Thursday, August 13, 2015
Dar es Salaam.Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii imefafanua kuwa hakuna uthibitisho kwamba mkimbizi
aliyekufa kwenye kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma, alikuwa akiumwa
ugonjwa wa ebola.
Serikali ilitoa taarifa kwa
vyombo vya habari jana baada ya kuzuka hali ya sintofahamu kufuatia kifo
cha mkimbizi huyo kuhusishwa na ugonjwa wa ebola ulioua maelfu wa watu
katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi.
Agosti
9 mwaka huu, Buchumi Joel (39) akitokea katika kambi ya wakimbizi ya
Nyarugusu alipokelewa katika hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni akiwa
na dalili za kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili, hasusan kwenye
fizi, macho na masikio.
Licha ya kupatiwa matibabu ya
hali ya juu kunusuru maisha yake, Buchumi aliaga dunia siku iliyofuata
na kuzikwa chini ya uangalizi wa ofisi ya afya ya mkoa.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo mpaka sasa hakuna
uthibitisho kwamba mgonjwa huyo amekufa kutokana na ebola, licha ya kuwa
na viashiria vya ugonjwa huo.
“Ili kupata uhakika wa
hilo tayari sampuli ya mgonjwa huyu imechukuliwa na kupelekwa kwenye
maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii kwa uchunguzi zaidi, kujua chanzo cha
ugonjwa huu,” ilisema taarifa hiyo.
Wizara hiyo
imeeleza kuwa imejiandaa vyema kudhibiti ugonjwa huo iwapo utaingia
nchini ikiwa ni pamoja na kutengeneza mpango kazi wa miaka mitatu
kuanzia 2015 hadi 2017.
Katika hatua nyingine, wananchi
wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo
uliotikisa dunia katika miaka ya hivi karibuni.
Miongoni
mwa tahadhari hizo ni kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, haja
ndogo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini
mwa mgonjwa mwenye dalili za ebola kupitia sehemu zenye michubuko au
vidonda.
Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali
na kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya anapohisiwa kuwepo mtu
mwenye dalili za ugonjwa huo.
Mpaka sasa zaidi ya watu
11,269 wamepoteza maisha katika nchi za Guinea, Liberia na Siera Leone
tangu kuibuka kwa mlipuko wa ugonjwa huo.
Jinsi ya kujikinga na ebola
-Kunawa mikono kabla na baada ya kula.
-Kusafisha mikono muda wote ili kuepuka kusambaza ugonjwa ikiwa mtu atakuwa amemshika mgonjwa au mazingira yenye maambukizi.
-Kuwahi katika vituo vya huduma za afya mtu anapohisiwa kuwa na dalili za ebola. huu.
Kuepukana na mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa ebola.
Kutumia kemikali za kuua vijidudu kutakasa mikono.
Kuepuka
kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za ugonjwa wa
ebola, badala taarifa za kifo hicho zipelekwe kwa uongozi wa kituo cha
kutoa huduma za afya kwa ushauri.
Habari kutoka:http://www.mwananchi.co.tz
Habari kutoka:http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment