Tuesday, 16 June 2015

Ajali nyingine yaua watu 23 Mufindi

Ajali nyingine yaua watu 23 Mufindi

 
Na Berdina Majinge
Kwa ufupi
Basi hilo, lifanyalo safari zake kati ya Iringa na Njombe, lilipata ajali hiyo saa 1:45 usiku wa kuamkia jana wakati dereva alipokuwa akijaribu kuyapita magari mengine kabla ya kugongana uso kwa uso na lori.
0Share 


Iringa. Watu 23 wamekufa papo hapo na wengine 34 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Another G kugongana na lori eneo la Kinyanambo A, Mafinga wilayani Mufindi, ikiwa ni takriban miezi mitatu baada ya ajali nyingine iliyoua watu 50 katika wilaya hiyo.
Basi hilo, lifanyalo safari zake kati ya Iringa na Njombe, lilipata ajali hiyo saa 1:45 usiku wa kuamkia jana wakati dereva alipokuwa akijaribu kuyapita magari mengine kabla ya kugongana uso kwa uso na lori.
Kaimu kamanda wa polisi wa Mkoa wa Iringa, Pudenciana Protas alisema basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Nicholaus Mangula (29) na lori la Kampuni ya Bravo Logistics lililokuwa likiendeshwa na Rogers Mdoe (39) na ambalo lililikuwa likitokea Zambia kuelekea Dar es Salaam.
Katika ajali hiyo, dereva wa lori alifariki dunia papo hapo.
Machi 10 mwaka huu, watu 50 walipoteza maisha kwenye ajali iliyotokea Mafinga, Changarawe, wakati kontena lililokuwa limebwa na lori lilipochomoka wakati dereva akijaribu kukwepa mashimo barabarani na kuangukia kwenye lori.
Alisema majeruhi wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi mjini Mafinga na maiti zimehifadhiwa hospitalini hapo ikiwamo ya dereva wa lori aliyekufa papo hapo.
Alisema chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa basi la Kampuni ya Another G ambaye alikuwa kwenye mwendo kasi na alikuwa akiyapita magari mengine bila tahadhari ndipo alipofika katikati alikutana na lori na kuamua kulichepusha nje ya barabara hali iliyosababisha kupinduka na kisha lori kuligonga basi hilo ubavuni.
Alisema baada ya ajali hiyo, dereva wa basi alikimbia lakini polisi wamemkamata na yupo chini ya ulinzi.
Waliokufa na kutambuliwa mpaka sasa ni Lukas Pascal, Brasto Samila, Dickson Luvanda, Albert Silla, Rogers Mdoe, Eva Mbalinga, Hadija Mkoi, Clemence Mtati, Mohamed Kalika, Kastoli Mwakyamba, Damian Myala na Sillo Nziku.
Waliojeruhiwa ni Majoline Lupembe (23) mkazi wa Iringa, Veronica Simba (20, Tabora), Shadia Ally (24, Iringa), Mariam Mbise (23, Mafinga), Anita Makwela (24, Kilolo), Benita Sagala (18, Njombe), Bertha Mkoi (27),  Rahel Mavika (18, Mufindi), Selina Fulgence (23, Kigoma) na  Maria Mwenda (17) mkazi wa Mafinga.
Majeruhi wengine ni Ndipako Mbilinyi (23, Njombe), Alexander Mkakazii (28, Mafinga), Meshack Kibiki (44, Mafinga), Simon Jumbe (22, Singida), Jerry Lutego (36, mkazi wa Mafinga), Enock Kanyika (18, Mafinga), Deogratius Kayombo (21, Mafinga) na Yusuph Lulanda (22) mkazi wa Njombe.
Wengine waliojeruhiwa ni Petro Mwalongo (21, Njombe), Paulo Chane (21, Kilolo), Kenned Msemwa (28, Njombe), Mode Shiraz (21, Singida), Emmanuel Antony (21, Mwanza), Godfrey Kanyika (39, Mafinga) na Boniface Bosha (20).
Majeruhi wengine ni Ambiana Meshack (35, Njombe), Martha Kanyika (30, Mafinga), Merina Tonga (miezi miwili), Yusuph Luhamba (34, Mafinga) pamoja na wanaume wawili na wanawake wawili ambao hawajatambulika kutokana na hali zao kuwa mbaya.
Petro Mwalongo, ambaye ni mmoja wa majeruhi waliokuwa kwenye basi hilo, alisema dereva wa basi alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi bila kuwa na tahadhari yoyote na hata walimpomsihi kupunguza mwendo hakuwasikiliza.
Mmoja wa shuhuda wa ajali hiyo ambaye ni mkazi wa jirani na ilipotokea ajali, James John alisema ni muhimu kwa madereva kuanza kufuata sheria za barabarani na kujali watu waliowabeba kwenye mabasi ili kupunguza vifo na mali za abiria.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Goodluck Mlimbila alisema walipokea miili ya watu 23 na majeruhi 34.
Alisema watano kati yao waliokuwa na hali mbaya zaidi wamehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa ajili ya matibabu zaidi.
Dk Mlimbila alisema majeruhi saba walitibiwa na kuruhusiwa huku wananchi wakiendelea kutambua miili ya maiti wengine na kuzichukua.
                                 Habari na Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment