Zigo la JK Kigoma kwa rais ajaye
Na Anthony Kayanda
Kwa ufupi
Kutokana na changamoto hizo, Rais Jakaya Kikwete
alipokuwa anaomba kura ili achaguliwe tena mwaka 2010 aliahidi
kutekeleza baadhi ya mambo na hilo lilichangia kumpa kura zaidi ya
10,000 kutoka Mkoa wa Kigoma na kumfanya aongoze kwa kuwazidi wagombea
wengine, hasa mpinzani wake mkuu Dk Willibrod Slaa wa Chadema.
Kigoma. Mkoa wa Kigoma upo
Magharibi ya Tanzania ikiwa ni mojawapo ya mikoa iliyobatizwa jina la
‘pembezoni’ kutokana na umaskini unaowakabili wakazi wake walio wengi,
lakini pia kwa miaka mingi umekuwa na changamoto ya miundombinu mibovu
ya barabara, usalama wa raia kutokana na ujambazi.
Kutokana na changamoto hizo, Rais Jakaya Kikwete
alipokuwa anaomba kura ili achaguliwe tena mwaka 2010 aliahidi
kutekeleza baadhi ya mambo na hilo lilichangia kumpa kura zaidi ya
10,000 kutoka Mkoa wa Kigoma na kumfanya aongoze kwa kuwazidi wagombea
wengine, hasa mpinzani wake mkuu Dk Willibrod Slaa wa Chadema.
Alitoa ahadi nyingi tu kama vile ujenzi wa
barabara, ujenzi wa kiwanja cha ndege, ujenzi wa daraja la mto
Malagarasi, ujenzi wa reli mpya ya kati, kuimarisha ulinzi na usalama
Ziwa Tanganyika, kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha biashara katika ukanda
wa Maziwa Makuu na kuhakikisha kuwa Kigoma inaunganishwa na umeme wa
gridi ya Taifa.
Barabara
CCM iliahidi kujenga barabara ya Kigoma hadi
Nyakanazi yenye urefu wa kilomita 330 kwa kiwango cha lami. Barabara
hiyo imekuwa haitengenezwi kwa madai ya ukosefu wa fedha, jambo ambalo
limesababisha adha kubwa kwa wasafiri hususani kipindi cha mvua nyingi
ambapo magari makubwa hukwama na kuziiba.
Hata hivyo, ujenzi wa barabara hiyo umeanza na kwa
upande wa Kigoma kuna mkandarasi kutoka China anayejulikana kwa jina la
CR 15 Group chini ya Mkandarasi Mshauri, DOCH Limited ya Dar es Salaam
ambapo inadaiwa amepewa kipande cha kilomita 50 ajenge kwa kiwango cha
lami.
Wameanza kuchimba barabara kuanzia kijiji cha
Kasangezi hadi Muzye, umbali wa kama kilomita tano hivi ikiashiria
kwamba ndiyo ujenzi unaanza rasmi, lakini kasi ndogo ya ujenzi inatia
shaka kama kweli serikali ina nia ya dhati kukamilisha ujenzi huo au
inatumika kama kampeni ili kupata kura kwa mgombea atakayepitishwa na
CCM.
Kwa upande wa Barabara ya Kigoma hadi Manyoni
mkoani Singida yenye urefu wa zaidi ya kilomita 600 imeanza kujengwa kwa
kiwango cha lami. Utekelezaji wake umekamilika kwa zaidi ya asilimia
50.
Licha ya kwamba ujenzi wake haujakamilika kwa
maana ya kwamba unaweza kutokaa Kigoma hadi Manyoni kwa lami, lakini
maeneo makubwa yamewekwa tabaka la lami, jambo lililofanya baadhi ya
mabasi yaanze kutumia barabara hiyo kuanzia Kigoma kwenda Dar es Salaam
na kabla ya hapo walikuwa wanatumia barabara ya Kigoma kupitia
Nyakanazi, Kahama, Singida na hatimaye kutokea Manyoni.
Kiwanja cha ndege Kigoma
Rais aliahidi kujenga kiwanja kitakachowezesha
ndege aina ya Boeing kutua Kigoma ili kurahisisha usafiri kati ya nchi
za Burundi, Kongo DRC na Rwanda.
Ilitarajiwa kiwanja hicho kiwe na njia ya kurukia
ndege yenye urefu wa mita 3,000 (sawa na kilomita 3) lakini ujenzi wake
umekamilika kwa kujengwa mita 1720 kwa kiwango cha lami, urefu ambao
hauwezi kutumiwa na ndege aina ya Boeing zilizolengwa kutua hapo kwa
ajili ya kubeba bidhaa kupeleka Ulaya na pia kutoa Ulaya kuzileta hapa
ikiwa ni pamoja na zile zinazopaswa kwenda Mashariki ya Kongo ambao
zaidi wanategemea bidhaa kutoka Kigoma.
Kiwanja hicho kimeingia kwenye mgogoro na baadhi ya wakazi wa
kata za Majengo na Machinjioni waliotakiwa kuhama ili kupisha ujenzi
huo, lakini wakakataa kuhama wakidai kuwa fidia waliyolipwa ni ndogo
ikilinganishwa na gharama halisi za maisha ya sasa.
Uthamini wa mali zao ulifanywa mwaka 2006 lakini
wamekuja kulipwa fedha mwaka 2013, miaka saba baadaye tena kwa thamani
ya mwaka huo wa 2006, wakati utaratibu upo wazi kwamba ikipita miezi
sita kabla mtu hajalipwa fedha baada ya kufanyiwa uthamini wa mali,
inatakiwa zoezi la uthamini lirudiwe upya ili mtu alipwe fedha kulingana
na wakati uliopo, lakini hilo halikufanyika.
Hiyo imekuwa changamoto kubwa na ahadi ya Rais
Kikwete inaonekana kukwama na hakuna dalili za wazi kuonyesha kwamba
mradi huo utatekelezwa kabla ya Novemba, 2015 atakapokabidhi madaraka
kwa rais ajaye.
Umeme wa Gridi ya Taifa
Mkoa wa Kigoma haujafanikiwa kuunganishwa kupata
umeme wa gridi ya Taifa na badala yake wakazi wake wanatumia umeme
unaozalishwa kwenye jenereta za kufua umeme na serikali ilikwama
kutekeleza ahadi yake ya kuiunganisha Kigoma na umeme ulioishia Kaliua
mkoani Tabora au Kahama mkoani Shinyanga.
Kitovu cha biashara
Rais Kikwete aliahidi kwamba atahakikisha mji wa
Kigoma unakuwa kama Dubai kwa maana kwamba unageuzwa kuwa kitovu cha
biashara katika ukanda wote huu wa nchi za Maziwa Makuu ambazo badala ya
kwenda kufuata bidhaa Dubai na China, wangelazimika kuja Kigoma kununua
bidhaa hizo.
Hadi sasa hakuna jitihada zozote za makusudi
zinazoonekana kutekeleza ahadi hiyo na badala yake mji unazidi kuchoka
na maisha ya wakazi wengi wa Kigoma yanazidi kuwa magumu.
habari kutoka gazeti la mwananchi:
habari kutoka gazeti la mwananchi:
No comments:
Post a Comment