Mimba za utotoni, nani wa kumfunga paka kengele?
Na Lilian Timbuka
Kwa ufupi
Hiyo ni changamoto inayolikabili taifa, huku baadhi
ya watu wakiliona kuwa ni jambo la kawaida na hulipuuza wakati wengine
wanalikemea.
Hiyo ni changamoto inayolikabili taifa, huku
baadhi ya watu wakiliona kuwa ni jambo la kawaida na hulipuuza wakati
wengine wanalikemea.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Haki za
Binadamu Duniani(Amnesty) iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam hivi
karibuni, Tanzania ni moja ya nchi zinaoongoza kwa matukio ya mimba za
utotoni.
Takwimu zinaonyesha kuwa, kwa siku, watoto 16 wanapachikwa mimba za utotoni.
Kwa mujibu wa wataalamu, hali hiyo imekuwa
ikiendelea kwa muda mrefu na kwa asilimia kubwa inazorotesha maendeleo
ya mtoto wa kike.
Ili kumwokoa mtoto wa kike kutoka janga hilo,
jitihada mbalimbali zimefanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali
kuhakikisha inawaokoa hasa wale ambao tayari wameshatumbukia katika
dimbwi hilo.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Chama
chaWaandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), unaonyesha kuwa katika kipindi
cha mwaka 2012/2013, matukio 228 ya mimba na matukio 42 ya ndoa za
utotoni yaliripotiwa.
Hata hivyo, mimba na ndoa za utotoni zimetajwa
kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyowapata watoto wa kike wa Tanzania,
tatizo ambalo bado ni kubwa katika baadhi ya maeneo ya Tanzania Bara na
Visiwani.
Mimba za utotoni na ukatili
Kwa kiasi kikubwa tatizo hilo linakwenda sanjari
na ukatili wa kijinsia ambapo kwa Tanzania Visiwani hali hiyo imeonekana
zaidi katika Mkoa wa Kusini Pemba na Wilaya ya Kati Unguja, huku upande
wa Tanzania Bara maeneo yenye ukatili dhidi ya wanawake pamoja na mimba
za utotoni yakitajwa kuwa ni Wilaya za Kahama, Tarime, Sengerema,
Newala, Mbulu, Bunda, Nkasi, Babati, Chunya, Dodoma, Bariadi, Busega na
Singida vijijini.
Bokhe Odhiambo (31), mkazi wa Tarime mkoani Mara,
anasema kuwa vitendo vya ukatilli dhidi ya wanawake ndani ya ndoa na
mimba za utotoni kwa watoto wa kike ni mambo ya kawaida na jamii
inaonekana kuwa haina muda wa kuyakemea.
“Kupigwa au kufanyiwa vitendo vya ukatili dhidi ya
wanawake ndani ya ndoa, migogoro ya ardhi na mimba za utotoni kwa
watoto wa kike ni mambo ya kawaida tu kwenye jamii yetu licha ya
wasaidizi wa kisheria kutoa elimu,” anssema Odhiambo.
Kutokana na changamoto hiyo, Chama cha Wanasheria Wanawake
Tanzania (Tawla) kimejitosa kutoa msaada wa kisheria katika mikoa yenye
changamoto lengo likiwa ni kupunguza tatizo hilo.
Mwenyekiti wa Tawla, Aisha Bade anasema kutokana
na ukubwa wa tatizo hilo chama chake kimeamua kusambaza wasaidizi wa
kisheria 400 nchi nzima lengo likiwa ni kusaidia kutatua migogoro ya
ardhi na mirathi.
Bade anasema Tawla imebaini kuwa mikoa ya Pwani na
Morogoro, Mtwara, Lindi, Arusha , Tanga, Shinyanga, Manyara na Mwaza
inaongoza kwa kuwa na migogoro ya mirathi, vitendo vya ukatili na
kuozesha watoto katika ndoa za utotoni.
Anasema kuwa mbali na mikoa hiyo pia mikoa ya
Tanga, Arusha, Dodoma inaongoza kwa kuwa na migogoro ya ardhi pamoja na
mirathi na hivyo juhudi mbalimbali zinahitajika kukabiliana na tatizo
hilo. “Tumesambaza wasaidizi wa kisheria 400 nchi nzima lengo ni kutatua
migogoro iliyopo hasa katika maeneo ya vijijini ambayo tumeona hayana
msaada wa kisheria” anasema Bade.
