Na Rachel Chibwete
Kwa ufupi
Misime alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu wiki hii ambayo inatarajiwa
kuwa na ugeni mkubwa wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM ambao amesema
kuwa unakadiriwa kuwakusanya watu takribani 10,000.
Dodoma. Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Dodoma, David Misime amewataka wageni wasiokuwa na shughuli muhimu ya
kufanya mkoani hapa kutokuja katika kipindi cha juma hili ili kuepusha
usumbufu utakaojitokeza.
Misime alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu wiki hii ambayo inatarajiwa
kuwa na ugeni mkubwa wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM ambao amesema
kuwa unakadiriwa kuwakusanya watu takribani 10,000.
Alisema ili kuepusha usumbufu utakaojitokeza kama
vile kukosa mahali pa kulala, ni vyema kama mtu hana shughuli ya muhimu
ya kufanya mjini hapa asije mpaka mkutano huo utakapokwisha.
“Kuna wengine wanataka kuja kwa ajili ya ushabiki
tu au kuja kushuhudia tukio zima na hata kama hawatakuja haitawaathiri
kitu hivyo ni vyema wasije ili kuepusha usumbufu,” alisema Misime.
Alisema Jeshi la Polisi limejipanga kuimarisha
ulinzi na usalama kwa wananchi wote watakaofika katika mkutano huo na
kuwataka wananchi kutoa taarifa za viashiria vyovyote vya uvunjifu wa
amani katika maeneo yao.
Aliwataka wamiliki wa nyumba za kulala wageni
kuhakikisha kuwa vitu vyote vyenye thamani vya wateja wao vinatunzwa
vizuri ili kuepusha usumbufu au kupotea kwenye mikono yao.
Ulinzi mkali bungeni
Jana, Polisi waliimarisha ulinzi bungeni kwa
kuongeza idadi ya askari na pia kufunga kipande cha barabara kuanzia
kwenye mzunguko wa kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani kupitia eneo
la Bunge hadi mwanzo wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Tawi la
Dodoma.
Kulikuwa na idadi kubwa ya polisi wa usalama
barabarani, utepe mweupe uliofungwa katika barabara hiyo huku kukiwekwa
kibao kilichoandikwa kwa maandishi mekundu, “barabara hii imefungwa.”
Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Dodoma, David Misime (pichani) alisema kufungwa kwa barabara
hiyo ni miongoni mwa shughuli za usalama.
Habari na: http://www.mwananchi.co.tz
Habari na: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment