Wednesday, 24 June 2015

Moto waunguza Msikiti wa Omary Bin Hatwah uliopo karibu na jengo la Yanga

      Baada ya Msikiti kuwa umeungua na huyu raia mwema akiwa anaangalia na kujaribu kukagua vizuri vitu vilivyoungua.

Msikiti uliopo jijini Dar es Salaam eneo la kariakoo mtaa wa jangwani na twiga  umeungua moto leo mnamo majira ya saa kumi na moja kasoro.

Chanzo cha moto huo hakikufahamika mara moja ingawa watu wengi waliuwa wanahisi kwamba pengine utakuwa umesababishwa na umeme.

Moto huo umeleta madhala makubwa ikiwa pamoja na kuunguza matanki ya maji, vitabu vya dini, makapeti, mabati, feni, na mtu mmoja alionekana kupata majeraha ya moto mguuni, vioo vya madilisha vilivunjwa ili kuokoa baadhi ya vifaa vya msikitini. 

Watu wa zima moto walichelewa kufika ingawa ofisi zao zipo karibu na eneo la tukio walitumia kama dakika 45.

Watu waliokuwepo eneo la tukio waliokuwa wanasaidia kuzima moto walitoa lawama zao kwa zima moto kwa kuchelewa kufika na kwa raia ambao sio wema waliokuwa wakijaribu kuiba badala ya kuokoa.

Habari hii imeletwa kwenu na Hatasisitupo.blogspot.com

Moto waunguza Msikiti uliopo karibu na jengo la Yanga




           
         Moto waunguza Msikiti uliopo karibu na jengo la Yanga
Moto huo ulianza majira ya saa kumi na moja kasoro na umeunguza sehemu kubwa ya msikiti bila ya kujulikana chanzo chake eneo kubwa lililoungua ni sehemu iliyokuwa ikitumiwa na wanafunzi wa dini ya kiislamu jambo la kushukuru leo hawakuwepo wakati moto huo ukitokea. kwa habari zaidi endelea kufuatilia blog yetu.

Zigo la JK Kigoma kwa rais ajaye

           Zigo la JK Kigoma kwa rais ajaye


Mji wa Kigoma unavyoonekana ,miongoni mwa ahadi zilizotolewa na JK 2010 ni kuigeuza Kigoma kuwa sasa Dubai .Picha ya Maktaba. 
Na Anthony Kayanda
Kwa ufupi
Kutokana na changamoto hizo, Rais Jakaya Kikwete alipokuwa anaomba kura ili achaguliwe tena mwaka 2010 aliahidi kutekeleza baadhi ya mambo na hilo lilichangia kumpa kura zaidi ya 10,000 kutoka Mkoa wa Kigoma na kumfanya aongoze kwa kuwazidi wagombea wengine, hasa mpinzani wake mkuu Dk Willibrod Slaa wa Chadema.



Kigoma. Mkoa wa Kigoma upo Magharibi ya Tanzania ikiwa ni mojawapo ya mikoa iliyobatizwa jina la ‘pembezoni’ kutokana na umaskini unaowakabili wakazi wake walio wengi, lakini pia kwa miaka mingi umekuwa na changamoto ya miundombinu mibovu ya barabara, usalama wa raia kutokana na ujambazi.
Kutokana na changamoto hizo, Rais Jakaya Kikwete alipokuwa anaomba kura ili achaguliwe tena mwaka 2010 aliahidi kutekeleza baadhi ya mambo na hilo lilichangia kumpa kura zaidi ya 10,000 kutoka Mkoa wa Kigoma na kumfanya aongoze kwa kuwazidi wagombea wengine, hasa mpinzani wake mkuu Dk Willibrod Slaa wa Chadema.
Alitoa ahadi nyingi tu kama vile ujenzi wa barabara, ujenzi wa kiwanja cha ndege, ujenzi wa daraja la mto Malagarasi, ujenzi wa reli mpya ya kati, kuimarisha ulinzi na usalama Ziwa Tanganyika, kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Maziwa Makuu na kuhakikisha kuwa Kigoma inaunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa.
Barabara
CCM iliahidi kujenga barabara ya Kigoma hadi Nyakanazi yenye urefu wa kilomita 330 kwa kiwango cha lami. Barabara hiyo imekuwa haitengenezwi kwa madai ya ukosefu wa fedha, jambo ambalo limesababisha adha kubwa kwa wasafiri hususani kipindi cha mvua nyingi ambapo magari makubwa hukwama na kuziiba.
Hata hivyo, ujenzi wa barabara hiyo umeanza na kwa upande wa Kigoma kuna mkandarasi kutoka China anayejulikana kwa jina la CR 15 Group chini ya Mkandarasi Mshauri, DOCH Limited ya Dar es Salaam ambapo inadaiwa amepewa kipande cha kilomita 50 ajenge kwa kiwango cha lami.
Wameanza kuchimba barabara kuanzia kijiji cha Kasangezi hadi Muzye, umbali wa kama kilomita tano hivi ikiashiria kwamba ndiyo ujenzi unaanza rasmi, lakini kasi ndogo ya ujenzi inatia shaka kama kweli serikali ina nia ya dhati kukamilisha ujenzi huo au inatumika kama kampeni ili kupata kura kwa mgombea atakayepitishwa na CCM.
Kwa upande wa Barabara ya Kigoma hadi Manyoni mkoani Singida yenye urefu wa zaidi ya kilomita 600 imeanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Utekelezaji wake umekamilika kwa zaidi ya asilimia 50.
Licha ya kwamba ujenzi wake haujakamilika kwa maana ya kwamba unaweza kutokaa Kigoma hadi Manyoni kwa lami, lakini maeneo makubwa yamewekwa tabaka la lami, jambo lililofanya baadhi ya mabasi yaanze kutumia barabara hiyo kuanzia Kigoma kwenda Dar es Salaam na kabla ya hapo walikuwa wanatumia barabara ya Kigoma kupitia Nyakanazi, Kahama, Singida na hatimaye kutokea Manyoni.
Kiwanja cha ndege Kigoma
Rais aliahidi kujenga kiwanja kitakachowezesha ndege aina ya Boeing kutua Kigoma ili kurahisisha usafiri kati ya nchi za Burundi, Kongo DRC na Rwanda.
Ilitarajiwa kiwanja hicho kiwe na njia ya kurukia ndege yenye urefu wa mita 3,000 (sawa na kilomita 3) lakini ujenzi wake umekamilika kwa kujengwa mita 1720 kwa kiwango cha lami, urefu ambao hauwezi kutumiwa na ndege aina ya Boeing zilizolengwa kutua hapo kwa ajili ya kubeba bidhaa kupeleka Ulaya na pia kutoa Ulaya kuzileta hapa ikiwa ni pamoja na zile zinazopaswa kwenda Mashariki ya Kongo ambao zaidi wanategemea bidhaa kutoka Kigoma.
Kiwanja hicho kimeingia kwenye mgogoro na baadhi ya wakazi wa kata za Majengo na Machinjioni waliotakiwa kuhama ili kupisha ujenzi huo, lakini wakakataa kuhama wakidai kuwa fidia waliyolipwa ni ndogo ikilinganishwa na gharama halisi za maisha ya sasa.
Uthamini wa mali zao ulifanywa mwaka 2006 lakini wamekuja kulipwa fedha mwaka 2013, miaka saba baadaye tena kwa thamani ya mwaka huo wa 2006, wakati utaratibu upo wazi kwamba ikipita miezi sita kabla mtu hajalipwa fedha baada ya kufanyiwa uthamini wa mali, inatakiwa zoezi la uthamini lirudiwe upya ili mtu alipwe fedha kulingana na wakati uliopo, lakini hilo halikufanyika.
Hiyo imekuwa changamoto kubwa na ahadi ya Rais Kikwete inaonekana kukwama na hakuna dalili za wazi kuonyesha kwamba mradi huo utatekelezwa kabla ya Novemba, 2015 atakapokabidhi madaraka kwa rais ajaye.
Umeme wa Gridi ya Taifa
Mkoa wa Kigoma haujafanikiwa kuunganishwa kupata umeme wa gridi ya Taifa na badala yake wakazi wake wanatumia umeme unaozalishwa kwenye jenereta za kufua umeme na serikali ilikwama kutekeleza ahadi yake ya kuiunganisha Kigoma na umeme ulioishia Kaliua mkoani Tabora au Kahama mkoani Shinyanga.
Kitovu cha biashara
Rais Kikwete aliahidi kwamba atahakikisha mji wa Kigoma unakuwa kama Dubai kwa maana kwamba unageuzwa kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wote huu wa nchi za Maziwa Makuu ambazo badala ya kwenda kufuata bidhaa Dubai na China, wangelazimika kuja Kigoma kununua bidhaa hizo.
Hadi sasa hakuna jitihada zozote za makusudi zinazoonekana kutekeleza ahadi hiyo na badala yake mji unazidi kuchoka na maisha ya wakazi wengi wa Kigoma yanazidi kuwa magumu.
                                                             habari kutoka gazeti la mwananchi:

Tuesday, 23 June 2015

Fanya haya upate mafanikio maishani

Fanya haya upate mafanikio maishani


 
Na Emanuel Gingi
Kwa ufupi
Hata hivyo, unajua siri ya kufanikiwa maishani? Makala haya yanajaribu kutaja baadhi ya njia za unazoweza kupita ili ufike katika safari yako.

Wengi tunapenda mafanikio maishani. Ukiwa mfanyabiashara, mwajiriwa, kiongozi, mama wa nyumbani au mwanafunzi, lazima uwe na ndoto ya kufanikiwa kama sehemu ya kutimiza ndoto yako.
Hata hivyo, unajua siri ya kufanikiwa maishani? Makala haya yanajaribu kutaja baadhi ya njia za unazoweza kupita ili ufike katika safari yako.
Kuwa na mawazo chanya: Akili yako ni kifaa cha ajabu, chaweza kuamua kufanikiwa au kutofanikiwa. Fanya unachoamua kufanya usifanye unachoambiwa ufanye pasipo kukipenda. Inategemea na mawazo uliyoyajaza ndani ya akili yako, kwa hiyo kwa nini usijaze mawazo yako au akili yako na hisia chanya za kufanikiwa?
Zungumza kuhusu mafanikio: Wachunguzi wanasema takribani asilimia 75 ya mawazo ya ndani ya mtu ni hasi, yatupasa kuyabadili mawazo au maneno na kuwa chanya muda wote. Kwa mfano, badala ya kusema tatizo sema fursa, badala ya kusema hakuna kitu ninachoweza kufanya, sema naangalia hatua nyingine.
Jipe mazoezi ya kufanikiwa: Inakupasa kujipa mazoezi ya kujihamasisha hata kama muda mwingine huwezi kujisikia vyema; lazima utoke na kujihamasisha katika hatua chanya.
Jitose: Lazima uishi maisha ya utulivu au kuridhika, jiepushe na mawazo ya kufeli.
Wasome waliofanikiwa: Ukitaka kufanikiwa lazima utafute maisha au uige maisha ya watu waliofanikiwa. Kati ya vitabu au nyaraka nzuri za kukujenga ni pamoja na kutafuta machapisho yanayozungumzia watu kama kina Mwalimu Julius Nyerere, Benjamin Franklin, Abraham Lincoln, Mahatma Ghandhi na wengineo.
Hivi ni vitabu vitakavyokuongezea mbinu au ujuzi wa kushinda changamoto na kuongeza thamani ya kubadilisha maisha yako yakawa mazuri.
Panda mbegu ya mafanikio: Inakupasa wewe mwenyewe kupanda mawazo ya mafanikio kwa kufanya yafuatayo: Nenda sehemu yeyote tulivu labda nyumbani au sehemu yeyote na uzime radio na televisheni. Tafuta kiti kikufaacho na utulize mawazo, anza kufikiria lengo moja ulikamilishe.
Chukua maono ya kukuwezesha au kukamilisha maono yako yafanikiwe. Ukianza kuwa na maono utaanza kujihisi vizuri, utasema vizuri, utaona vizuri. Ni wewe mwenyewe tu. Angalizo ni kuwa kama hujaweka muda maalumu, ni vigumu kukamilisha jambo litokee
Fikiria mafanikio: Lazima uone picha kubwa kwa kila kitu unachokifanya usipoteze muda kwa vitu ambavyo si muhimu katika maisha. Vaa utofauti chanya kwenye familia, jumuiya, kampuni au taasisi. Fikiria makubwa leo kesho utapata mazuri, ukweli ni kwamba ukifikiria makubwa lazima upate makubwa, ukifikiria madogo utapata madogo.
Jiwekee malengo: Vitu ambavyo vinaangusha watu katika maisha ni kukosa malengo madhubuti. Weka malengo katika uchumi, familia, afya, roho na pia taaluma .
Hatua za kuchukua ni hizi: hakikisha lengo au malengo yamepangika, yanafikiwa, yanaeleweka, na yana muda maalumu wa kuyafikia.
Jali mwonekano wako: Watu wenye kupenda mafanikio kwanza wako makini kimwonekano. Ukweli ni kwamba ukiwa upo vizuri kimwonekano utajisikia vizuri. Vaa mavazi na sura ya mafanikio. Kuwa na akili ya mafanikio, wenye hamasa ndiyo wanaokwenda mbele kwa kujiamini.
Wasaidie wengine: Endeleza nia yako kwa kuwasaidia wengine, shirikisha kipawa chako na wengine bila kutarajiwa kulipwa. Faida kubwa ambayo utaipata ni kujenga ujasiri mkubwa pia uzoefu ambao utakufanya uwe tofauti. Daima watu wenye mafanikio, wanapenda hamasa chanya na zenye maana huku wakiwasaidia wengine.
                                         Habari kutoka Gazeti la Mwananchi.