“Mbali na mikoa hiyo pia mikoa ya Tanga, Arusha,
Dodoma nayo ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kuwa na changamoto
kubwa ya migogoro ya ardhi na miradhi na kwamba juhudi za pamoja
zinahitajika kushirikia katika kutatua changamoto hiyo ili kupunguza
madhara yanayoweza kutokea kutokana na tatizo hilo”anasema Beda.
Tawla imefanya nini?
Anasema kuwa Tawla ilianza mafunzo ya wasaidizi wa
sheria mwaka 2006 na kutokana mafunzo hayo zaidi ya wananchi 4,600
wamenufaika kwa kupata msaada wa kisheria vijijini katika kipindi cha
mwaka jana pekee.
John Maziku, mkazi wa mkoani Shinyanga, anasema
kuwa utoro kwa wanafunzi a shule za sekondari na msingi ni tatizo
linaloukabili mkoa huo kwa sasa na sababu kubwa ni wazazi kutokuwa
karibu na watoto wao.
“Wazazi wengi wanakwenda migodini wanakaa huko kwa
muda mrefu na hwakumbuki kama wana familia, mama anabakia na mzigo
mkubwa wa kuitunza.
“Wazazi ndiyo chanzo kikubwa cha utoro katika
wilaya ya Bukombe kwa sababu baba anapokwenda kwenye machimbo ya migodi
hakumbuki kuwa wanaacha shule na kwenda kutafuta pesa,”anasema.
Mwajuma Mohamed (15), mkazi wa Ushirombo amekatiza
masomo yake akiwa darasa la sita baada ya kupewa mimba na dereva wa
magari makubwa. Hivi sasa ana mtoto wa miezi saba, lakini baba yake
hajawahi kupeleka huduma ya mtoto.
Mchango wa Tamwa
Mkurugenzi
Mtendaji wa Tamwa, Valerie Msoka anasema wamefanya kampeni ya kutoa
elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondai na msingi juu ya umuhimu wa
elimu na madhara ya mimba za utotoni ambayo bado chama hicho kinaendelea
nayo, lengo likiwa kuifikia mikoa yote nchini.
Anasema kwamba elimu hiyo imetolewa katika wilaya
kumi za mikoa ya kusini ambayo ni Lindi na Mtwara na kwamba mikoa ya
Pwani na Dar es Salaam imepata elimu hiyo kupitia mradi wa GEWE,
unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Denmark (Danida).
“Elimu inayotolewa kwa wanafunzi inalenga
kumwezesha mwanafunzi namna ya kujitambua na kujua malengo ya elimu
aipatayo itamsaidiaje katika maisha yake ,” anasema Msoka.
Anasema mafunzo hayo ni kitu cha muhimu na yatachangia maendeleo ya mwanafunzi hapo baadaye.
“Hata kama wazazi wanapomlazimisha kuolewa, binti
anatakiwa kukataa ili aweze kumaliza elimu yake vizuri,” anasema Msoka
na kuongeza: “Kazi hii ya kupambana na janga hili ni lazima pia lifanywe
na wanasiasa hasa katika kipindi hiki tunachoelekea katika Uchaguzi
Mkuu.” Anabainisha kuwa miongoni mwa wanasiasa imejengeka tabia ya
kutotilia maanani matatizo kama ya unyanyasaji wa kijinsia, hasa kipindi
kama hiki wakihofia kukosa kura.
“Ninawasihi wanasiasa, waache tabia ya kufumbia
macho matatizo yanayowakabili wapiga kura wao bali wayatafutie
ufumbuzi,” anasema Msoka.
Hata hivyo, swali linalobaki ni nani wa kulaumiwa
kwa mimba za utotoni; ni nani wa kuwafichua watuhumiwa na kukomesha ouvu
huo, nani wa kumfunga paka kengele?
Habari hii imepatikana katika gazeti la Mwanannchi.
Habari hii imepatikana katika gazeti la Mwanannchi.
No comments:
Post a Comment