Ajali nyingine yaua watu 23 Mufindi
Na Berdina Majinge
Kwa ufupi
Basi hilo, lifanyalo safari zake kati ya Iringa na
Njombe, lilipata ajali hiyo saa 1:45 usiku wa kuamkia jana wakati dereva
alipokuwa akijaribu kuyapita magari mengine kabla ya kugongana uso kwa
uso na lori.
Iringa. Watu 23 wamekufa papo
hapo na wengine 34 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Another G
kugongana na lori eneo la Kinyanambo A, Mafinga wilayani Mufindi, ikiwa
ni takriban miezi mitatu baada ya ajali nyingine iliyoua watu 50 katika
wilaya hiyo.
Basi hilo, lifanyalo safari zake kati ya Iringa na
Njombe, lilipata ajali hiyo saa 1:45 usiku wa kuamkia jana wakati
dereva alipokuwa akijaribu kuyapita magari mengine kabla ya kugongana
uso kwa uso na lori.
Kaimu kamanda wa polisi wa Mkoa wa Iringa,
Pudenciana Protas alisema basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Nicholaus
Mangula (29) na lori la Kampuni ya Bravo Logistics lililokuwa
likiendeshwa na Rogers Mdoe (39) na ambalo lililikuwa likitokea Zambia
kuelekea Dar es Salaam.
Katika ajali hiyo, dereva wa lori alifariki dunia papo hapo.
Machi 10 mwaka huu, watu 50 walipoteza maisha
kwenye ajali iliyotokea Mafinga, Changarawe, wakati kontena lililokuwa
limebwa na lori lilipochomoka wakati dereva akijaribu kukwepa mashimo
barabarani na kuangukia kwenye lori.
Alisema majeruhi wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya
Mufindi mjini Mafinga na maiti zimehifadhiwa hospitalini hapo ikiwamo ya
dereva wa lori aliyekufa papo hapo.
Alisema chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa
basi la Kampuni ya Another G ambaye alikuwa kwenye mwendo kasi na
alikuwa akiyapita magari mengine bila tahadhari ndipo alipofika katikati
alikutana na lori na kuamua kulichepusha nje ya barabara hali
iliyosababisha kupinduka na kisha lori kuligonga basi hilo ubavuni.
Alisema baada ya ajali hiyo, dereva wa basi alikimbia lakini polisi wamemkamata na yupo chini ya ulinzi.
Waliokufa na kutambuliwa mpaka sasa ni Lukas
Pascal, Brasto Samila, Dickson Luvanda, Albert Silla, Rogers Mdoe, Eva
Mbalinga, Hadija Mkoi, Clemence Mtati, Mohamed Kalika, Kastoli
Mwakyamba, Damian Myala na Sillo Nziku.
Waliojeruhiwa ni Majoline Lupembe (23) mkazi wa
Iringa, Veronica Simba (20, Tabora), Shadia Ally (24, Iringa), Mariam
Mbise (23, Mafinga), Anita Makwela (24, Kilolo), Benita Sagala (18,
Njombe), Bertha Mkoi (27), Rahel Mavika (18, Mufindi), Selina Fulgence
(23, Kigoma) na Maria Mwenda (17) mkazi wa Mafinga.
Majeruhi wengine ni Ndipako Mbilinyi (23, Njombe),
Alexander Mkakazii (28, Mafinga), Meshack Kibiki (44, Mafinga), Simon
Jumbe (22, Singida), Jerry Lutego (36, mkazi wa Mafinga), Enock Kanyika
(18, Mafinga), Deogratius Kayombo (21, Mafinga) na Yusuph Lulanda (22)
mkazi wa Njombe.
Wengine waliojeruhiwa ni Petro Mwalongo (21,
Njombe), Paulo Chane (21, Kilolo), Kenned Msemwa (28, Njombe), Mode
Shiraz (21, Singida), Emmanuel Antony (21, Mwanza), Godfrey Kanyika (39,
Mafinga) na Boniface Bosha (20).
Majeruhi wengine ni Ambiana Meshack (35, Njombe), Martha Kanyika
(30, Mafinga), Merina Tonga (miezi miwili), Yusuph Luhamba (34,
Mafinga) pamoja na wanaume wawili na wanawake wawili ambao
hawajatambulika kutokana na hali zao kuwa mbaya.
Petro Mwalongo, ambaye ni mmoja wa majeruhi
waliokuwa kwenye basi hilo, alisema dereva wa basi alikuwa akiendesha
kwa mwendo kasi bila kuwa na tahadhari yoyote na hata walimpomsihi
kupunguza mwendo hakuwasikiliza.
Mmoja wa shuhuda wa ajali hiyo ambaye ni mkazi wa
jirani na ilipotokea ajali, James John alisema ni muhimu kwa madereva
kuanza kufuata sheria za barabarani na kujali watu waliowabeba kwenye
mabasi ili kupunguza vifo na mali za abiria.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Goodluck Mlimbila alisema walipokea miili ya watu 23 na majeruhi 34.
Alisema watano kati yao waliokuwa na hali mbaya
zaidi wamehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa
ajili ya matibabu zaidi.
Dk Mlimbila alisema majeruhi saba walitibiwa na
kuruhusiwa huku wananchi wakiendelea kutambua miili ya maiti wengine na
kuzichukua.
Habari na Gazeti la Mwananchi
Habari na Gazeti la Mwananchi