Wednesday, 17 June 2015

BALOZI SEIF AWATAKA WAZAZI KUWAPOKEA WATOTO WAO WALIOACHANA NA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA

Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana na mmoja kati ya Vijana sita walioamua kuachana na matumizi ya Dawa za Kulevya katika Kijiji cha Fujano hapo katika Viunga vya vya Skuli ya Fujoni. Kati kati yao ni Mwakilishi wa Umoja wa kusaidia mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya na Pombe Tanzania Bwana Abdulrahman Mohammed Abdulla.
Mwakilishi wa Umoja wa kusaidia mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya na Pombe Tanzania Bwana Abdulrahman Mohammed Abdulla akielezea mikakati ya taasisi yake katika mapambano dhidi ya Dawa za kulevya hapa Nchini.
Balozi Seif akizungumza na baadhi ya Wananchi mara ya kukabidhiwa Vijana Sita walioamua kuachana na matumizi ya Dawa za kulevya waliokuwa wakipata mafunzo kwenye Kituo cha Mombasa nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Kushoto ya Balozi Seif ni Sheha wa Shehia ya Fujoni Bwana Said Mgeni Bakari na wa kwanza kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaskazini “ B “ Nd. Hilika Khamis na Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi.
Kijana Ayoub Hussein Ayoub Mmoja kati ya Vijana sita walioamua mkuachana na matumizi ya Dawa za kulevya akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake kuushukuru uongozi wa Jimbo la Kitope kwa kusaidia mbinu na uwezeshaji uliowachangia wao kuacha dawa hizo.
Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi shilingi Milioni 5,000,000/- Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Dr. Mustafa Gharu aliyevaa T. Shirt ya Buluu hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa kibanda cha maji katika kijiji cha Kinduni.

                                                                                                    Picha na – OPMR – ZNZ.

Wazazi wameaswa kuwa tayari kuwapokea Vijana au watoto wao walioamua kuacha matumizi ya dawa za kulevya ili kuwalinda na vishawishi vinavyoweza kutoa nafasi ya kuwarejesha tena kwenye matumizi ya Dawa hizo pamoja pombe haramu.

Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi ametoa wosia huo wakati wa kuwapokea Vijana Sita wa Kijiji cha Fujoni walioamua kuacha kutumia Dawa za kulevya na kupata mafunzo watakayoyatumia kuwasomesha wenzao kuachana na Dawa hizo hapo katika Skuli ya Fujoni Wilaya ya Kaskazini “ B “.

Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema wapo Wazazi na Familia Nchini ambao bado wanaendelea na tabia ya kuwatenga Vijana wao walioathirika na Dawa za kulevya kwa kuchelea kufanyiwa matendo ya maudhi kama wizi.

Alisema tabia hiyo inafaa kuachwa kwa vile kama haikutafutiwa ufumbuzi inaweza kuzalisha zaidi Vijana wanaotumbukia katika matumizi ya Dawa za kulevya na hatimae kuwa na kundi kubwa la walevi ndani ya Jamii ambao ni nguvu kazi ya Taifa.

Balozi Seif alionyesha furaha yake kutokana na ujasiri mkubwa ulioonyeshwa na vijana hao wa kuamuwa kuacha matumizi ya Dawa za kulevya na kujitolea kuwa mfano kwa wenzao wenye tabia hiyo.

Aliwaomba Vijana hao kuwa na hadhari ya kutokubali kudanganywa na baadhi ya watu hasa wanasiasa ya kushawishiwa kujiingiza matika matendo maovu kama uvunjifu wa Amani.

Balozi Seif alisema katika kipindi hichi cha Taifa kukaribia katika uchaguzi Mkuu Vijana wana wajibu wa kupima kwanza chochote wanachoambiwa kabla ya kufikia uamuzi wa kuchukuwa hatua.

Katika kukabiliana na changamoto hizo Balozi Seif alifahamisha kwamba akili za kuambiwa lazima vijana hao pamoja na Wananchi wote wanapaswa kuzichanganya na zao ili kupata maamuzi muwafaka.

Akiunga mkono maamuzi ya Vijana pamoja na wazee wa Kijiji cha Fujoni katika juhudi za kukaa pamoja na kutafuta mbinu za kukabiliana na matatizo ya matumizi ya Dawa za kulevywa Kijijini hapo Balozi Seif aliahidi kuwapatia Boti ya Uvuvi na vifaa vyake ili iwasaidie katika shughuli zao za kujiongezea ajira.

Balozi Seif alieleza kwamba Mapato ya Boti hiyo pia wanaweza kuanzia jengo la Ofisi yao kwa hatua ya ujenzi wa msingi na yeye atakuwa tayari kuongeza nguvu katika kuwapatia vifaa ikiwemo matofali kwa ajili ya kuendeleza jengo lao.

Akitoa Taarifa fupi Mwakilishi wa Umoja wa kusaidia mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya na Pombe Tanzania Bwana Abdulrahman Mohammed Abdulla alisema Taasisi yao iliyoasisiwa mwaka 2009 tayari imeshafungua vituo Vinne vya kutoa mafunzo kwa vijana walioamua kucha dawa za kulevya Bara na Zanzibar.

Bw. Abdulrahman alisema vijana kati ya 56 na 65 wameshapatiwa mafunzo kwenye vituo hivyo ambapo zaidi ya asilimia 35% ya Vijana waliopita kwenye vituo hivyo wamerejea katika hali za kawaida na kufanya matumizi ya udungaji wa sindao kupungua pia.

Alifahamisha kwamba mafunzo hayo hulengwa zaidi katika kuwapatia Vijana hao ushauri nasaha unaojumuisha uwepo kwa baadhi ya wazazi kwenye vituo hivyo, tiba pamoja na huduma za michezo.

Mwakilishi huyo wa Umoja wa kusaidia mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya na Pombe Tanzania alifahamisha kwamba zipo baadhi ya changomoto zinazokwamisha utekelezaji na malengo ya taasisi hiyo.

Alitaja baadhi changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa huduma rafiki katika Vituo vya Afya jambo ambalo huwakatisha tamaa Vijana walioamua kuacha matumizi ya Dawa za kulevya na kurejea tena baada ya kukosa usimamizi mzuri.

Mapema Sheha wa Shehia ya Fujoni Bwana Said Mgeni Bakari alisema Wananchi wa Kijiji cha Fujoni waliadhimia kusimamia mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya ndani ya Kijiji hicho.

Sheha Said alisema dhamira hiyo ndiyo iliyoibua kuanzishwa kwa Kikundi shirikishi na Polisi jamii kwa lengo la kukabiliana na wimbi la vitendo hivyo vya matumizi pamoja na uuzaji wa Dawa za kulevya na Pombe ndani ya Kijiji hicho.

Alifahamisha kwamba licha ya juhudi zilizochukuliwa na Wananchi hao lakini bado lipo tatizo la ukosefu wa vifaa vya kufanyia kazi pamoja na Ofisi kwa Kikundi hicho cha Polisi Jamii na ulinzi shirikishi Fujoni.

Vijana hao Sita wa Kijiji cha Fujoni walioamua kuachana na matumizi ya Dawa za Kulevya walipatiwa mafunzo ya Miezi sita katika Nyumba ya kurekebishia Tabia kwa watu walioamua kuacha Matumizi ya Dawa za Kulevya ya Mombasa nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Wakati huo huo Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif ameukabidhi Uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } shilingi Milioni 5,000,000/- kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kibanda cha Maji katika Kijiji cha Kinduni.

Ujenzi wa Kibanda hicho una lengo la kuimarisha miundo mbinu ya upatikanaji wa huduma za Maji safi na Salama ndani ya Kijiji hicho chenye changamaoto ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Balozi Seif aliushukuru Uongozi mzima wa Mamlaka ya Maji Zanzibar kwa hujudi uliochukuwa wa kushirikiana na ule wa Jimbo la Kitope katika kuwaondoshea usumbufu wa huduma ya maji safi na salama wananchi wa jimbo hilo.

Alisema juhudi hizo kwa kiasi kikubwa zimechangia kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji katika Vijiji vingi vilivyomo ndani ya Jimbo la Kitope.

Akipokea fedha hizo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kibanda cha Maji Kinduni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Dr. Mustafa Garu alisema miradi mingi ya Maji iliyoanzishwa na Mamlaka hiyo inatekelezwa ili kuwaondoshea usumbufu wa huduma ya Maji Wananchi walio wengi Nchini.

Dr. Garu aliutaja mradi wa Maji uliopata Mkopo kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika uko tayari kufanya kazi na utakuwa ukihudumia kwenye maeneo mengi ya Mji wa Zanzibar.

Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Mamlaka ya Maji Zanzibar aliwahakikishia Wananchi kwamba Mamlaka hiyo itafanya juhudi ya kuwapatia huduma za maji wananchi wakaondelea kuwa na uhaba wa huduma hiyo katika kipindi kinachoingia cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Alisema ule mpango wa kusambaza huduma za maji Mjini na Baadhi ya Vijiji vyenye upungufu wa huduma hiyo kwa kutumia Magari maalum ya kusambazia maji utaendelea kutekelezwa ili kuwapa fursa Wananchi kupata muda wa kufanya mambo mengine ya Kimaisha.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment