Friday, 3 July 2015

Wanne wahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua albino

                 https://encrypted-tbn1.gstatic.com/images?q=tbn:ANd9GcRwp1dXuojJxQfkcrHy6jHhwoxsuGfHSoEp1EDfA_RoIXSleGQA6g

Na Lauden Mwambona, Mwananchi

Mbeya. Washtakiwa wanne kati ya watano wa kesi ya kumuua mtu mwenye ulemavu wa ngozi (albino) Henry Mwakajila mwaka 2008 wilayani Rungwe, wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa mjini hapa jana.
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Nyanda za Juu Kusini aliwataja waliohukumiwa kuwa ni Hakimu Mwakalinga na Leonard Mwakisole wote wakazi wa Kijiji cha Kiwira wilayani Rungwe na Gerard Kalonge na Asangalwisye Kayuni wa Kijiji cha Mbembati wilayani Ileje.
Mshtakiwa aliyenusurika kwenye kesi hiyo ni Mawazo Figomole ambaye alikuwa mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo ambaye aliachiwa huru baada ya ushahidi kutojitosheleza dhidi yake.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda hiyo, Dk Mary Revila alisema mahakama imeridhika pasipo shaka na ushahidi ulitolewa dhidi ya washtakiwa hao na kwamba, wanastahili kunyongwa hadi kufa huku akisisitiza kwamba ushahidi kwa mshtakiwa namba nne haukujitosheleza.
Awali, ilielezwa mahakamani hapo kwamba Februari 5, mwaka 2008, washtakiwa hao walimteka marehemu Henry akiwa katika Shule ya Sekondari Ukukwe wilayani Rungwe na kwenda kumuua.
Ilielezwa kwamba Mshtakiwa Kayuni ambaye ni mganga wa jadi maarufu kwa jina la Katiti alikutwa na utumbo uliodaiwa kuwa wa binadamu na hatimaye Mkemia Mkuu wa Serikali alithibitisha kwamba ulikuwa wa marehemu Henry.
Ilifafanuliwa kwamba mshtakiwa Kalonge alikutwa na vidole vinne na mifupa 10 iliyodaiwa kuwa ya binadamu na baadaye Mkemia Mkuu wa Serikali kuthibitisha kuwa ilikuwa ya marehemu Henry.
                                                             Habari na: http://www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment