Tuesday, 30 June 2015

CHADEMA WATIFUANA LUDEWA MZIMU WA UKABILA WAWATAFUNA

 

Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe kimeingia katika mgogoro mkubwa kutokana na wanachama wa chama hicho kushangazwa na kitendo cha uongozi wa chama hicho kutoka kanda ofisi za mkoa wa Mbeya kufanya uchaguzi wa viongozi wa wilaya kwa kushitukiza.

Wakiongea kwa nyakazi tofauti baadhi ya wananchama wa chama hicho hapa wilayani kwa masharti ya kutotajwa majina yao kwa kuhofia kuvuliwa uanachama walisema kuwa licha ya kuwa uongozi wa awali ulikuwa na mapungufu ya kuwa na migogoro ya mara kwa mara hasa katika kuendekeza ukabila lakini ulikuwa na watu wenye uwezo wa kufanya maamuzi kutokana na elimu waliokuwa nayo.

Walisema kuwa kitendo cha viongozi wa kanda kuitisha mkutano mkuu wa dharula na kufanya uchaguzi wa viongozi wengine kimewashitua wanachama hao ambao walikuwa na imani kubwa na viongozi wao wa awali hivyo kuwaletea viongozi wengine ni sawa na kukivuruga chama na kusababisha kushindwa vibaya katika uchaguzi mkuu ujao.

Aliyekuwa katibu mwenezi wa chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Ludewa Bw.Kathbet Haule apotakiwa kutolea maelezo kuhusiana na mgogoro huo unaokitafuna chama alisema kuwa viongozi wa wilaya akiwemo yeye kama katibu mwenezi hawajavuliwa madaraka  na nib ado wao ni viongozi wa wilaya licha ya kuwa waliochaguliwa kupitia uongozi wa kanda wanajinadi kuwa wao ndio viongozi.

“sisi ni viongozi wa chadema wilaya ya Ludewa nabado tunatambulika waliochaguliwa ni tume tu kama taxforce itakayofanya kazi katika kipindi hiki cha uchaguzi lakini sisi tutabaki kuwa viongozi wa wilaya na kama wanawatangazia watu kuwa sisi tumepigwa chini huo ni uongo kwani kazi ya ofisi ya kanda si kuchagua viongozi wa wilaya”,alisema Bw.Haule.

Kuhusiana na mgogoro mkubwa unaokitafuna chama hicho wilayani hapa Bw.Haule alisema kuwa ni kweli baadhi ya viongozi ndani ya chama wamekuwa wakishindwa kuelewana kutokana na baadhi ya mambo mfano ni katibu na mwenyekiti ndio walikuwa na mgogoro ambao ungeweza kumalizika kabla ya kufanya uchaguzi uliofanyika. 

Bw.Haule alisema kuwa suala la ukabila ndani ya chama hicho wilayani Ludewa limekuwa likuzungumzwa mara kwa mara licha ya kuwa hakuna malalamiko kwa maandishi yaliyowahi wasilishwa katika ofisi yake na katibu ila kumekuwa na minong’ono kwa baadhi ya wanachama kulalamikia jambo hilo hivyo hakuna uhakika kama jambo hilo ni chanzo cha migogoro ndani ya chama.
                          Habari na: http://habariludewa.blogspot.com

No comments:

Post a Comment