya CCM, mpenda
haki na ajue kupambana na dhuluma, asiwe mtu anayetumia nafasi ya
uongozi kujilimbikizia mali.
“Awe ni mtu makini anayezingatia masuala ya uongozi,” alisema.
Alisema katika kipindi hiki cha
mchakato wa uteuzi, kanuni zitakazotumika ni zile Kanuni za Uteuzi wa
Wagombea katika Vyombo vya Dola, zilizotolewa na Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC) ya CCM ya mwaka 2010.
Pia, katika kipindi hiki cha
mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola, ni sehemu
ya kazi za chama ndani ya chama. Alisema vikao vya uchujaji,
vitazingatia pia Kanuni za Uongozi na Maadili Toleo la mwaka 2012.
Alisema kipindi ambacho CCM
hudhihirisha dhana ya kazi ya msingi na muhimu katika kujenga uongozi
mmoja katika chama, kazi ya kutekeleza kwa dhati kanuni na demokrasia na
nidhamu ndani ya chama.
Alisema kanuni hiyo, ndiyo
inakiwezesha chama hicho kuwa cha demokrasia na papo hapo kuwa chombo
cha kuongoza mapinduzi kutokana na nidhamu yake inayokipa uongozi moja
katika vitendo.
Alisema miiko ya shughuli za
uchujaji na uteuzi wa wagombea, itazingatiwa. maadili na nidhamu ya
chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uteuzi wa wagombea wa
CCM katika vyombo vya dola, lazima vizingate na wale wote wanaohusika.
“Ni mwiko kwa kiongozi yeyote kwa
maneno au vitendo kumpendelea au kumsaidia kupata kura nyingi mwombaji
mmoja dhidi ya mwingine.”
Alisema Chama kinakataza mgombea
kutumia au kuhusisha ukabila, dini, rushwa, rangi, hila na eneo
analotoka katika shughuli yoyote ya uchaguzi.
Alisema ni mwiko kwa mgombea kufanya kampeni ya kupakana matope na ya aina nyingine yoyote ile dhidi ya mgombea mwingine.
Aidha, alisema ni mwiko kwa
kiongozi yeyote au mwombaji yeyote wa nafasi ya uongozi, aliyekabidhiwa
dhamana ya usimamizi, uangalizi, uchujaji na uteuzi, kufanya vitendo vya
ukiukaji wa kanuni ambazo ni Katiba ya CCM, sheria, ratiba na taratibu
za uteuzi.
Mangula alisema kwa mujibu wa
kanuni za uteuzi wa wagombea wa CCM katika vyombo vya dola, kutangaza
nia kunaruhusiwa kwa masharti, ikiwemo bila kuathiri haki ya mwanachama
ya kutangaza nia wakati wowote nia yake ya kutaka kugombea nafasi fulani
ya uongozi katika vyombo vya dola, lakini kwa kuwa nafasi hizo
zimewekwa muda maalumu wa miaka mitano.
Alisema wakati wa kutafuta
wadhamini 450, kila anachokifanya mwana CCM anayetafuta wadhamini,
kitaingia katika kumbukumbu za tathmini ya mgombea mtarajiwa.
Pia, alisema kamati za maadili za
wilaya, zikutane mara baada ya wagombea watarajiwa kujaza majina ya
wadhamini wilayani. Alisema mpaka sasa wagombea urais waliojiandikisha
wamefikia 22 na wengine bado wanakwenda.
HABARI NA MASAMA BLOG
No comments:
Post a Comment